The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu -79

6

ILIPOISHIA…
HAKUNA aliyekuwa tayari kuamini kama kweli Kevin na Catarina, mwanamke aliyeaminika kufa miaka mingi, walikuwa wamerejea Tanzania, tena wakiwa wenye afya njema kabisa, wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wote walikuwa wakifurahia uwepo wa watoto wao.

Magari maalum yalikuwepo kuwasubiri, wakaingia ndani yake na safari kuelekea nyumbani ikaanza, kwa saa kadhaa magari yaliendeshwa na hatimaye safari ikafikia mwisho nyumbani kwa akina Kevin ambako maandalizi ya chakula yalifanyika, watu wakala, kunywa na kufurahia kumwona tena Catarina.

Catarina aliongea na wazazi wake juu ya yeye kubaki nyumbani kwa akina Kevin akiwaeleza wazi kwamba hakuwa tayari kumwacha kwani kufanya hivyo kungeweza kuleta shida baadaye jambo ambalo wazazi wa pande zote mbili walilikubali bila ubishi wowote ule.

Mapenzi  yalikuwa moto, kila walikotembea walikuwa wote, walipoketi pia walikuwa pamoja, si Catarina wala Kevin aliyekuwa tayari kuwa mbali na mwenzake, penzi lilikuwa shamushamu, ni jambo hilo ndilo lililosababisha wazazi wa pande zote mbili kufanya maandalizi ya ndoa harakaharaka ili hatimaye watoto wao wafunge ndoa na kuishi pamoja, jambo ambalo lilisubiriwa kwa hamu kubwa na Kevin pamoja na Catarina.

Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…
SONGA NAYO…

MAANDALIZI ya ndoa yalikuwa yamepamba moto, ndoa ya Catarina  na Kevin ilikuwa gumzo kila kona ya Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake,  wazazi wa pande zote mbili walionekana kuwa bize ili tu kuhakikisha kwamba kila kitu kinakwenda sawa, ndugu, jamaa na marafiki wote, tayari walishapewa taarifa ili kuwa tayari kwa ajili ya ndoa ya Catarina na Kevin.

Wakati wazazi wakiendelea upande wao, upande wa Catarina na Kevin nao walionekana kuwa bize, wakipita katika maduka mbalimbali jijini kwa ajili ya kufanya manunuzi ya nguo ambazo wangevalia siku hiyo maalum, walitaka kupendeza.
“Nataka upendeze Catarina wangu, hivyo hakikisha unafanya maamuzi sahihi wakati wa kununua shela lako, sawa mpenzi?”
“Usijali, kwa kazi yangu ya uanamitindo, ujuzi kidogo nilioupata hakika sitakuangusha, nitapendeza mpaka unisahau.” Yalikuwa ni majibu ya Catarina akimweleza Kevin ndani ya gari kuelekea maeneo ya Posta katika maduka  makubwa yaliyouza nguo za harusi.

Kitendo cha watu kugundua kwamba Catarina  na Kevin walitarajia kufunga ndoa muda si mrefu, kilifanya kila walipokwenda waandishi wawe nyuma yao, wengi wakitaka kuandika makala na habari mbalimbali kwa matukio ambayo yalimtokea Catarina jinsi walivyokutana na Kevin, maisha aliyopitia, kutangazwa kwa kifo wakati alikuwa hai.

Catarina akageuka staa, gumzo kila alikopita, magazeti na televisheni vikieleza juu ya mapenzi yao, Kevin alivyojitolea uboho kumwokoa na ugonjwa wa saratani ya damu, jinsi alivyonusurika kifo kwa kutupwa katika hifadhi ya American National Park, hakika habari zake zilionekana kuvutia watu wengi nchini Tanzania. Ndugu wa pande zote mbili tayari walishafika mjini ili kuungana nao katika kusherehekea siku hiyo muhimu maishani.

Mwezi mmoja tu baadaye, baada ya vikao kukaa na kupanga juu ya tukio hilo muhimu, tarehe kumi na nane mwezi wa saba ndiyo ilipangwa kufungwa kwa ndoa hiyo na walifikia muafaka wa kufunga ndoa katika kanisa la St. Peters na sherehe kubwa ingefuata katika Ukumbi wa Mlimani City.

“Kila kitu sasa kiko sawa, ni vyema Catarina na Kevin wakaelezwa juu ya jambo hili!” Ilikuwa ni sauti ya Mdoe akimweleza mzee David, baba wa Catarina.

“Nadhani wanafahamu, wanachotakiwa kufanya wao ni kuweka mambo yao sawa, ninadhani wamefanya hivyo.”
“Tuamini hivyo,” yalikuwa ni maongezi ya wazee wawili, mzee Mdoe na David siku moja baada ya kumaliza kikao cha harusi.

Siku zilionekana kwenda kidogokidogo kwa Catarina na Kevin, pamoja na kwamba mbele yao ulikuwa mwezi mmoja tu kukamilisha ratiba, lakini kwao ilikuwa ni kama mwaka, walitamani jambo hilo lifike haraka.
“Unajua nini Catarina!”
“Nini?”
“Nimekaa na wewe muda mrefu sana lakini hamu haiishi.”
“Si wewe tu, mimi pia mpenzi, nahisi kuchelewa.”
“Bado wiki tatu ni nyingi mno, sijui kwa nini waliweka tarehe ya mbali kiasi hicho, hawa wazee bwana….” aliongea Kevin huku akicheka.

Wiki ya kwanza ikakatika, hatimaye ikaja ya pili mbele yao ilibaki wiki moja tu kukamilisha zoezi,  maandalizi yote yalishafanyika kwao, marafiki, ndugu na jamaa walishachanga kiasi cha shilingi milioni mia moja na themanini ili kuhakikisha kila kitu katika ndoa hiyo maarufu kinakwenda sawa.
“Mungu ni mwema sana mke wangu mtarajiwa.”
“Kwa?”
“Baba ameniambia ndoa yetu mpaka sasa imekusanya kiasi cha shilingi milioni mia moja na themanini.”
“Nalijua hilo, sijui tutazifanyia nini fedha zote hizo? Mimi mwenyewe nilishangaa siku moja baba aliponiita na kunieleza.”
“Sishangai, tunao marafiki wengi mno wanaotupenda, umesahau!”
“Kweli…ndoa yetu imekuwa maarufu kila kona, hapa tu bado hiyo siku yenyewe ikifika sijui itakuwaje kila kona ya Jiji la Dar es Salaam, huwezi amini juzi nilikuwa natafuta kitu kwenye mtandao wa kijamii nikakuta picha yetu humo iliyoambatana na tarehe yetu ya kufunga ndoa, hakuna siri tena.”
“Mungu atusaidie tumalize salama. Ninakupenda mno, sipo tayari kukupoteza tena, wewe ulimaanishwa kuwa wangu, nikikumbuka mapito tuliyopitia najikuta nalia, tunapendana hakika,” aliongea Catarina huku akimpigapiga Kevin mgongoni.

“Hakuna haja ya kulia tena, amini tu kwamba Mungu alikuwa na kusudi juu ya yote yaliyotokea kwetu.”
“Hakika!”
Zilipobaki siku tatu mbele, wazazi wa Catarina walimwita mtoto wao na kumweleza kwamba sasa alitakiwa kurudi nyumbani akisubiri ndoa ifungwe kwani haikuwa sawa yeye kutokea nyumbani kwa akina Kevin siku ya ndoa, Catarina akapokea ujumbe huo ingawa kwa shingo upande na kurejea nyumbani, ahadi ya Kevin ikiwa ni kuja kumtembelea kila siku.

“Nenda tu nyumbani, nitakuja kukutembelea amini.”
“Kevin! Kevin usiache, unajua siamini kama tumekutana tena.”
“Amini mpenzi mimi ni wako na wewe ni wangu maisha yote.”
“Basi mimi jioni naondoka kurejea nyumbani, kumbuka bado siku tatu tu tufunge ndoa yetu.”
“Usiogope.”
Yalikuwa ni maongezi ya Catarina na Kevin asubuhi moja baada ya wazazi wa Catarina kutuma ujumbe kwamba ilikuwa ni lazima arudi nyumbani kuagana na ndugu zake na kwa desturi za Kiafrika, halikuwa jambo jema kutoka nyumba moja siku ya ndoa yao.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa, Catarina akawa amerejea nyumbani na kazi ya Kevin ikawa ni kutimiza ahadi yake, kila siku jioni alikwenda nyumbani kwa akina Catarina kumjulia hali na kumweleza jinsi mipango ilivyokuwa ikiendelea na kwamba kila kitu kilikwenda sawa kabisa.
***
Saa tisa kamili siku ya Jumamosi tarehe iliyopangwa, Kevin akiwa na familia yake tayari alikuwa kanisani ndani ya suti nyeupe yeye na mpambe wake, hakika alivutia, kamera nyingi zikimzunguka kuchukua picha za tukio pamoja na kumbukumbu, mtu pekee aliyesubiriwa alikuwa ni Catarina, huyo ndiye aliyekuwa wa muhimu wakati huo. Muda wote Kevin alionekana kuzungusha macho yake huku na kule kuangalia na wakati mwingine kutupa macho yake kwenye simu.
“Nini tena Kevin.”
“Catarina mama, simwoni mbona amechelewa kiasi hiki?”
“Tumeongea nao wako njiani, msafara wake ni mrefu kidogo, hivyo atafika muda mfupi ujao.”
“Mpaka nimwone ndiyo nitaamini.” Aliongea Kevin na haikuchukua muda mrefu akashuhudia msafara mrefu wa magari mengi ya kifahari yakitembea kuingia eneo la kanisani, akashusha pumzi, alichotaka wakati huo ni kumwona Catarina wake basi, ndipo mambo mengine yaendelee.

“Afadhali…” aliongea akishuka garini huku akipiga hatua kulifuata gari lililombeba Catarina.
“Kevin unakwenda wapi?” Mpambe aliuliza.
“Nataka kumwona Catarina.”
“Hairuhusiwi, utamwona kanisani.”  Ilikuwa ni sauti ya mpemba wa Kevin, hapo hapo bila kuchelewa, akamshika Kevin mkono na kumwongoza kuelekea mlango wa kanisa, hapo wakafuata taratibu zote kisha kuanza kuingia na kutembea kwenda mbele ambako angemsubiri mkewe aingie.

Kanisa lilikuwa limefurika watu, mastaa mbalimbali wakionekana hapo, wapiga picha na vyombo mbalimbali vya televisheni navyo vilikuwepo kuchukua matukio, hakika ndoa ilikuwa imetikisa jiji.

Wakiwa hapo, dakika tano tu baadaye, Kevin alishuhudia Catarina akiingizwa akiwa ameshikwa mkono na mtu aliyemfahamu, hakuwa mwingine bali baba yake mzazi Catarina, alipendeza kupindukia, shela lake lililoburuzika kwa nyuma, ndilo lililoacha midomo wazi ya watu wote waliokuwemo ndani ya kanisa, Catarina alipendeza  kwelikweli, hamu ya Kevin ikawa ni kumwona kwa karibu amkumbatie na ikiwezekana ampige mabusu.

“Leo ni leo, ndiyo siku niliyokuwa nikiisubiri kwa hamu, kufunga ndoa na Kevin, mwanaume wa maisha yangu, ahsante Mungu kwa neema hii…” aliwaza  Catarina akitembea kuelekea mbele huku machozi yakimbubujika.
Alizipiga hatua kidogokidogo huku akisindikizwa na wimbo wa injili uliosikika kwa mbali ndani ya kanisa, macho ya watu wote yakimshangaa kwa uzuri na jinsi alivyopendeza, hakika alivutia, hatimaye wakafika mbele na Kevin, akampokea mke wake kisha kuketi wakisubiri tukio muhimu kwao.

Wakati zoezi hilo likiendelea, padri akiwa mbele kabisa akiendesha misa, mwanaume mmoja aliyevalia vyema alionekana akiingia kwa haraka na kutembea kwa ujasiri moja kwa moja kwenda mbele mahali walipokuwa maharusi padri akifungisha ndoa, akasimama pembeni kabisa na Kevin aliyekuwa amepiga magoti chini,  mara ghafla macho ya padri yakashuhudia mwanaume huyo akichomoa visu viwili na kumwelekezea Kevin, kilichosikika hapo ilikuwa ni kelele tu.
“Noooo!” (Hapana!) Padri alipiga kelele.

Je, nini  kitaendelea? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi Jumatano.

SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

6 Comments
  1. neema mikey says

    jamal tu huyo,hakuna ndoa tena hapo

  2. Emmanuel says

    Inarukaruka xna

  3. vero says

    Mbona hamrushi nyingine? Au ndo mwisho hapo????

  4. abdallah dadi says

    gooooood
    thaaaana

  5. Vermund Msemwa says

    Mnakawia sana kuweka sehemu zinazo fuata!!

  6. abubakari makumbusya says

    Jamani mboma kimya au imeisha

Leave A Reply