The House of Favourite Newspapers

Mnyika: Bawacha Haijaundwa Kupeleka Wabunge wa Viti Maalum

0

Katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika amelitaka Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha) kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi kwa ustawi wa chama hicho na Taifa.

 

Mnyika ameeleza hayo jana Jumanne Mei 18, 2021 katika kikao maalum cha kuchagua viongozi wa baraza hilo baada ya waliokuwepo kuvuliwa nyadhifa zao na kufukuzwa uanachama.

 

Mnyika amesema viongozi watakaochaguliwa wasifikirie kuwa baraza hilo lina kazi ya kuchagua viti maalum vya udiwani na ubunge, wanapaswa kutambua kuwa ni baraza la kutetea wanawake, kupigania tume huru na katiba mpya.

 

“Nyinyi wanawake wa Chadema kupitia baraza lenu mna nafasi ya pekee kuandika historia kama wamama wa mabadiliko, kama walezi wa haki. Kazi ya kuandika historia hiyo inaanza leo,” amesema.

 

Huku akiwagusia wanawake 19 waliovuliwa uanachama wa Chadema baada ya kula kiapo cha kuwa wabunge wa viti maalum bila ridhaa ya chama hicho, Mnyika amesema lazima katikati ya usaliti, uhasi na ubinafsi waibuke wanawake wengine wasonge mbele mpaka waifikie Tanzania wanayoitaka.

 

Amewataka kuweka pembeni ubinafsi na makundi na kuchagua kwa haki viongozi wa baraza hilo huku akiwataka waendeleze mapambano ya kuvunjwa kwa katiba ya nchi kwa wanawake hao 19 kuendelea kuwa wabunge licha ya kufukuzwa Chadema.

Leave A Reply