The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu – 4

1

ILIPOISHIA…
WATOTO wawili wamependana, hawa ni Kevin na Catarina, binti mzuri mwenye umbile la kuvutia ingawa bado ni mdogo na ana ndoto za kuwa mwanamitindo maarufu duniani huku Kevin akitamani kuwa mhandisi ingawa baba yake anapenda awe daktari.

Wako katika mapenzi mazito ingawa hakuna aliyewahi kufunguka na kumweleza mwenzake hisia alizokuwa nazo, wazazi wa Catarina wakaligundua hilo na kuamua kumhamishia mtoto wao nchini Uganda kuendelea na masomo, lengo likiwa ni kumtenganisha na Kevin kabisa.

Catarina akiwa nchini Uganda akili yake yote ikiwa kwa Kevin, ambaye pia anateswa na fikra za Catarina.

Shule ilipofungwa binti huyo alirejea Tanzania, siku ya kwanza tu alipofika alisimama kwenye veranda ambako siku zote alipatumia kuwasiliana na Kevin na kuanza kumwita, baba yake akatokeza na kumwambia bado Kevin alikuwa yupo shuleni St. Joseph alikokuwa akisoma na akampa taarifa za mateso ya hisia aliyokuwa nayo.
Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…

TAARIFA za baba yake Kevin kwamba mwanaye alikuwa akiteseka kwa fikra juu yake, zilimsikitisha sana Catarina. Ukimya uliotokea kati yao kwa muda mrefu akiwa shuleni Uganda ulimfanya ahisi pengine Kevin alishamsahau na kuendelea na maisha mengine, kusikia alikuwa akiteseka juu yake kuliyachipusha mapenzi aliyokuwa nayo kwa Kevin maradufu, akatamani kumwona wakati huohuo.

“Nikienda shuleni kwao naweza kuruhusiwa kumwona?”
“Hapana, shule hiyo ni wakali sana, hawaruhusu kabisa mtoto kuonana na watu wa nje mpaka siku ya kutembelewa, hata mimi mwenyewe nikienda pale siwezi kumwona, msubiri tu afunge shule, kwani wewe utakuwepo hapa mpaka lini?”
“Mwezi wa nane!”

“Basi mtaonana mwezi wa saba akifunga, zimebaki siku chache sana.”
Kwake zilikuwa siku chache lakini kwa Catarina ilikuwa ni miaka, asingeweza kuvumilia wiki tatu bila kumtia Kevin machoni, moyoni mwake alipata suluhisho la nini cha kufanya, akapanga siku iliyofuata wazazi wake wakiondoka kwenda kazini, yeye atoroke kwenda mjini shule ya St. Joseph kujaribu kumwona Kevin.

Aliporejea ndani ya nyumba yao aliketi sebuleni na kuongea na baba yake ambaye aliendelea na nasaha zake za kila siku juu ya Kevin, akimtaka ajiepushe naye kabisa bila kuelewa kilichokuwa kikiendelea moyoni mwa binti huyo wakati huo, maongezi hayo hayakumvutia kabisa Catarina ambaye saa nzima baadaye alimuaga baba yake na kuelekea chumbani ambako hakuna alichokifanya zaidi ya kumuwaza Kevin, huku akibubujikwa machozi na kulowanisha mashuka.

Mama yake aliporejea kutoka kazini saa kumi na mbili jioni, ndipo Catarina aliamshwa na kutoka chumbani baada ya kuoga na kujisikia vizuri, alifurahi kumwona tena mama yake, lakini kilichomkera baada tu ya salamu ni nasaha dhidi ya Kevin huku akisisitiziwa kusoma kwa bidii na kuachana na masuala ya mapenzi katika umri mdogo.

“Siyo mapenzi mama!”
“Ni nini?”
“Nampenda tu, simaanishi kufanya naye tendo la ndoa.”
“Wote tulianza kwa kusema maneno hayo hayo, mwisho wa siku tukajikuta tunafanya jambo ambalo hatukulipanga!”

“Niamini mama, Kevin wala hajui kwamba mimi ninampenda.”
“Hujawahi kumweleza?”
“Sijawahi, hata yeye hajawahi kunitamkia, sisi ni marafiki tu, yapaswa mtuamini.”
“Marafiki mnachanganyana akili kiasi hicho? Maana hata mwenzako naye nasikia huko shuleni ni yaleyale!”

Usiku wa siku hiyo ulikuwa mrefu mno kwa Catarina, hakupata usingizi kabisa, akitamani asubuhi iwadie lakini kitendo hicho kilitokea taratibu mno kuliko siku nyingine zote, saa tisa na nusu usiku ndipo alipata usingizi na kuzinduka saa tatu asubuhi wazazi wake wakiwa tayari wamekwishaondoka kuelekea kazini.

Wafanyakazi wa ndani walimwandalia kifungua kinywa ambacho alikitumia baada ya kuoga na kujiandaa kwa safari, akatoka hadi kituo cha basi ambako alipanda na kusafirishwa hadi katikati ya Jiji la Dar es Salaam maeneo ya Posta ilipokuwa shule ya St. Joseph, saa yake ya mkononi ilisomeka saa nne na nusu wakati anafika kwenye lango la kuingilia ndani ya shule hiyo, mlinzi alikuwepo kumuuliza maswali.

“Nimekuja kumwona Kevin Mdoe!”
“Anasoma kidato cha ngapi?”
“Cha kwanza.”
“Leo siyo siku ya kuona wanafunzi.”

“Nina ujumbe natakiwa kumpa.”
“Labda uende ofisini kwa walimu ukawaeleze lakini yeye mwenyewe huwezi kumwona.”
“Sawa, naomba niende huko ofisini kwa walimu.”

St. Joseph ilikuwa ni shule iliyosifika si Dar es Salaam peke yake bali Tanzania nzima kwa malezi ya watoto, ilifaulisha sana watoto katika matokeo ya kidato cha nne na cha sita, ndiyo maana wazazi wengi waliikimbilia ingawa sheria zake zilikuwa kali mno.

Mtoto akishaingia kwenye lango la shule hiyo haikuwa rahisi kumwona mpaka wakati wa likizo au siku za kutembelea watoto na kupata ripoti kutoka kwa walimu wao, Catarina alipoingia kwenye ofisi ya mwalimu wa Taaluma na kueleza shida yake ya kumwona Kevin akisingizia ni dada yake, alikataliwa kabisa, akabembeleza lakini haikuwezekana, mwisho wa siku akashukuru na kuondoka moyoni akiwa amechukia.
“Umemwona?” Mlinzi alimuuliza lakini hakumjibu kitu.

Akiwa nje ya lango alifikia uamuzi wa kusubiri mpaka muda wa watoto kuondoka shuleni kwenda kwenye mabweni yao, taarifa alizokuwa nazo ni kwamba wanafunzi wa St. Joseph walisoma hapo lakini mabweni yao yalikuwepo maeneo ya Mtoni kwa Aziz Ali, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na ilikuwa lazima wabebwe kwa mabasi ya shule kupelekwa huko baada ya masomo.

“Nitasubiri hapa mpaka wakati wanaondoka,” alisema Catarina akiwa ameketi kwenye ngazi za kuingilia kwenye duka la kuuza vitabu lililoko nje ya shule hiyo.

Ilikuwa tayari imeshagonga saa tano kamili, saa nne kabla magari hayajaanza kusomba wanafunzi kupeleka mabwenini, Catarina alichagua kuvumilia mpaka muda huo ufike ili amwone Kevin, hata kama angempungia tu kwa mbali na kuliona tabasamu lake, ingetosha.

Alikunywa soda kwenye kibanda cha jirani kisha kurejea na kuketi kwenye ngazi mpaka saa tisa kamili ndipo akaona lango limefunguliwa na magari yameanza kutoka moja baada ya jingine, macho yake yakipitia kila mwanafunzi aliyekuwa ameketi ndani kwa kasi ya ajabu, yakimwangalia mtu mmoja tu; Kevin.

Gari la tatu lilipokuwa linatoka, alimwona Kevin ameketi kiti cha mbele ya mlango, moyo wake ukalipuka, akashindwa kuvumilia na kuanza kupiga kelele akimwita huku akilikimbiza basi hilo, watu waliomwona walimshangaa! Kevin aliposikia jina lake likiitwa aligeuka kuangalia nje, akamwona Catarina akikimbilia, basi alichokifanya ni kuamua kuruka kupitia dirishani, wenzake walijaribu kumshika lakini walishachelewa, akaangukia kichwa kwenye barabara ngumu ya lami!

Damu zikaanza kumtoka puani, mdomoni na masikioni, tayari Catarina alishafika na kuanguka juu yake akimkumbatia kwa uchungu, huku akisema maneno: “Don’t die! Don’t go Kevin, I love you very much!” yaliyomaanisha: “Usife, usiondoke Kevin, ninakupenda mno!” Watu walifika na kumvuta, wakamnyanyua Kevin ambaye alikuwa hajitambui na kumpakia ndani ya gari jingine, wanafunzi wote walikuwa wakilia na walimu pamoja na mkuu wa shule walishakusanyika.

“Mungu wangu! Nilishawaza kuweka nyavu kwenye haya madirisha ya magari ya shule muda mrefu!” Mtawa ambaye ndiye alikuwa mkuu wa shule alitamka maneno hayo akimwangalia Kevin akipakiwa ndani ya gari ili awahishwe Hospitali ya Muhimbili.

Catarina ndiye aliyeokota mfuko wa Kevin wa madaftari, aliendelea kulia akiwa ameubeba mgongoni, gari liliondoka na Kevin na kumwacha hapo, alichofanya ni kukodisha teksi na kumwamuru dereva awahi Muhimbili, alikuwa mdogo kwa umri lakini akili yake ilikuwa ni ya kikubwa kwa sababu ya kuishi na watu wazima kwa muda mrefu wakati anakua.

JE, nini kitaendelea Muhimbili? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi Jumatano.

1 Comment
  1. reginah says

    ITS GUD STORY

Leave A Reply