The House of Favourite Newspapers

Mnangagwa Kurejea Zimbabwe Leo, Kuapishwa Ijumaa

0
Aliyekuwa makamu wa rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.

EMMERSON Mnangagwa ambaye alikuwa makamu wa rais wa Zimbabwe, anatarajiwa kurejea leo Zimbabwe, ikiwa ni zaidi ya wiki mbili tangu alipoondoka baada ya kufukuzwa kazi.

Mmoja wa wasaidizi wa Mnangagwa, Larry Mavhima amesema kuwa kiongozi huyo anarejea leo jioni na anatarajiwa kuzungumza na vyombo vya habari maara baada ya kuwasili Zimbabwe. Siku ya Jumapili Mnangagwa aliteuliwa kuwa rais wa chama tawala nchini Zimbabwe cha ZANU-PF kuchukua nafasi ya Mugabe.

 

Shirika la utangazaji la Zimbabwe limesema kuwa Mnangagwa ataapishwa siku ya Ijumaa kuwa rais wa mpito wa nchi hiyo.

 

Jana jioni, Mugabe mwenye umri wa miaka 93, alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya urais, hatua iliyohitimisha utawala wake wa miaka 37, baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa madaraka nchini Zimbabwe kwa siku kadhaa, bila ya kumwaga damu. Jeshi hilo lilimtaka Mugabe ajiuzulu, huku akikosolewa kwa kuharibu uchumi wa nchi.

 

Hatua ya Mugabe kujiuzulu ilipokewa kwa shangwe kubwa na nderemo, huku Wazimbabwe wakiimba na kucheza katika mitaa mbalimbali ya nchi hiyo, kama anavyoelezea mkaazi mmoja wa Harare James Makona.
Wananchi wa Zimbabwe wakishangilia

 

”Tuna furaha sana kuhusu jambo lote hili. Kwa sababu tumeteseka kwa muda mrefu sana. Nadhani kwa hatua hii mpya, sasa kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Makona.

 

Spika wa Bunge la Zimbabwe Jacob Mudenda ndiye aliisoma barua ya Mugabe kujizulu urais, wakati wa kikao maalum cha bunge ambacho kilikuwa kimeanza mchakato wa kisheria kumuondoa Mugabe madarakani.

 

Jana Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75, ambaye ana uhusiano wa karibu na jeshi, ambalo lilisaidia kumuondoa Mugabe madarakani, alitangaza kuwa amekataa mualiko uliotolewa na Mugabe wa kurejea nyumbani ili kujadiliana kuhusu hali ya kisiasa katika taifa hilo. Alisema angerejea tu Zimbabwe, iwapo angehakikishiwa kuhusu usalama wake.

Leave A Reply