The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu-56

0

ILIPOISHIA…

Kwa kutumia washirika wake waliobaki nje, Jackson Motown anafanya kila kinachowezekana kuhakikisha Catarina anakufa ili kupoteza ushahidi wote kwani hayuko tayari kuingia mikononi mwa sheria. Anamtumia Dracula ili kufanikisha mpango huo akimuahidi kiasi kikubwa cha fedha.

Dracula anapanga mpango mzima kwa kushirikiana na Ofisa wa FBI ambaye ni kibaraka wao ili kukamilisha zoezi hilo. Anaingia nyumbani kwa Catarina kama Padri Coronel Garsia kukiwa hakuna hata mtu mmoja, si FBI wala Catarina aliyemshtukia. Anajifanya mtoa nasaha na kumfanyia maombezi msichana huyo.
Je unajua nini kiliendelea?
SONGA NAYO…
N
yumbani, wazazi wa Catarina hawakuwa na amani hata kidogo, muda ulikuwa ukienda mbele lakini hakukuwa hata na dalili za binti yao kurejeshwa nyumbani. Walibaki wakiulizana kwani halikuwa jambo jepesi mtu apelekwe sehemu mpaka wakati ambao giza lilianza kuingia hakuwa amerudishwa.
Mioyo yao ilikuwa na hofu kubwa, walibaki kuwa na wasiwasi mno. Kuna kipindi walishauriana kwamba lingekuwa jambo zuri kama wangewapigia simu FBI na kuwauliza juu ya kilichokuwa kikiendelea lakini wakaona wasubiri kwanza kwa kujipa moyo kuwa inawezekana watu hao walikuwa njiani kurudi nyumbani hapo.
“Hatutakiwi kuwa na hofu mke wangu,” baba yake Catarina, mzee David alimwambia mke wake kwa sauti ya chini.
“Ila kutakuwa na tatizo, ni lazima tujue nini kinaendelea, nahisi kwamba vijana wa Jackson Motown watakuwa wamemteka binti yetu,” alisema mama yake Catarina, maumivu aliyoyasikia moyoni mwake, yalikuwa makali yaliyoyafanya machozi yake kuanza kutiririka mashavuni mwake.
Mzee David akamsogelea mkewe na kuanza kumbembeleza kwa kumpigapiga mgongoni. Yeye mwenyewe alikuwa na hofu moyoni mwake lakini hilo hakutaka mke wake afahamu kwani alijiona kuwa mtu pekee ambaye alitakiwa kumfariji mkewe, kama yeye alikuwa na hofu, nani angemfariji mwenzake?
Waliendelea kujipa moyo kwamba ndani ya dakika chache, Catarina, Padri Coronel na Afisa wa FBI, Clarence wangerudi nyumbani hapo lakini haikuwa hivyo. Sekunde zilikwenda mbele, dakika zilikatika lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyefika nyumbani.
Hawakutaka kusubiri tena, walichokifanya ni kupiga simu makao makuu ya FBI na kuwaambia kile kilichokuwa kikiendelea, hawakutaka kuficha, waliwaambia kuhusu wasiwasi waliokuwa nao hivyo afisa mmoja wa FBI aliyekuwa makao makuu kumpigia simu Clarence, kitu cha ajabu kabisa, simu haikuwa ikipatikana.
“There is problem somewhere,” (kuna tatizo sehemu) alisema afisa mmoja wa FBI.
“What is it?” (Ni lipi hilo?)
“I don’t know yet, but we have to know what is going on,” (bado sijui, lakini tunatakiwa kujua nini kinaendelea), alisema afisa huyo.
Hawakutaka kuamini kile walichoambiwa, walichokifanya ni kuwaagiza maofisa wengine wa FBI waende katika nyumba aliyohifadhiwa Catarina ili kuona kama kile walichoambiwa kama kilikuwa na ukweli wowote ule.
Ilikuwa safari iliyochukua saa moja njiani, wakafika, hawakumkuta Catarina, wazazi wake walikuwa ndani huku wakiwa wamekumbatiana, muda wote, mama yake Catarina alikuwa akilia tu huku akimwambia mumewe kwamba Jackson Motown alikuwa amemuua binti yake.
“She is safe,” (yupo salama) alisema mmoja wa FBI.
“Are you sure?” (una uhakika?) aliuliza mama yake Catarina.
“We are trying to call our officer but we can’t reach him. You don’t have to worry, she is safe,” (Tunajaribu kumpigia afisa wetu lakini hatumpati. Msiwe na hofu, yupo salama) alisema afisa mmoja wa FBI huku yeye mwenyewe akiwa hana uhakika kama huko alipokuwa Catarina alikuwa salama au la.
****
Moyo wa Catarina haukuwa na amani hata kidogo, hakujua kitu gani kilichokuwa kikiendelea mahali hapo. Giza liliingia lakini badala ya kurudi nyumbani, walizidi kwenda mbele zaidi.
Muda wote Catarina alipojiuliza juu ya mahali walipokuwa wakielekea, bado afisa wa FBI, Clarence alizidi kumtoa wasiwasi lakini bado msichana huyo hakumwamini kabisa. Mbele yake akakiona kifo, hakuamini kama kweli alitakiwa kuwa na uhuru mpaka hatua hiyo waliyofikia.
“Let me go back home, please” (Tafadhali naombeni nirudi nyumbani), alisema Catarina huku akitaka kufungua mlango.
Kutoka pale gari liliposimama mpaka wanaifikia ile kona wala hawakuchukua sekunde nyingi wakafika na kisha gari kusimamishwa. Catarina alibaki akishangaa, hakujua mahali walipokuwa na hakujua sababu iliyowapelekea kusimama sehemu hiyo.
Hakukuwa na usalama mahali hapo, kila alipoyapeleka macho yake huku na kule, hakukuwa na mtu yeyote yule. Alichokifanya Clarence ni kuzima gari hilo kitu kilichomuongezea Catarina hofu moyoni mwake.
“What are we doing here?” (tunafanya nini hapa?) aliuliza msichana huyo, hakukuwa na mtu aliyejibu swali hilo zaidi ya Clarence kuachia tabasamu pana.
Wakati Catarina akiwa ameduwaa, mara akashtukia mlango wa upande aliokuwa yeye ukifunguliwa na mwanaume mwenye misuli mingi kisha kumtoa ndani ya gari lile. Catarina alijitahidi kupiga kelele akiomba msaada lakini hakukuwa na mtu aliyemsaidia zaidi ya Padri Coronel ambaye ndiye alikuwa Dracula akicheka kwa dhihaka kubwa.
“Umetusumbua sana,” alisema Dracula huku akiteremka kutoka ndani ya gari.
Wanaume wengine wanne wakatokea sehemu walipokuwa wamejificha na kisha kumfuata Catarina, wawili wakamshikilia. Afisa wa FBI, Clarence akateremka kutoka garini, mpango waliokuwa wameufanya tayari ulifanikiwa na kitu alichokuwa akikisubiri ni kulipwa kiasi cha fedha walichokubaliana kama malipo ya kazi kubwa aliyoifanya.
“Malipo inakuwaje?” aliuliza Clarence huku akimwangalia Dracula.
Hata kabla mwanaume huyo hajajibu swali lolote, Clarence akashtukia akipigwa mtama na mtu aliyetokea nyuma yake. Kwa kuwa lilikuwa pigo la kushtukiza, akashindwa kujua afanye nini, mwanaume mwingine naye akatokea na wote kuanza kumshambulia, lengo lao kubwa lilikuwa ni kutaka kumlegeza kwanza.
Walipoona wamempiga pasipo kumjeruhi sehemu yoyote kwa nje, wakamchukua na kumuingiza ndani ya gari, humo, wakachukua chuma kizigo na chenye makali na kumpiga nacho kwenye paji la uso, kichwa kikapasuka na damu kutapakaa kwenye kioo, huo ukawa mwisho wa Clarence, mwili wake wakaufunga mkanda na pale mbele kwenye kioo napo wakakupasua kuonyesha kama kulikuwa na kitu kilichopasua kioo na kukipiga kichwa chake.
Kila kitu kilichokuwa kikiendelea, Catarina alikuwa akikishuhudia kwa macho yake, muda wote alikuwa akipiga kelele kwa hofu kwani alijua fika kwamba mara baada ya hao watu kumalizana na Clarence, wangehamia kwake.
“Naombeni niondoke, padri…padri…naombeni niondoke,” alisema Catarina huku akiwa ameshikwa pande zote mbili. Alilia lakini hakukuwa na aliyemjali, kila mmoja alikuwa bize na mambo yake.
“Nani padri?” aliuliza Dracula huku akionekana kuwa na hasira.
“Nakuomba, kumbuka wewe ni mtumishi wa Mungu, naomba unionee huruma,” alisema Catarina, hakuacha kulia, alitia huruma lakini huo haukuwa muda wa kumhurumia mtu yeyote yule, walikuwa hapo kwa ajili ya kufanya kazi waliyotumwa tu.
Walipomalizana na Clarence, katapila lililokuwa mbali na eneo hilo likaanza kuletwa mahali pale. Catarina hakujua ni kitu gani kiliendelea na katapila lile lakini lilipofikishwa eneo hilo, akachukuliwa na kisha kulazwa chini huku akiwa amefungwa kamba.
Kabla ya kufanya walichotaka kumfanyia Catarina, Dracula akachukua chuma kizito na chenye makali na kisha kujikata katika mkono wake wa kushoto huku lengo likiwa ni kuwafanya FBI waamini pale atakapowaambia kwamba kulikuwa na ajali imetokea, Catarina na Clarence wamekufa na yeye kujeruhiwa vibaya.
Alisikia maumivu makali lakini hakujali, ilikuwa ni lazima kufanya hivyo kuitia upofu FBI. Alipomaliza, akamwambia dereva wa lile katapila kuanza kuligonga lile gari alilokuja nalo pamoja na Catarina, tena haswahaswa upande ule aliokalia msichana huyo ili pale watakaposema kwamba alijeruhiwa vibaya kabla ya kufa, kila mtu aamini hilo.
Hakukuwa na muda wa kupoteza mahali hapo, harakaharaka katapila lile likaanza kuligonga lile gari, yote hayo yalishuhudiwa kwa macho ya Catarina na kugundua kwamba hata huyo padri hakuwa mtumishi wa Mungu kama alivyojua bali alikuwa muuaji kutoka katika Kundi la Jackson Motown.
“Naomba msiniue, padri, wewe ni mtu wa Mungu! Naomba msiniue…” alisema Catarina.
“Nani mtumishi wa Mungu?” aliuliza Dracula, hata vazi la kipadri akaliweka pembeni.
Gari lile lilipopondwa vya kutosha na kuonekana dhahiri kupata ajali, Dracula akachukua nyundo kubwa, akawataka vijana wale wamshikilie vizuri Catarina pale chini alipokuwa huku lengo lake likiwa ni kumpiga na nyundo ile kichwani na kisha mwili wake wauingize ndani ya gari.
“Naomba msi…” alisema Catarina lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, Dracula akaingilia.
“Nyamazaaa…” alisema mwanaume huyo. Pale chini, Catarina akalazwa chali na moja kwa moja Dracula kunyanyua nyundo juu na kutaka kuishusha kichwani mwa Catarina. Muda wote msichana huyo alikuwa akilia, hakukuwa na aliyejali.
“Kawasalimie wote huko kuzimu,” alisema Dracula huku akijiandaa kuishusha nyundo ile kichwani mwa Catarina ambaye alikuwa akipiga kelele za kuomba asiuawe.
Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi Jumatano.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply