The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu – 61

0

KEVIN ameungana na wazazi wake mahakamani ambako anatakiwa kutoa ushahidi dhidi ya Jackson Motown akiwa na mzee Thomas Edmund aliyemwokoa! Kazi hiyo wameifanya, Jackson Motown na washirika wake wamechanganyikiwa kabisa kwani inaonekana hakuna mlango wa kutokea kwenye kesi hiyo ambayo waliamini ilikuwa imepita.

Ghafla mzee Edmund alipomaliza kutoa ushahidi wake ulioonyesha jinsi alivyomwokoa Kevin, mtu amevamia mahakamani akiwa na bastola mkononi na kumfyatulia Jackson Motown ambaye ameanguka chini kizimbani na kutulia, maneno anayoyasema mtu huyo ni “Wewe mjinga ulifikiri nimekufa?

imerudi kutoka kuzimu kufanya kitu kimoja tu; kukuua bwana Motown! Namuomba Mheshimiwa Jaji anihukumu kifo sasa hivi, nastahili kufa sababu ya mabaya ambayo huyu mtu mbaya alinituma kuyafanya! Niko tayari kufa kwa sababu yeye pia ameku…”

Kabla hajamaliza risasi zinalia tena naye anaanguka chini mbele ya kizimba alichomo Jackson Motown. Je, amepigwa risasi na nani? Na mtu huyu ni nani? Catarina yuko hai ama amekufa? SONGA NAYO…

HEKAHEKA ya ajabu ilijitokeza ndani na nje ya chumba cha mahakama, milio ya risasi ilimtisha karibu kila mtu aliyekuwa mahakamani, hata jaji hakuweza kuvumilia, akakimbilia ndani kama walivyofanya watu wengine kuokoa maisha yao, haikuwezekana tena kuendelea na kesi.

Mwili wa mwanaume huyo ambaye askari walipomchunguza waligundua ni mtu wa karibu wa Jackson Motown, Dracula, ulikuwa umelala sakafuni ukivuja damu nyingi baada ya kupigwa risasi kichwani upande wa sikio la kulia, alionekana kabisa akitingishika kama ishara ya kukata roho, baadaye akatulia.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Jackson Motown, yeye alikuwa ametulia kabisa kizimbani alimoangukia,Dragon na wenzake wakiwa kando, bila kuelewa kilichokuwa kimetokea sababu ya upofu wao! Walichokifanya askari ni kuingia ndani ya kizimba na kumbeba Jackson Motown huku Dragon na wenzake wakiondolewa kizimbani kupelekwa ndani ya jengo la mahakama kulikokuwa na chumba maalum wakiwa chini ya ulinzi.

Mwili wa Jackson Motown ulioonekana kabisa alikufa mara tu baada ya kupigwa risasi, ulipakiwa kwenye gari la wagonjwa lililokuwepo mahakamani pamoja na mwili wa Dracula, askari wakaingia ndani na safari kuelekea Hospitali ya New York Orthopaedic Center iliyokuwa karibu kabisa na mahakama hiyo ikaanza.

Waandishi wa habari waliokuwepo walirekodi kila kilichotokea mahakamani hapo na kuanza kurusha kupitia mitandao ya kijamii na taarifa mbalimbali za habari kabla hata gari la wagonjwa halijafika hospitali, miili ilishushwa na kuingizwa chumba cha wagonjwa mahututi ambako daktari baada ya kuipima miili yote, alithibitisha Jackson Motown kuwa amekwishapoteza uhai, Dracula akipumua na moyo wake kupiga kwa mbali.

“Resuscitation! Resuscitation!” (Kuhuisha! Kuhuisha!) Dk. Linox Honey alipiga kelele kwenye spika zilizokuwemo chumba cha wagonjwa wa dharura akiwaita wataalam wa kuhuisha maisha ya watu waliokuwa katika hatari ya kufa.

Dakika mbili tu walishafika na mashine zao, zikafungwa kwenye mwili wa Dracula bila kujali alifanya nini mahakamani, ilikuwa ni lazima maisha yake yaokolewe, askari waliokuwemo ndani ya chumba hicho walisema alikuwa ni shahidi muhimu mno katika kesi ya marehemu Jackson Motown ambaye maiti yake ilikuwa imelazwa juu ya kitanda kando yao.

“Inject hydrocotizone 200mg, elevate the lower parts of the bed, control bleeding and call the Lab guys to come here and do blood grouping and cross matching so that we can have the patient transfused with blood!” (Mchomeni Hydrocotizone 200mg, nyanyueni kitanda miguuni ili damu nyingi ielekee kichwani, dhibitini damu inayovuja na waiteni watu wa maabara waje hapa kumpima kundi lake la damu na kuangalia inafanana na damu ipi ili awekewe damu!) Daktari alizidi kupiga kelele.

Hayo yote yakiendelea, mwili wa Jackson Motown uliondolewa na kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti, haikuwa rahisi kuamini kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa Jackson Motown! Dunia nzima ilitaarifiwa kupitia vyombo vya habari wakati Dracula akiwa chumba cha upasuaji, madaktari wakihangaika kuondoa risasi iliyokuwa imekamata kichwani mwake, mmoja wa askari mahakamani alimpiga risasi kichwani na mwingine mguuni.

Saa tano baadaye Dracula alitolewa chumba cha upasuaji na kurejeshwa chumba cha wagonjwa mahututi ambako aliendelea kupata matibabu akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, hakuwa na fahamu yoyote ndani ya saa sabini na mbili akipumulia mashine, madaktari waliofanya upasuaji huo wakiongea na wakuu wa jeshi la polisi na viongozi wa mahakama na FBI waliwaahidi kwamba Dracula angepona kwani upasuaji wake ulikuwa umefanyika kwa mafanikio makubwa.

“One thing I am not sure of is whether he will be able to speak again!” (Kitu kimoja sina uhakika nacho ni kama ataweza kuzungumza tena!)

“It is important that he speaks, because he is a key witness in a murder and rape case!” (Ni vizuri akazungumza, kwa sababu ni mtu wa muhimu sana kwenye kesi ya mauaji na ubakaji!)
“Fifty to sixty percent because the speech center in the brain was touched by the bullet” (Uwezo wa kuzungumza ni asilimia hamsini hadi sitini, kwa sababu kituo cha kuzungumza kwenye ubongo kimeguswa na risasi!)

“Oh my God! He knows a lot of Jackson Motown’s secrets!”(Mungu wangu! Anajua siri nyingi za Jackson Motown!)
“I can’t promise that he will be able to speak!” (Siwezi kuahidi kwamba ataweza kuongea!)
***
Ilikuwa ni siku ya furaha mno kwa wazazi wa Kevin, huzuni ilikuwa ni kwa upande wa wazazi wa Catarina na kwa Kevin furaha hiyo ilikuwa haijakamilika kwa sababu Catarina hakuwepo! Wote walikuwa ndani ya nyumba iliyolindwa na FBI, mzee Thomas Edmund pia alikuwepo, hapo ndipo walipoelekea baada ya kutoka mahakamani ambako milio ya risasi iliwafanya wakimbie kuokoa maisha yao, kilichotokea kiliwashtua wote, hasa baada ya Jackson Motown kupigwa risasi na mtu ambaye waligundua alikuwa ni mtu wake wa karibu aliyekuwa amepotea katika mazingira ya kutatanisha, hakuna aliyehisi kwamba mtu huyo ndiye alikuwa Padri Coronel Garsia.

Mzee Edmund aliwasimulia namna alivyomwokoa mtoto wao, wazazi nao wakaeleza jinsi Catarina alivyoondoka nyumbani akiwa na Padri na hakurejea tena, wote walikubaliana kwamba kesi iliyokuwa mahakamani ikiisha na hukumu kutolewa ilikuwa ni lazima kazi ya kumtafuta Catarina au kufahamu kilichompata baada ya kuondoka nyumbani iendelee iwapo FBI walikuwa wameshindwa kuitekeleza, mzee Edmund aliahidi kuwapa kila aina ya ushirikiano.

“Kesi ikiisha tu lazima nianze kazi iliyonileta Marekani, sikubali kabisa Catarina apotee hivihivi, hata kama amekufa, basi angalau niione mifupa yake, ndipo nitaamini!” Aliongea Kevin kwa uchungu mkubwa.

Wiki moja baadaye, wakiwa bado wamo ndani ya nyumba, mke wa Edmund akiwa pia ameungana nao, walisikia juu ya maziko ya Jackson Motown yaliyohudhuriwa na watu wachache mno kupitia vyombo vya habari na kwamba Dracula alikuwa akiendelea na matibabu, alisharejewa na fahamu lakini hakuwa na uwezo wa kuongea.

“Huyu akizungumza atafichua kila kitu juu ya ukatili alioufanya Jackson Motown, lazima kuna sababu kwa nini alisema anamuua mtu mbaya aliyemtuma kufanya mambo mabaya, pengine anaelewa kilichompata Catarina na hata Padri Coronel Garsia!” Mzee Thomas Edmund aliongea, bila kuelewa kwamba mtu huyohuyo ndiye alikuwa Padri Garsia.

Kesi haikuweza kuendelea, Dracula akisubiriwa awe na uwezo wa kuongea lakini haikutokea, miezi sita baadaye Dragon na wenzake wakiwa mahabusu na Kevin, wazazi wake na wazazi wa Catarina wakiendelea kuishi kwenye nyumba iliyolindwa na FBI bila kuelewa mahali Catarina alipokuwa, ndipo Dracula alianza kuongea maneno machache.

Je, nini kitaendelea? Catarina yuko wapi? Ataungana na Kevin? Fuatilia siku ya Ijumaa katika Gazeti la Championi Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply