The House of Favourite Newspapers

Mkuu wa Mkoa Iringa Aunadi Mkoa Wake Kiutalii (Video)

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza (katikati mbele) akielezea fursa mbalimbali zinazopatikana katika mkoa huo.
Waandishi wa habari na viongozi mbalimbali wa Iringa na sekta ya utalii, wakifuatilia kwa makini mkutano huo.
Masenza akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela (aliyekaa kushoto) na viongozi wengine wa mkoa huo.

TAARIFA YA MKUU WA MKOA WA IRINGA, MHE. AMINA MASENZA KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSIANA NA MAONESHO YA UTALII KARIBU KUSINI PAMOJA NA MAADHIMISHO YA KITAIFA YA SIKU YA UTALII DUNIANI 2018 YATAKAYOFANYIKA MKOANI IRINGA SEPTEMBA 26 HADI 30, 2018. 

 

Ndugu,

Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Utalii Tanzania,

Kaimu katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa

Mkuu wa Wilaya ya Iringa

Wawakilishi wa Wakurugenzi toka Idara za malikale, Wanyamapori na Utalii, Misitu na Idara nyinginezo za Serikali

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa

Wakuu wa Taasisi mbalimbali,

Wataalamu wote

Wadau wa Sekta ya Utalii,

Wageni waalikwa,

Waandishi wa habari,

Mabibi na Mabwana

Awali ya yote kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia afya njema na hatimaye  tukakutana  hapa  leo  hii.

 

Kisha naomba nitumie fursa hii kuwashukuru wadau wote wa utalii na wadau wa maendeleo kwa ujumla ndani na nje ya nchi kwa kuendelea kushirikiana na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini  katika kufanikisha Maonesho ya Utalii Karibu Kusini yanayoenda sambamba na Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani Kitaifa kwa Miaka Miwili mfululizo  ambayo yamekuwa yakifanyika Mkoani Iringa yakijulikana kwa jina la Utalii Karibu Kusini, Mwaka huu ni mwaka wa tatu  kufanikisha Maonesho haya.

Tangu Maonesho haya yaanze rasmi 2016 mafanikio mbalimbali yamejitokeza katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Kuimarika kwa uhamasishaji wa sekta ya Utalii kupitia matamasha kama vile Tulia Trust huko Mbeya, Mbio za magari, Mbio za Nyika kwa Mikoa ya Iringa, Mbeya, Ruvuma na Songwe, Ongezeko la ushiriki wa wadau katika maandalizi ya maadhimisho hayo akiwemo mdau mkubwa toka kampuni ya Capital Plus international na ongezeko la washiriki katika Maonesho toka 225 mwaka 2016 hadi 435 mwaka 2017

 

Ndugu wana habari,

Ni wazi kwamba  kanda ya Nyanda za juu Kusini inayoundwa na mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe, Ruvuma, Rukwa na Katavi imebarikiwa kuwa na idadi kubwa ya vivutio vya kihistoria, kiutamaduni na kiikolojia vinavyofanya upekee wa mikoa hii katika sekta ya utalii hapa nchini na Ulimwenguni kwa ujumla. Hii ni kwa sababu  sehemu kubwa ya vivutio hivi vimehusishwa na mfumo wa utawala na kupigania uhuru tangu enzi za vita dhidi ya uvamizi wa wakoloni. Mfano mapambano kati ya Chifu Mkwawa na wakoloni wa Kijerumani pamoja na vita vya Majimaji.

 

 

Aidha, Mikoa ya nyanda za juu Kusini inasifika kuwa na hifadhi zenye sifa za kipekee ikiwemo Taifa ya Ruaha yenye makundi makubwa ya tembo na wanyama wengine. Hifadhi nyingine ni Kitulo yenye aina mbali mbali za maua ambayo hayapatikani mahali pengine Duniani; na Udzungwa yenye wanyama adimu duniani kama vyura wa Kihansi, nyani wa kipekee (kipunji), mapango, michoro ya kale na mito mikubwa na maziwa.

 

Aidha, wakuu wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini tumelipokea kwa mikono miwili agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.  Dkt. John Pombe Magufuli la kufungua Utalii kwa kutangaza vivutio vinavyopatikana katika mikoa ya nyanda za juu Kusini.Mhe. Rais alitoa maagizo hayo wakati wa kilele cha sherehe za Mei Mosi 2018, Mkoani Iringa.

 

Aidha, Katika utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt.Hamisi Kigwangalla, wakati akifunga rasmi maonesho ya utalii ya Kimondo yaliyofanyika Mkoani Songwe hivi karibuni alitumia fursa hiyo kuzindua rasmi maonesho ya tatu ya Utalii Karibu Kusini. Mhe. Waziri aliitaka mikoa ya nyanda za juu Kusini kwa kushirikiana na wizara ya Maliasili na Utalii kuandaa kalenda ya pamoja itakayoainisha matukio ya kimkakati katika  kutangaza vivutio vya utalii katika mikoa ya nyanda za juu Kusini. Kwa sasa tunaendelea kuufanyia kazi maagizo hayo na tunaamini kwa pamoja tutafanikiwa, Umoja ni Ushindi.

 

 

 

Ndugu wana habari,

Katika kuhakikisha kwamba Maonesho ya tatu ya Utalii Karibu Kusini 2018 (Southern Circuit Tourism Exhibition 2018) ya mwaka huu yanakuwa ya kipekee zaidi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa ambayo ndio waratibu wa maonesho hayo  ikiwakilisha mikoa mingine ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii, tumeamua kushirikiana na kampuni ya Capital Plus Plus International ya jijini Dar es Salaam katika kufanikisha maandalizi ya maonesho haya.

 

Kupitia ushirikiano huu tunatarajia kwamba tutaongeza wigo mpana zaidi wa ushiriki wa sekta binafsi katika maonesho haya. Tofauti na miaka miwili iliyopita maonesho ya mwaka huu yataambatana na nyongeza ya matukio kadhaa ya kimichezo, kitaaluma na kiutamaduni ili kuongeza tija zaidi katika kufikia malengo ambayo hasa ni kuongeza mazao ya utalii katika kanda yetu.

 

Ndugu wana habari,

Kilele cha Maonesho ya Utalii Karibu Kusini 2018 yanayotarajiwa kufanyika Septemba 26 hadi 30, 2018 katika viwanja vya Kihesa Kilolo Mkoani Iringa ambapo mbali na Kongamano la kujadili masuala ya Utalii na Uchumi litakalofanyika  tarehe 27 Septemba, 2018, pia tutakuwa na matukio ya kimichezo kama ifuatavyo:

 

  1. Mashindano ya mchezo wa Golf yanayotarajiwa kufanyika Wilayani Mufindi kuanzia Julai 27 hadi 29, 2018 yakihusisha washiriki kutoka vilabu mbalimbali vya mchezo huo ndani na nje ya nchi na hivi tunapozungumza hapa tayari maandalizi ya mashindano hayo yanaendelea kwa kushirikiana na wenzetu wa Mufindi Golf Club pamoja na wamiliki wa Uwanja huo Kampuni ya Unilever Tea Tanzania Limited. Nitumie fursa hii kuwaomba sana washiriki pamoja na wadhamini wajitokeze kwa wingi ili kufanikisha hili.

 

  1. Mashindano ya Mbio za Baiskeli. Mashindano haya yatafahamika kwa jina la ‘Southern Circuit Utalii Cycling Challenge’ yanatarajiwa kufanyika Septemba 29 Mkoani Iringa yakihusisha pia watu wenye ulemavu. Mbio hizi zitaanzia katikati ya mji wa Iringa na kuhitimishwa kwenye viwanja vya Kihesa Kilolo ambapo washiriki na baiskeli zao, watazamaji, pamoja na miundombinu itakayohusika na mbio hizi itapambwa na agenda yetu ambayo ni kutangaza vivutio vya utalii katika kanda ya Nyanda za juu Kusini. Washiriki na wadhamini pia wanaombwa kujitokeza kudhamini mbio hizi zinazotarajiwa kuwa na mvuto mkubwa.

 

3.Ngoma za Asili. Tunarajia kwamba katika kipindi chote cha maonesho haya yaani Septemba 26 hadi 29 vikundi kadhaa vya ngoma za asili kutoka mikoa mbalimbali ya Nyanda za juu kusini vitakuwa vikionyesha umahili wao katika kucheza na kuimba nyimbo za asili yao ikiwa nisehemu ya utekelezaji wa agizo la serikali la kuhuisha urithi wa utamaduni. Wito kwa wapenzi na wadau wa aina hii ya burudani wajitokeze kwa wingi kuunga mkono vikundi vyetu kwa kutazama pamoja na kudhamini pia.

  1. Kilele cha matukio yote haya ya kimichezo kitakuwa Septemba 30 ambapo pia ndio itakuwa kilele cha Maonesho ya Utalii Karibu Kusini 2018, kitakachopambwa na Mashindano ya mbio za nyika (marathon). Mbio hizi zinazofahamika kwa jina la ‘Southern Circuit Utalii Marathon 2018’ zitaanzia katikati ya mji wa Iringa na zitahitimishwa katika viwanja vya maonesho vya Kihesa Kilolo.

 

Tunatarajia kupokea washiriki kutoka ndani na nje ya nchi na lengo letu kuona ndani ya miaka michache tu mbio hizi zinakuwa ni moja ya mbio kubwa sio tu hapa nchini bali pia nje ya nchi ili tuweze kuwavutia washiriki wengi ambao si tu watakuja kukimbia mbio hizi bali pia watatembelea vivutio vya kiutalii vinavyopatikana katika ukanda wa nyanda za juu Kusini na kukuza Utalii wa michezo.

 

Aidha, katika kipindi chote cha maonesho haya  tumejipanga kuwe na utaratibu wa usafiri kwa washiriki, wageni  pamoja na wenyeji wa Mkoa Iringa ili  waweze kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika ukanda huu. Nawaomba sana wananchi wote wajipange kushiriki katika maonesho haya makubwa. Pia niwaombe sana wadau wetu wa maendeleo ikiwemo sekta binafsi wajitokeze kwa wingi kuu mkono maonesho haya. Asanteni sana kwa kunisikiliza

 

Mungu Ibariki Afrika,

Mungu Ibariki Tanzania,

Long live Utalii Karibu Kusini!

 

 

 

Comments are closed.