The House of Favourite Newspapers

Mkwasa Akabidhiwa Mikoba Yanga

0

MABOSI wa Yanga wamewaambia wapinzani wao, Simba kwamba wasitarajie kwamba watakutana na urahisi watakapokutana nao wakiamini kocha Luc Eymael hawajui vizuri, katika mchezo wao ujao wa Machi 8 katika Ligi Kuu Bara kwa kuwa wana mipango mbadala.

 

Hivyo maamuzi ambayo Yanga wamefikia ndani kwa ndani ni kumpa nguvu na kumkabidhi mikoba kwa asilimia kubwa Charles Mkwasa ambaye ni kocha msaidizi kwa kuwa anawajua vizuri Simba.

 

Maamuzi hayo yamekuja baada ya mabosi wa Yanga kumuona Eymael hana ufahamu mkubwa kuhusu Simba huku mchezo huo wa Ligi Kuu Bara ukitarajiwa kuwa na presha kubwa kutokana na upinzani wa jadi baina ya timu hizo za Kariakoo.

Mkwasa alifanya vizuri wakati timu hizo zilipokutana raundi ya kwanza kwa kuilazimisha Simba sare ya mabao 2-2 licha ya kuwa Simba ndiyo waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kushinda kutokana na kuwa katika kiwango bora na waliongoza 2-0.

 

Hadi sasa zimesalia siku nane tu kabla ya timu hizo kuvaana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela ameliambia Championi Ijumaa, kuwa wanaamini Mkwasa atamsaidia Eymael kutokana na kuifahamu Simba kwa undani mkubwa lakini pia kufahamu utamaduni wa klabu hiyo katika mechi hiyo.

 

“Ni kweli kocha ni mgeni katika mechi kama hizi za Simba na Yanga ndiyo maana kuna makocha wazawa kama Charles Mkwasa ambaye anajua utamaduni wetu, anawajua wachezaji wa Kitanzania lakini pia anawajua wachezaji wa Simba.

“Anaijua Simba vilivyo kwa hiyo tunaamini atakuwa msaada mkubwa kwa kocha katika kuhakikisha tunashinda katika mechi hii na Simba lakini pia mechi nyingine.

 

“Lakini tuna mbinu nyingine mbadala ambayo tutampa kocha, yote hayo ikiwa ni kutaka kuwafahamu Simba ili tutakapokutana nao iwe rahisi kwake kupata ushindi,” alisema Mwakalebela.

 

Mbelgiji akosa usingizi kisa Simba

Wakati huohuo, Eymael amesema kuwa anapitia kipindi kigumu kwa sasa lakini atapambana kupata matokeo mbele ya Simba.

Kabla ya kumenyana na Simba, Yanga ina dakika 180 za kucheza na Alliance Februari 29 na Mbao FC mnamo Machi 3 zote zitapigwa kwenye Uwanja wa Taifa.

 

“Ligi ni ngumu na mechi ninazokutana nazo zina vikwazo vingi kabla ya kukutana na Simba nitakuwa na mechi nyingi za kucheza hivyo nina muda wa kuandaa kikosi lakini ni ukweli kwamba sipati usingizi kwa ajili ya Simba.

 

“Ukitazama msimamo utaona kwa namna ambavyo wametuzidi kwa pointi nyingi mpaka idadi ya mabao, licha ya yote haya, matumaini ya kufanya vizuri yapo, mashabiki watupe sapoti,” alisema.

Stori na Said Ally na Lunyamadzo Mlyuka

Leave A Reply