The House of Favourite Newspapers

ACP MWAKALUKWA: VYOMBO VYA HABARI MUUNGANISHE NGUVU NA POLISI

0
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, ACP Barnabas David Mwakalukwa,  akiongea na wanahabari wa Kampuni ya Global Publishers, alipowatembelea leo Bamaga-Mwenge jijini, Dar.
Mhariri mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally (wa kwanza kushoto) na Mhariri wa Ijumaa Wikienda, Sifael Paul (wa pili) wakiongea na ACP Barnabas David Mwakalukwa.
ACP Barnabas Mwakalukwa akifafanua jambo.
Saleh Ally akiongea jambo na ACP Barnabas Mwakalukwa.
…Wakiagana.

MSEMAJI wa Polisi nchini, ACP Barnabas David Mwakalukwa, leo amezungumza na wanahabari wa Kampuni ya Global Publishers, alipowatembelea ofisini kwao ambapo ilikuwa ni sehemu ya kujitambulisha kwao baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo hivi karibuni.

Jeshi la Polisi hivi karibuni limekuwa likifanya mabadiliko katika nafasi zake mbalimbali ambapo awali nafasi ya Mwakalukwa ilikuwa ikishikiliwa na ACP Advera Bulimba ambaye amepangiwa majukumu mengine.

Mwakalukwa amevitaka vyombo vya habari kushirikiana kwa hali na mali (kuunganisha nguvu) na jeshi la polisi ili kufichua maovu yanayofanyika kwenye jamii kwa lengo la kuimarisha amani ya nchi na usalama wa raia.

Aidha ameiomba Global Publishers kushirikiana na jeshi hilo kutoa elimu ya sheria na usalama wa raia kupitia magazeti yake ya Uwazi, Ijumaa, Championi, Amani, Risasi na mitandao yake ya kijamii ili elimu hiyoiwafikie wananchi wengi zaidi hasa vijijini jambo ambalo litaweza kupunguza uhalifu kama mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina.

Mbali na hayo, Mwakalukwa alitoa rai kwa vyombo vyote vya habari kuacha kuripoti matukio pekee, badala yake waripoti matukio na kutoa maoni kwa jeshi la polisi yatakayolisaidia jeshi hilo kudhibiti na kukomesha hali ya uvunjifu wa amani hapa nchini.

Msemaji huyo wa polisi alimaliza kwa kuipongeza Global Publishers kwa kazi nzuri ya wanayoifanya ya kufichua maovu kupitia Kikosi chake cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) jambo ambalo linalirahisishia jeshi hilo kutekeleza wajibu wake.

PICHA: RICHARD BUKOS NA SWEETBERT LUKONGE.

Leave A Reply