The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu 60

0

ILIPOISHIA…
WAZAZI wa Catarina, siku moja wakiwa wanaangalia taarifa ya habari, wanashangaa kuona Serikali ya Marekani ilikuwa imekata rufaa katika kesi ya Jackson Motown na tayari yeye na wenzake wote walikuwa wamekamatwa na kuwekwa mahabusu baada ya ushahidi muhimu wa kesi hiyo kupatikana.

Siku nne baada ya taarifa hiyo, ilikuwa ni siku ya kesi kusikilizwa tena, wanakuwa watu wa kwanza kufika mahakamani ambako wanashuhudia majira ya saa mbili kamili asubuhi Jackson Motown akiletwa ndani ya gari la polisi na kushushwa akiwa na wenzake wanne waliotembea wakiwa wameshikiliwa sababu walikuwa ni vipofu.

Wanaingizwa kwenye chumba maalum na baadaye mahakama ilipokuwa tayari wanaingizwa kwenye chumba cha kuendeshea kesi, wazazi wa Catarina pamoja na wale wa Kevin walikuwa katikati ya watu wasiopungua mia moja ndani ya chumba hicho.

Upande wa mashtaka unapewa nafasi ya kuelezea sababu ya kukata rufaa haraka, watu wote wakiwa kimya, majaji wakiandika maelezo yote kwenye kompyuta zao! Inamshangaza kila mtu aliyesikia taarifa kwamba mashahidi wawili muhimu walikuwa wamepatikana na walikuwa tayari kusimama katikati ya mahakama hiyo kutoa ushahidi dhidi ya Jackson Motown na wenzake.

Ghafla shahidi wa kwanza anajitokeza. Ni Kevin. Anapojitokeza tu, mshagao mkubwa na kelele zinasikika, huku mama yake akimkumbatia kwa nguvu na kuanguka wote chini akiwa haamini kilichotokea kwa sababu mwanaye walishamzika. Taharuki inasababisha jaji ashindwe kuelewa kinachoendelea, anaamuru mahakama iende kwenye mapumziko ya muda wa dakika ishirini kabla ya kuendelea tena.
Je, nini kitaendelea?
SONGA NAYO…

TAYARI polisi walishafika karibu yao na kuwatenganisha, Kevin akaondolewa kwa mama yake akibubujikwa na machozi ya furaha, ndivyo ilivyokuwa kwa mama na baba yake Catarina, wao pia walikuwa wakilia! Hakuna aliyekuwa tayari kuamini kilichotokea mbele ya macho yao, waliona ni kama ndoto, kwamba wangezinduka baadaye na kujikuta wamelala kitandani.
“Mama! Catarina yuko wapi?” aliuliza Kevin kwa sauti huku akiingizwa ndani ya kizimba.
“Tutaongea mwanangu!”
Kila mtu ndani ya chumba cha mahakama alikuwa kwenye mshangao lakini aliyekuwa amepigwa na ganzi mwili mzima kwa kilichotokea alikuwa ni Jackson Motown, yeye pia alikuwa akilia, akiwa haamini kama macho yake yalikuwa yamemwona Kevin! Hakuwa na jibu ya nini kilitokea mpaka akawa hai wakati alishalipuka ndani ya nyumba ya mzee Thomas Edmund.
“Who is that witness?”(Huyo shahidi ni nani?) Ilikuwa ni sauti ya Dragon akimuuliza Jackson Motown, hakuwa na uwezo wa kuona.
“We are doomed!”(Tumekwisha!)
“Why?” (Kwa nini?)
“You can’t believe, this bastard is alive!”(Huwezi kuamini, huyu mwanaharamu yuko hai!)
“Who?” (Yupi?)
“Kevin!”
“Oh my God! Kevin is alive? But Dracula claimed that he bombed him?” (Oh Mungu wangu! Kevin yuko hai? Lakini Dracula alidai kumlipua kwa bomu?)
“He lied!”(Alidanganya!)
“So what are we going to do?”(Sasa tutafanya nini?)
“No way! The needle is ours!”( hakuna la kufanya! Sindano ya sumu ni halali yetu!)
Kabla hawajaendelea na maongezi yao, mlango wa kuingia mahakamani ulifunguliwa, askari akapiga kelele kuashiria kwamba jaji alikuwa anaingia, watu wote wakakaa tayari, sekunde zisizozidi tano baadaye Jaji Johnson Macline akaingia huku akitembea kwa madaha.
Alikuwa ni jaji aliyeheshimiwa sana nchini Marekani kwa hukumu zake, hakuwa na upendeleo hata kidogo, watu wengi walidai ndiye jaji pekee nchini Marekani ambaye hakuwa na doa la rushwa! Alitumika sana katika kesi ngumu za dawa za kulevya na ugaidi, mara ya mwisho alimhukumu Mmarekani raia wa Colombia aliyejihusisha na biashara ya unga aina ya Cocaine kutokea Brazil miaka mia moja na hamsini na tano jela, hukumu ambayo hakuna jaji yeyote aliyewahi kuitoa katika historia ya Jiji la New York, jina lake likawa limeingia kwenye historia.
Mahakama iliamua kumpa kesi ya Jackson Motown sababu ya historia yake, kila mtu aliamini haki ingetendeka kwani pamoja na utajiri wake na ushawishi mkubwa aliokuwa nao, Jackson Motown asingeweza kumrubuni Jaji Johnson Macline ili aweze kujinasua na kitanzi.
Aliketi kwenye kiti chake, akavaa miwani yake kisha kuruhusu shahidi asimame na kuongozwa na wakili wa Serikali kutoa ushahidi wake, Kevin alisimama na kuanza kusimulia historia nzima ya maisha yake tangu alipokutana na Catarina, uhusiano kati yao, alivyoondoka nchini Tanzania kwenda Afrika Kusini kufanya kazi ya uanamitindo na hatimaye kuhamia New York ambako baadaye mawasiliano kati yao yalipotea, akaamua kusafiri hadi Marekani kufuatilia.
“Nikisaidiana na Ubalozi wa Tanzania, Washington DC niligundua kuwa Catarina alikuwa kwenye matatizo makubwa baada ya kukutana na wakala wake Mario Pizaro, baadaye Mario alikufa katika mazingira ya kutatanisha, ndipo nikaamua kumfuatilia Jackson Motown huko Miami, nikatekwa na watu wake na kupelekwa porini kwa lengo la kuuawa, lakini Mungu hakupanga nife, kwani kwenye buti ya gari walimonifungia kulikuwa na galoni yenye tindikali, hivyo walipofungua tu ili wanitoe niliwamwagia tindikali hiyo, ndipo nikajiokoa!”
“Watu uliowamwagia tindikali ukiwaona unaweza kuwatambua?”
“Ndiyo.”
“Wapo hapa?”
“Ndiyo.”
“Wako wapi?”
“Ni Jackson Motown pamoja na washirika wake walioharibiwa sura na tindikali!”
“Mheshimiwa jaji inatosha!” Wakili wa Serikali Lilian Mathew alisema.
Upande wa utetezi ulianza kumuuliza Kevin maswali mengi kuhusu alichokiongea, akajibu kwa ufasaha na alipomaliza akaondolewa kizimbani na kupelekwa kwenye chumba maalum, muda mfupi baadaye shahidi wa pili naye akaruhusiwa kuingia, huyu alikuwa ni mzee Thomas Edmund ambaye katika ushahidi wake alieleza kinagaubaga jinsi alivyokutana na Kevin na habari aliyomsimulia ndipo akapanga mpango wa kuudanganya ulimwengu kwamba amekufa ili amfiche kwa usalama wake, pia akaeleza namna alivyolipata bomu na maiti, akalilipua maiti ikiwa ndani yake, ili Jackson Motown na washirika wake waone kama amekufa wakati alikuwa amemficha nyumbani kwake katikati ya Jiji la New York.
Kila mtu ndani ya chumba cha mahakama alikuwa kimya wakati Thomas Edmund akitoa ushahidi wake, Jackson Motown alikuwa akilia kama mtoto mdogo, furaha yote aliyoipata baada ya kuachiwa huru mara ya kwanza ilikuwa imeyeyuka! Sasa hakuwa na namna tena ya kujinasua, sifa za Jaji Johnson Macline zilimtisha, alikuwa hahongeki wala hashawishiki kwa kitu chochote, kitanzi alikiona mbele yake.
“We are finished!” (Tumekwisha!) Jackson Motown alimwambia Dragon.
“Sure! There is no escape!”(Hakika! Hakuna jinsi ya kuchomoka!)
“We better get ready for the needle!”(Ni bora tujiandae kwa sindano ya sumu!)
Upepo ulishabadilika ndani ya chumba cha mahakama, watu walionyesha chuki ya wazi kabisa kwa Jackson Motown, hakuonekana asiye na hatia tena, bali muuaji aliyeua watu wengi wasio na hatia! Tamaa ya watu wote ilikuwa ni kuona anahukumiwa kifo bila kupoteza wakati, wote walikuwa kimya wakimsubiri jaji apange siku ya kutoa hukumu.
Ukimya ulitawala ndani ya chumba hicho, kiasi kwamba hata mihemo ya watu ilisikika, jaji akiwa ameinamisha kichwa chake akichapa mambo fulani kwenye kompyuta yake, ghafla watu wote wakiwa hawana hili wala lile, alionekana akiingia mwanaume aliyefungwa bendeji begani na mkononi, akasimama katikati ya ukumbi wa mahakama, askari wakiwa wamepigwa na butwaa alichomoa bastola yake na kuanza kumfyatulia Jackson Motown huku akipiga kelele!
“You fool nigga thought I died? I am back from hell to do only one thing: Kill you Mr. Motown! I am asking you honorable Judge to sentence me to death now! I deserve to die for the bad things that this bad man sent me to do! I am ready to die because he is dead to…!” (Wewe mjinga ulifikiri nimekufa? Nimerudi kutoka kuzimu kufanya kitu kimoja tu; kukuua bwana Motown! Namuomba Mheshimiwa Jaji anihukumu kifo sasa hivi, nastahili kufa sababu ya mabaya ambayo huyu mtu mbaya alinituma kuyafanya! Niko tayari kufa kwa sababu yeye pia ameku…) aliongea mwanaume huyo lakini hakuimalizia sentensi yake, milio ya risasi ikasikika tena, akaanguka chini mbele ya kizimba alichokuwa ameanguka Jackson Motown.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi Jumatano.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply