The House of Favourite Newspapers

Mke wa Rais Ahukumiwa Jela Miaka 58

MKE wa rais wa zamani wa Honduras, Porfirio Lobo, aitwaye Rosa Elena Bonilla (52) amehukumiwa kwenda jela miaka 58 mara baada ya kupatikana na hatia ya kutumia Paundi 635,000 (takriban Tsh. Bilioni 1.8) za misaada ya kimataifa na fedha za umma kwa matumizi binafsi.

Mwendesha mashtaka wa nchi hiyo amesema  Bonilla alitumia fedha hizo kwa miaka minne wakati mumewe akiwa rais ambapo alinunua vito vya thamani, alilipia matibabu na karo za watoto wake.

Wakati msaidizi wa Bonilla naye akifungwa miaka 48, wakili wa Bonilla amesema mteja wake hana hatia na kuwa watakata rufaa.

Bonilla alikamatwa Februari 2018 baada ya kufanyika uchunguzi dhidi ya upotevu wa fedha kutoka kwenye mfuko wa umma, zikiwemo fedha za kununulia viatu vya watoto maskini.

Hii si mara ya kwanza kwa mwanafamilia ya Lobo kuhukumiwa, kwani mwaka 2017 mtoto wa kwanza wa rais huyo alihukumiwa kwenda jela miaka 24 kwa kukiri kujaribu kuingiza dawa za kulevya nchini humo.

Comments are closed.