The House of Favourite Newspapers

Mrembo Mbosso Akinikataa, Najiua!

IKIWA umepita mwezi tangu asherehekee na mpenzi wake 40 ya mwanaye, mrembo mmoja kutoka Mombasa, Kenya aliyejulikana kwa jina moja la Munira ameibuka na kumwambia staa wa Muziki wa Bongo Fleva, Mbwana Kilungi ‘Mbosso’ kuwa akimkataa, basi anajiua.

 

Kwa mujibu wa Munira, ametokea kumpenda kimapenzi Mbosso tangu akiwa Yamoto Band akitumia jina la Maromboso enzi hizo, hivyo akalazimika kufunga safari na kuweka kambi katika Ofisi za Wasafi Classic Baby (WCB) zilizopo Mbezi-Beach (Kwa Zena) jijini Dar.

 

“Ninampenda sana Mbosso. Najua Kenya kuna wanaume wengi sana ambao wangenioa, lakini sipo tayari. Nimeuza simu yangu na nimepata nauli ya kuja Dar kumuona Mbosso wangu.

“Nipo tayari kufanya kila kitu kwa ajili yake,” alisema Munira.

 

Mrembo huyo aliongeza kuwa, endapo Mbosso hatakubaliana na ombi lake la kuwa naye kimapenzi, basi atachukua uamuzi mgumu wa kujiua.

“Mbosso nisikilize! Kama hutanikubalia ombi langu, nipo tayari kunywa sumu nife, sitaki kuishi tena. Kama utanikubalia, nitawalea watoto wako wote na kufanya kila ulitakalo.

 

“Nakupenda wewe na upo peke yako kwangu,” aliendelea kusema Munira huku akitokwa na machozi kuonesha msisitizo.

Baada ya kukaa kwa muda katika ofisi hizo, Munira alifanikiwa kuonana na Mbosso, lakini alionesha kutokubaliana naye alichoambiwa.

 

“Eti amenipa nauli ya shilingi 10,000 na kuniambia nirudi kwetu Kenya. Siwezi kurudi kwetu bila kukubaliwa ombi langu na Mbosso. Nampenda jamani!” Alimaliza kusema Munira.

Gazeti la Ijumaa lilimtafuta Mbosso kujibu madai ya Munira kumtaka kimapenzi pia kutaka kujiua endapo atakataliwa ombi lake la kuwa naye kimapenzi.

 

“Siwezi kabisa kumlaumu kwa anachokifanya, lakini atambue kuwa nina familia na watoto. Kitendo cha mimi kujiingiza katika uhusiano tena kwa mtu nisiyemfahamu naweza kusema ni jambo la kipumbavu sana.

“Namtaka arudi tu nyumbani kwao Mombasa,” alisema Mbosso.

 

Mbosso, kabla ya kujiunga na WCB alikuwa Yamoto Band. Aliwahi kudaiwa kuwa katika uhusiano wa siri na mchekeshaji marehemu Boss Martha na kupata mtoto mmoja.

Kwa sasa mkali huyo anayetikisa na Wimbo wa Shilingi akiwa na Reekado Banks wa Nigeria, yupo kwenye uhusiano na Rukia ambaye pia ni mzazi mwenzake.

Stori: Neema Adrian, Dar

Comments are closed.