The House of Favourite Newspapers

Msemaji Wa Serikali Ataja miradi Inavyotekelezwa, Atoa pole Kwa Waandishi – Video

0

Katibu Mkuu Wizara Ya Habari  na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi, leo Machi 15, 2020 amezungumza na wanahabari katika Ukumbi wa Idara ya Habari, Dodoma na ametoa pole kwa waandishi wa habari mkoani Morogoro waliopata majeraha kutokana na kulipukiwa na mitungi ya gesi wakati wakitekeleza majukumu yao. Amesema Serikali inaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo. Pia ameeleza mambo mbalimbali yaliyotekelezwa na Serikali kufikia mwaka huu.

Kuhusu Corona, Dk Abbasi amesema; “Tumejiandaa katika kanda zote, pale Dar es Salaam kuna eneo tumelitenga na iwapo akitokea mtu mwenye Corona atapelekwa huko, tunafuatilia na tunapokea maoni ya wataalamu.”

Kuhusu deni la Taifa, amesema; “IMF wametathmini deni letu la Taifa na kuona ni himilivu, wamevutiwa pia na mapambano dhidi ya rushwa na wametambua namna tulivyowekeza katika sekta ya afya, elimu na miundombinu.”

Kuhusu migogoro ya ardhi,amesema;“Mpaka kufikia Machi mwaka huu, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi imetatua migogoro ya ardhi zaidi ya 10,000, pia mapato kwenye sekta ardhi yameongezeka kutoka Tsh Bil 54.1 mwaka 2014/15 hadi kufikia Tsh Bil. 100 kwa mwaka 2018/19

Kuhusu mradi wa maji, amesema; “Mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria unaogharimu Tsh Bil. 600 na kunufaisha wakazi Mil.1.8 katika vijiji zaidi ya 90 katika maeneo yote ya mradi kuanzia kanda ya ziwa hadi kufikia Tabora mjini, Igunga na Nzega, umeanza kunufaisha watumiaji.”

Kuhusu ujenzi wa majengo ya ofisi awamu ya pili, amesema; “Maandalizi ya ujenzi wa majengo ya ofisi awamu ya pili na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami (km 40) katika mji wa Serikali Mtumba unaendelea.Watumishi 15,361 wa Wizara na Taasisi za Serikali wamehamia Makao Makuu ya Serikali, Dodoma, ujenzi wa awali wa Ofisi za Serikali katika mji wa Serikali, Mtumba umekamilika.”

Kuhusu mapato kwenye michezo, amesema; “Natoa onyo, usije ukaleta ujanja ujanja katika mechi zote zinazochezwa kwa kuanzia katika viwanja vya taifa vya Dar es Salaam, tuzisaidie timu, zimekuwa masikini kwa muda mrefu, tunataka kuhakikisha vilabu na serikali vinapata mapato stahili.”

Kuhusu mkopo wa masharti nafuu, amesema;”Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), zimesaini mikataba mitano inayohusu utekelezaji wa miradi mitatu ya kimkakati kwa mkopo wa masharti nafuu ya USD Mil 495.59 ambayo ni sawa na TZS Tril 1.14.”

Kuhusu rekodi ya Mchezo wa Simba na Yanga, amesema; “Mchezo wa Simba na Yanga uliochezwa Machi 8, 2020 umeweka rekodi ya mapato kwa kuingiza shillingi Milioni 545.4 kwa timu na mapato ya Serikali shillingi Milioni 153.2 ambayo hayajawahi kupatikana wakati wote katika historia ya Simba na Yanga.”

Leave A Reply