Mkoa wa Katavi Wapiga Hatua Mapambano ya Virusi vya Ukimwi (VVU)
MKOA wa Katavi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali umefanikiwa kutekeleza afua mbalimbali za kupambana na UKIMWI ambapo mkoa umefanikiwa kufikia malengo ya 95 ya kwanza kwa 111.1% kufikia malengo ya 95 ya pili kwa 96.9%.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dkt. Omari Sukari katika maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani iliyoadhimishwa kimkoa katika Shule ya Msingi Kasekese wilayani Tanganyika.
Dkt. Sukari ameeleza kuwa idadi ya vituo vya kutolea huduma za tiba na malezi kwa watu wanaoishi na VVU (CTC) imeongezeka kutoka vituo 34 mwaka 2020 hadi vituo 51 kufikia Septemba, 2022.
Ameongeza kuwa idadi ya vituo vya kutolea huduma za ushauri nasihi na upimaji wa VVU imeongezeka kutoka vituo 76 mwaka 2020 hadi vituo 83 kufikia Septemba 2022.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Katibu Tawala wa mkoa wa Katavi Hassan Rugwa akimwakilisha mkuu wa mkoa huo amewataka viongozi, wataalamu pamoja na wadau mbalimbali kuelekeza nguvu zaidi katika kutoa elimu juu ya umuhimu wa kupima virusi vya UKIMWI na kutambua hali ya afya zao ili kuchukua hatua stahiki na kwa wakati.
Rugwa ameeleza kuwa kutokana na hali ya maambukizi ya VVU kuwa 5.9% katika mkoa wa Katavi, ambayo ni kiwango cha juu ikilinganishwa na kiwango cha maambukizi ya VVU cha Taifa ambacho ni 4.7% ni muhimu kama mkoa kujipanga.
Katika maadhimisho hayo ya siku ya UKIMWI Duniani iliyobeba kaulimbiu inayosema Imarisha Usawa yamefana katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kasekese ambapo shughuli mbalimbali zikiwemo upimaji wa Afya pamoja na Elimu kuhusu masuala mbalimbali ya Afya zimefanyika kwa Mafanikio makubwa.