The House of Favourite Newspapers

Mke wa Mjeshi Anaswa Akiiba Nyanya Gengeni!

0

UKIWA mume wa mtu, bila shaka utashangazwa kusikia; “Mkeo kanaswa akiiba nyanya gengeni!” Hicho ndicho kilichomtokea afande mstaafu wa jeshi la wananchi (JWTZ) mkoani Morogoro.

 

Mwanajeshi huyo aliyetajwa kwa jina moja la Robart, alipigwa na butwaa hivi karibuni baada ya kupewa taarifa kuwa mkewe, Salma Mohamed, yuko chini ya ulinzi baada ya kunaswa akituhumiwa kuiba nyanya.

 

Mbali na nyanya, Salma alidaiwa kuiba pia vitunguu, nazi na viungo vingine kwenye genge linalomilikiwa na mfanyabiashara Joseph Emmanuel lililopo Mtaa wa Nane Nane, Kata ya Tungi mjini Morogoro.

 

HABARI KAMILI

Taarifa kutoka eneo la tukio ambako mwandishi wetu alifika mapema kushuhudia sekeseke hilo, zinaeleza kuwa, Salma alikutwa na mkasa huo alfajiri mwishoni mwa wiki iliyopita.

 

Inaelezwa kuwa, kunaswa kwa mke huyo wa ‘mjeda’ kulitokana na kile kinachoitwa mtego kutoka kwa mmiliki aliyedai kuchoka kuibiwa bidhaa zake mara kwa mara.

“Kila mara nilikuwa naona bidhaa zinaisha bila kujua, nikawa ninawahisi jirani zangu kuwa ndiyo wananiibia.

 

“Leo nikaona nilale humuhumu kwenye genge langu ili nione kinachochukua bidhaa zangu.

“Alfajiri ya leo ndipo nikamuona huyu mama anakuja na mfuko mkubwa na kuanza kupakia vitu, nikamdaka,” alisema Joseph.

 

KILICHOMKUTA BAADA YA KUNASWA

Kama kawaida zogo linapotokea, wa kwanza kujaa huwa ni watu ambao kwa lugha ya mjini huitwa ‘inzi’ kwa lengo la kuja kushuhudia.

 

Baada ya umati wa watu wakiwemo majirani zake kibiashara na Joseph kufika, walianza kumpa kipigo hevi mtuhumiwa huyo kwa kile walichomtuhumu kuwa ni mwizi.

Hata hivyo, penye wengi huwa haliharibiki neno, baadhi yao walikuwa wakimtetea na haraka kuamua kumuita Mwenyekiti wa Mtaa huo, Zainabu Makarabo ambaye alifika na kujaribu ‘kusovu’ tatizo hilo.

 

Yaliyotazamwa kwa mapana yake ni madai ya mke huyo wa mjeda kutuhumiwa kwa wizi pamoja na utetezi wa Salma kuwa yeye hakuwa mwizi, bali alifika kwenye genge la mtu anayejuana naye (wanajuana kivipi tusijadili sana) na kwamba amekuwa akifanya hivyo mara kwa mara.

Hata hivyo, Joseph alikiri kumfahamu mama huyo, lakini huko kujuana alikosema mwanamke huyo ndiko alikokukana laivu kwa sababu ya kuhofia familia yake kwa sababu ana mke na watoto.

 

MUME WA MTUHUMIWA AITWA ENEO LA TUKIO

Watu hawana dogo, baada ya kuona zogo linazidi, mtu mmoja kati yao aliamua kumtwangia simu mume wa Salma na kumpa taarifa nzima kwamba afike maeneo ya Nane Nane kumshuhudia mkewe kanaswa kwa wizi wa nyanya gengeni.

Taarifa hiyo ilimshtua na kumshangaza afande Robart na kwamba kila alipomdadisi mtoa ujumbe, yeye alisisitiza; “Wewe njoo haraka, wanaweza wakamuua mkeo!”

 

Dakika sifuri kama wasemavyo watoto wa mjini, mume wa Salma alifika eneo la tukio na kukuta watu kama wote wakiwa wamemzonga mkewe.

Kwanza alitaka kuonesha ujeda wake kwa kuwakoromea waliokuwa wamemuweka mtu kati mkewe, lakini aliposomewa tuhuma zake kwa undani, akawa mpole.

 

”Mke wangu umeniacha kitandani saa 11:00 alfajiri, umeniaga unawahi sokoni Mawenzi kununua bidhaa za biashara yako.

“Hapa ndiyo Mawenzi? Na huu wizi ndiyo ununuzi wa bidhaa uliosema,” Robart alimlalamikia mkewe ambaye naye anatajwa kuwa ni mama ntilie wa eneo la Msamvu mkoani Morogoro.

 

Kuonesha kuwa hakufurahishwa na kitendo cha aibu alichokifanya mkewe, mjeda huyo alianza kukoki ngumi ili amtundike nazo, lakini watu wakamwambia; “Acha… acha bwana…huwa hatufanyi hivyo!”

“Jose (mmiliki wa genge) unaweza kuniambia hivi vitu alivyoiba ni shilingi ngapi?” Mjeda aliuliza kwa lengo la kutaka kulipa ili mambo yaishe.

 

MTUHUMIWA AZUA ZOGO UPYA

Baada ya Jose kumtajia mjeda kiwango ambacho anatakiwa kumlipia mkewe, ghafla Salma aliibuka na kupinga kwa kusema kiasi hicho ni kikubwa.

 

“Yaani Jose umeamua kuniaibisha kwa kuniita mwizi, sawa, nakushukuru, lakini kwa kiasi hicho ulichosema hakiwezekani kulipwa.

“Vitu gani vya hela yote hiyo, una dhambi wewe, alilalamika Salma na kuzuia ulipwaji wa gharama zilizotajwa jambo ambalo lilimkera mwenyekiti wa mtaa huyo aliyekuwa akishughulikia kupoza tukio.

 

APELEKWA POLISI

Mwenyekiti wa mtaa huo alipoona mambo yanazidi kukorogeka akasema; “Isiwe tabu..!” Akawapigia simu Polisi ambao walifika eneo la tukio kwa muda mwafaka na kumchukua mtuhumiwa hadi kituo cha kati kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Kitendo hicho cha Polisi kiliwafanya watu waliokuwa wamekusanyika eneo hilo kuondoka eneo la tukio na kwenda kuendelea na mambo mengine.

 

MASHUHUDA WANENA

Wakihojiwa na mwandishi wetu, baadhi ya mashuhuda walionekana kumsikitikia zaidi mjeda kwa kile walichokiita ni kutiwa aibu na mkewe.

 

“Hili ni tukio la aibu hasa kwa mwanaume kwa sababu kama kweli huyo mwanamke alikwenda gengeni kuiba, unajiuliza alikosa nini wakati yeye ni mfanyabiashara na mumewe ingawa ni mstaafu, lakini bado ana uwezo wake,” alisema ljumaa Kombo, mkazi wa Nane Nane.

 

Naye mama Ratifa alisema; “Nashindwa kuelewa kwa sababu huyu dada namfahamu vizuri, sasa sijui niseme alikuwa anaiba ili akapikie chakula au ndiyo tabia yake tu.”

 

STORI: Dustan Shekidele, Morogoro

Leave A Reply