The House of Favourite Newspapers

MKE WA MAJUTO: NIPO TAYARI KUOLEWA

IKIWA imepita miezi tisa baada ya kifo cha mchekeshaji maarufu nchini, Amri Athumani ‘King Majuto’, aliyekuwa mke wake, Aisha Yusuph amefunguka kuwa yupo tayari kuolewa. 

 

Mwandishi wa Risasi Jumamosi aliwasiliana naye hivi karibuni na kuzungumza naye mengi kuhusu maisha yake baada ya mumewe kutangulia mbele za haki, ambapo alidokeza kuwa baada ya kulia sana kwa kifo cha mumewe huyo, kwa sasa anaona ni muda mwafaka wa kuingia kwenye ndoa mpya.

 

Mbali na hilo, Aisha ambaye kwa sasa anaishi jijini Tanga katika makazi mengine nje ya nyumba aliyokuwa akiishi na marehemu Mzee Majuto, aliweka wazi mambo mengine ambayo wengi walikuwa hawayafahamu kabla.

 

TUJIUNGE NA AISHA

Risasi Jumamosi: Umesema unaishi Tanga lakini siyo Donge, pale ulipokuwa ukiishi na marehemu mumeo, ni wapi sasa unaishi?

Aisha: Ujue kwetu ni huku huku Tanga, ndipo wazazi wangu walipotokea. Ni mwenyeji sana wa huu mji. Sipo pale tena, lakini naishi hapa hapa Tanga.

Risasi Jumamosi: Vipi huwa unakwenda katika ile nyumba uliyokuwa ukiishi na mumeo? 

Aisha: Ndiyo naenda… hata juzi tu nimetoka hapo.

Risasi Jumamosi: Ukienda pale unajisikiaje ukizingatia wewe na mumeo mlikaa miaka mingi pale?

Aisha: Yaani huwa naumia sana, sana. Sio rahisi kwa sababu ni mtu ambaye nilimzoea sana, hivyo naumia mno siwezi kuelezea.

 

Risasi Jumamosi: Vipi kuhusu watoto wenu?

Aisha: Mtoto wangu mdogo ndio huwa ananiliza kila siku, maana anaweza kuvaa viatu anatoka nje anasema anamsubiri Magufuli (Rais Dk. John Pombe), ampeleke India akamchukue baba yake. Anaamini kuwa atarudi, hajui kabisa kama hayupo. Nikuambie ukweli, Majuto alikuwa akiwapenda sana watoto wake, ndiyo maana inakuwa ngumu kwao kumsahau.

 

Risasi Jumamosi: Kuna zile fedha ambazo Waziri (wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo) Mwakyembe (Dk. Harison) alitoa amri marehemu apewe, vipi mlishapata hizo fedha?

Aisha: Nimesikia hata mimi hilo, lakini kwa sababu kuna mtu alikuwa akisimamia, ngoja nitauliza halafu nitatoa jibu.

Risasi Jumamosi: Inamaana wewe mkewe huna taarifa sahihi kuhusiana na hilo?

Aisha: Hapana kwa sababu kuna mtu alikuwa akisimamia.

Risasi Jumamosi: Muda umeshakwenda sana tangu kifo cha mumeo na unaonekana bado mwanamke mdogo kiumri,vipi akitokea mtu sasa hivi wa kutaka kukuoa, utakuwa tayari?

Aisha: Ni kweli bado nadai lakini sasa hivi naangalia mtu mkweli mwenye kujielewa ambaye atakuwa tayari kwa ndoa. Awe na mapenzi ya dhati, mwenye kumwogopa Mungu. Awe mcha Mungu kweli, anayeswali. Sipendi vijana hawa wa siku hizi, akiwa mtu mzima mwenye kujitambua, mwenye kazi au biashara inayoeleweka, nitakuwa tayari. Kifupi mtu anayejitambua.

Risasi Jumamosi: Sifa gani nyingine ya ziada kwa mume wako huyo mtarajiwa?

Aisha: Awe mchakarikaji, mwanaume anayehangaika. Najua nikipata mwanaume wa aina hiyo, tutaweza kusaka maendeleo pamoja.

Risasi Jumamosi: Haya asante sana kwa ushirikiano wako.

Aisha: Asante nawe pia dada, karibu wakati mwingine

STORI: Imelda Mtema, Risasi Jumamosi

Comments are closed.