The House of Favourite Newspapers

Mrundi: Msiogope Ubingwa Simba Lazima

Kaimu Kocha wa Simba, Masoud Djuma.

SIKU chache baada ya kutolewa katika hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi, Kaimu Kocha wa Simba, Masoud Djuma amewashusha presha mashabiki wa timu hiyo akisema atapambana kufa au kupona kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

 

Djuma ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tangu aanze maandalizi ya kukinoa kikosi chake kwa ajili ya kujiandaa na mechi zijazo za ligi kuu ambazo wataanza kucheza na Singida United.

 

Kocha huyo Mrundi, hivi karibuni alikabidhiwa timu hiyo kuinoa akichukua mikoba ya Joseph Omog aliyetimuliwa baada ya kuvuliwa ubingwa wa Kombe la FA na Green Warriors ya Ligi Daraja la Pili.

Kikosi cha timu ya Simba.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Djuma alisema katika kuhakikisha wanatengeneza heshima na imani kwa mashabiki wa timu hiyo, ni lazima watwae ubingwa wa ligi kuu.

“Tayari tumepoteza mataji mawili ambayo ni ya FA na Kombe la Mapinduzi ambayo tumeshiriki na kutolewa, hivyo basi ni lazima tuchukue taji la ubingwa wa ligi kuu.

 

“Najua siyo kazi rahisi kuchukua ubingwa huo wa ligi kuu, lakini kutokana na maandalizi ninayoendelea kuyafanya katika mazoezi yangu nina imani kubwa tutafanikisha malengo yetu.

“Nimeona baadhi ya upungufu

katika kikosi changu niliyopanga kuyarekebisha ikiwemo baadhi ya wachezaji kutoushika mfumo wangu wa uchezaji, naamini malengo yetu yatakamilika,” alisema Djuma.

Simba hadi sasa ipo kileleni mwa ligi kuu ikiwa na pointi 26 sawa na Azam FC inayoshika nafasi ya pili lakini imezidiwa kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Stori; Wilbert Molandi, Championi Jumamosi

CHIRWA ALIVYOSHUSHWA KWA ULINZI WA POLISI

Comments are closed.