The House of Favourite Newspapers

Mnigeria, Mbongo Kortini kwa Kusafirisha Madawa

0

RAIA wa Nigeria na Mtanzania mmoja wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo kosa la uhujumu uchumi na kusafirisha dawa za kulevya aina heroin kilogram zaidi ya 37.

 

Washitakiwa hao ni Kenechi Okpala, raia wa Nigeria, na Aziza Mohammed ambao wamesomewa hati ya mashtaka katika mahakama hiyo na Wakili wa Serikali, Kija Luzungana, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Kassian Matembele.

 

Kesi hiyo imekuja kwa usajili wa namba 97 ya mwaka 2020.

 

Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Kassian Matembele, amedai mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi hivyo washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote mpaka pale DDP atakapotoa mamlaka kwa mahakama hiyo.

 

Katika shitaka la kwanza linalomuhusu mshitakiwa namba moja, Kenechi Okpala, Luzungana amedai kuwa Novemba 28 mwaka 2020 mshitakiwa huyo alikamatwa maeneo ya Kimara Temboni Jijini Dar es Salaam akiwa na dawa za kulevya aina ya heroin kilogram 4.47 kinyume na sheria.

 

Katika shitaka la pili kwa washitakiwa wote,  Luzungana amedai kuwa katika tarehe hiyohiyo Kenechi na Aziza Mohamed walikamatwa eneo la Kimara Temboni mtaa wa Upendo wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin kilogram 34.5.

 

Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Wankyo Simon, amedai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika, hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 23 mwaka huu na washtakiwa wamepelekwa rumande.

Leave A Reply