The House of Favourite Newspapers

MMILIKI MABASI YA PRINCESS MURO AFIKISHWA MAHAKAMANI

MFANYABIASHARA na mmiliki wa mabasi ya Princess Muro, Majid Abdallah, maarufu kama Kimaro (51) akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili yakiwa ni pamoja na wizi na utakatishaji wa mafuta.

MFANYABIASHARA na mmiliki wa mabasi ya Princess Muro, Majid Abdallah maarufu kama Kimaro (51) leo Oktoba 23.2018 amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la wizi na utakatishaji wa mafuta.

Mwendesha Mashtaka na Wakili wa Serikali, Esther Martin,  amedai mbele ya Hakimu Mkazi Maira Kasonde kuwa mshtakiwa ametenda makosa hayo kati ya Januari 2015 na Januari 2018 katika maeneo tofauti ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

 

Katika shtaka la wizi imedaiwa siku na mahali hapo mshtakiwa aliiba lita 15950.3 za mafuta aina ya Diesel na Lita 10925.22 za mafuta aina ya Petrol mali ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

 

Katika shtaka la utakatishaji, imedaiwa, siku hiyo katika sehemu tofauti  za Jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa alitakatisha lita hizo za mafuta kwa kuyauza na kuyabadilisha kwa fedha huku akijua kuwa mafuta hayo ni zao la kosa la wizi na alifanya hivyo kwa lengo la kupoteza uhalisia wa mafuta.

 

Hata hivyo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikilizwa kesi za uhujumu uchumi.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 5, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika.

Comments are closed.