The House of Favourite Newspapers

MNEC Gungu Atoa Vitabu Vya Uongozi Na Maadili

0
Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa Emmanuel Gungu Silanga akimkabidhi vitabu vya kanuni za uongozi na maadili Mwenyekiti wa CCM Simiyu Shemsa Mohamed Seif katika maadhimisho ya miaka 47 ya sherehe za kuzaliwa chama hicho wilayani busega mkoani simiyu

 

Katika kuadhimisha miaka 47, ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama hicho, Taifa (MNEC), Mkoa wa Simiyu, Emmanuel Gungu Silanga, ametoa vitabu vya uongozi na Maadili ya Chama, Katiba na Kanuni kwenye Kata zote za Mkoa huo, ili kuwawezesha Viongozi ambao wanataka kuomba uongozi ndani ya Chama kujua kazi zao.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Kata ya Nyaluwande, Wilayani Busega, Mjumbe huyo wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, amesema Vitendea kazi hivyo kwa viongozi hao ngazi ya Kata vitawasaidia kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa na kukisaidia chama kutekeleza majukumu yake vizuri.

“Kama mtakumbuka vizuri mwaka jana tukiwa Maswa wakati tunasherekea sherehe kama hizi niliahidi kutoa vitabu hivi kwa Mkoa mzima, leo navikabidhi hapa tukiwa tunasherekea miaka 47 ya kuzaliwa CCM,

“Vitendea kazi hivi ni nyenzo nzuri kwa viongozi wetu kuweza kutimiza majukumu yao vizuri.Hii pia itawasaidia hata wale ambao wanataka kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama kujua kazi zao,”alisema Gungu.

Kutokana na hatua ya Mjumbe huyo wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoa Vitabu hivyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed Seif alipongeza kwa kueleza kuwa vitabu hivyo ni msaada mkubwa kwa Chama, kwani vitasaidia kuwajenga viongozi na kuwawezesha kujua majukumu yao.

“Naomba nikupongeze sana Mnec Gungu, umefanya jambo kubwa sana vitabu hivi vitawasaidia viongozi wetu kuwaimarisha na kuwajenga vizuri kutekeleza majukumu yao naomba nichukue nafasi hii kukupongeza sana,”alisema Shemsa.

Gungu pia katika maadhimisho hayo alitoa mifuko ya saruji 30 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Kata ya CCM Nyaluwande sambamba na kutekeleza ahadi yake ya kutoa mifuko ya saruji 100 kwa ajili ya ujenzi ya Zahanati ya Kata ya Shigala Wilayani Busega, ambapo Wanachi wa Kata hiyo walimuomba kutokana na Kata hiyo kukosa Zahanati.

 

 

Leave A Reply