The House of Favourite Newspapers

Mkubwa Fella; Mheshimiwa diwani fundi wa utunzi Yamoto Band

0

said fella

Imelda mtema na Mayasa Mariwata,Risasi Jumamosi

SAID Fella ‘Mkubwa Fella’ si jina geni kwa wapenzi wa muziki Bongo kwa kuwa ni mmoja kati ya wadau muhimu wa Muziki wa Bongo Fleva.

Ametoa sapoti kubwa kwa wasanii mbalimbali na hadi sasa anaendelea kuwasimamia Wanaume TMK sanjari na Yamoto Band, vijana wanaofanya vizuri kwenye ulimwengu wa dansi la kisasa.
Fella ambaye makazi yake ni Mbagala Kilungule iliyopo Wilaya ya Temeke jijini Dar amesema ndoto yake kubwa aliyokuwa nayo tangu zamani ilikuwa ni kuifanya Wilaya ya Temeke iwe katika ramani ya muziki kitu ambacho kwa kiasi fulani amefanikiwa.

fella (1)
Katika mazungumzo yake na waandishi wetu hivi karibuni, Fella amefafanua mambo mbalimbali aliyopitia hususan kwenye muziki na udiwani akiwakilisha Chama cha Mapinduzi (CCM):

Kwa nini aliamua kugombea udiwani?
“Unajua udiwani ni kazi ya kijamii kabisa, tangu awali nilikuwa na nia na mpango thabiti kabisa wa kuja kuwakomboa wanakilungule ndiyo maana nilijipanga na nikatimiza ndoto yangu.”

fella (2)Amewezaje kufanya kazi ya siasa na muziki?
“Mimi naona kazi zote zinafanana na kila unachokifanya kinaigusa jamii kwa kuwa muziki wangu ni kwa ajili ya kuinua vipaji kwa jamii na hata huku kwenye udiwani ni kwa ajili pia ya kutatua matatizo yanayowasumbua sana wakazi wa huku.

Nini ameshafanya tangu apewe udiwani?
“Kwa kweli namshukuru Mungu sana tayari nimeshachimba visima na nimejenga Barabara ya Kampalange mpaka Barabara ya Kosi tena kwa kutumia hela yangu ya mfukoni na sasa hivi wakazi wa huku hawana shida ya maji kabisa kama mwanzo.”

Ana mpango wa kugombea Ubunge baadaye?
“Kwa kuwa lengo langu ni kuwainua wananchi wangu wa Temeke nina mpango huo baadaye Kikubwa namuomba Mungu anipe uzima, ninapenda kazi za kuwatumikia wananchi.”
Ni kweli yeye ni mtunzi wa nyimbo zote za Yamoto?
“Ndiyo, si mtunzi bali kuna sehemu naimba kidogo na kwa kweli namshukuru sana Mungu kwa hilo.

Kwa nini hapendi kuonekana runingani akiimba?
(Kicheko) Wanamuziki wangu wakinifagilia kidogo kwa kibwagizo cha mkubwa Fella mimi naridhika kabisa kwa hilo.

Mbali na Yamoto, ana mpango wa kuanzisha kundi jingine?
“Ndiyo, tena hilo litakuwa hatari zaidi ni la vijana wadogo, kwa kweli wako vizuri sana linaitwa Salamu Temeke mimi mwenyewe nawaogopa. Wanaimba hatari. Muda si mrefu Watanzania wataanza kuwasikia.

Ana mpango gani kwa vijana wenye vipaji?
“Mpango ni mkubwa ila tu kwa ajili ya maisha tunaanza kutoa vijana kidogokidogo kwa sababu huwezi kuwakusanya wote kwa pamoja itakuwa haina maana, unaweza kushindwa kuwasimamia wote ikawa matatizo,” alimalizia Fella.

Leave A Reply