The House of Favourite Newspapers

MLINZI WA MAKABURI: NILISHAWISHIWA NIUZE KIGANJA CHA MTOTO!

DAR ES SALAAM: Mzee mmoja, Charles Magilagila, wa Tabata Segerea ambaye ni mlinzi wa makaburi wa eneo hilo amefunguka jinsi alivyoombwa kiganja cha mtoto aliyezikwa siku moja.  

 

Akizungumza na gazeti la Amani, alisema kuwa anakutana na changamoto hizo lakini hiyo ya kuombwa kiganja cha mtoto imemfanya aamini kuwa dunia sasa imekwisha.

“Unajua siku zote usione binadamu wanatembea, wana mambo mengi sana hata ukiyatafakari unaweza usielewe na siku ambayo nimeombwa kiganja cha mtoto nilijua dunia imekwisha,” alisema.

 

Aliongeza kuwa, siku hiyo alikuwa analinda usiku wakaja watu wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Prado nyeusi na kumuomba kuzungumza naye ambapo alipowakubalia ndipo walipomuomba kama anaweza kuwasaidia kiganja cha mtoto mchanga.

“Mimi sikujua kama watu hao wangeweza kuniambia maneno hayo, nilijua kuwa walitaka kuzika mtu wao kesho, hivyo wamekuja kuniambia nichimbe kaburi mapema lakini sivyo, walitaka kiganja! Kwa kweli nilistaajabu sana,” alisema.

 

Aliongeza kuwa aliwaambia kuwa kamwe hawezi kufanya kazi hiyo kwa sababu yeye ni Mkristo safi kwa hiyo mambo kama hayo tangu aanze kuchimba makaburi na kuyalinda, hajawahi kufanya hivyo. “Waliniambia kama ningefanikisha zoezi lao wangenilipa shilingi milioni moja lakini nilikataa japo nina shida na hizo fedha, nilikataa kabisa, niliona ni dhambi kubwa.” alisema Magilagila.

Mzee huyo alisema kuwa baada ya kuwakatalia watu hao anaowataja kuwa ni washirikina waliondoa gari kwa kasi huku wakiniambia kwa hasira kuwa watakipata kiganja usiku huohuo sehemu nyingine.

Siku za hivi karibuni, Amani limekuwa likielezwa na vyanzo mbalimbali kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa wakinunua viungo mbalimbali vya binadamu kwa ajili ya matumizi yao ya kishirikina jambo ambalo ni kinyume na sheria.

 

Amani linaendelea kufanyia kazi madai hayo ambapo tayari limetega mitego yake katika makaburi mbalimbali ya Jiji la Dar ili kuweza kuwanasa wahusika. Endapo wahusika hao wataingia kwenye kumi na nane za Amani, wataanikwa ili ikiwezekana wachukuliwe hatua na vyombo vinavyohusika.

Stori: Imelda Mtema, Amani.

EXCLUSIVE: DIAMOND HAKUNIALIKA, ASIJISAHAU SANA – VIDEO

Comments are closed.