The House of Favourite Newspapers

Mkulima na Dereva Kortini Meno ya Tembo ya Mil 173

0

WATU wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kukutwa na kujihusisha na nyara za serikali zenye thamani ya zaidi ya Sh 173.

 

 

Washitakiwa hao Hussein Seif, mkulima wa Kisarawe mkoani Pwani na Ally Palupalu, dereva mkazi wa Chanika, Dar es Salaam walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.

 

 

Akiwasomea mashtaka Wakili wa Serikali, Kija Luzungana katika shtaka la kwanza la kukutwa na nyara za serikali kinyume na sheria, alidai mnamo Machi 23, 2021 eneo la Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam washitakiwa wote kwa pamoja walikutwa na vipande 8 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh 173,248,500 mali ya serikali ya Tanzania bila kibali cha Mkurugenzi wa Idara ya Wanyama Pori.

 

 

Katika shitaka la pili la kujihusisha na nyara za serikali kinyume na sheria, Luzungana alidai tarehe na eneo hilo hilo washtakiwa wote kwa pamoja walikutwa wakisafirisha vipande nane vya meno ya tembo vyenye thamani hiyo bila kibali cha Mkurugenzi wa Idara ya Wanyama Pori.

 

 

Luzungana alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika hivyo aliomba tarehe nyingine ya kutajwa. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 13. Washitakiwa hao hawakutuhusiwa kujibu na walipelekwa mahabusu kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

 

 

Katika kesi nyingine watu wawili wamefikishwa katika Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Huruma Shaid kwa mashitaka ya kukutwa na kujihusisha na nyara za serikali zenye thamani ya Sh milioni 8.4 kinyume na sheria.

 

 

Adam Mohammed, mkulima wa Kilwa Kivinje mkoani Lindi na Nganya Mkanyagae mfanyabiashara wa Bagamoyo mkoani pwani walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Nguka Faraji.

 

 

Katika shtaka la kwanza la kupatikana na nyara za serikali alidai mnamo Machi 13, 2021 katika eneo la Mbagala rangi tatu, Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam washtakiwa hao wote wawili walikutwa wakimiliki ngozi ya chui yenye thamani ya Sh 8,084,958 mali ya Serikali ya Tanzania bila kibali cha Mkurugenzi wa Idara ya Wanyama Pori.

 

 

Katika shtaka la pili la kujihusisha na nyara za serikali, Nguka alidai mnamo Machi 13, 2022 katika eneo la Mbagala rang tatu, Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, washitakiwa hao kwa pamoja walikutwa wakisafirisha ngozi ya chui yenye thamani ya Sh Sh 8,084,958 mali ya serikali ya Tanzania bila kibali cha Mkurugenzi wa idara ya Wanyama pori jambo ambalo ni kinyume na sheria.

 

 

Nguka alidai upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hajatoa kibali cha kusikiliza kesi hiyo mahakamani hapo hivyo washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote.

 

 

Washtakiwa walipelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kupeleka wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kila mmoja watakaosaini bond ya Sh milioni tano na mmoja kati yao awe na hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.

 

 

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 13 mwaka huu.

Leave A Reply