The House of Favourite Newspapers

MSHINDI SHINDA NYUMBA ASEMA: SIJAAMUA NITAISHI WAPI

0
George Majaba akiwa na familia yake.

BAADA ya kazi kubwa ya muda wa zaidi ya miezi sita ya kuendesha Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili na mshindi wake kupatikana Septemba 27, mwaka huu katika droo kubwa iliyofanyika katika viwanja vya Las Vegas, Mabibo jijini Dar es Salaam, kitu kidogo kilichobakia hivi sasa ni makabidhiano.

Global Publishers ambao ndiyo waendeshaji wa bahati nasibu hiyo, inajiandaa kumkabidhi nyumba hiyo ya kisasa, George Majaba ambaye kazi yake ni kondakta wa mabasi yaendayo kati ya Dodoma Mjini na Vijijini, akiwa ni mkazi wa Makole.

Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho ambaye hivi sasa yupo katika mapumziko mafupi baada ya kufunga ndoa mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema wiki ijayo itafahamika nini kitaendelea kuhusu makabidhiano hayo.

Nyumba aliyoshinda George Majaba.

“Nafikiri nitakuwa katika nafasi nzuri zaidi wiki ijayo ya kusema ni lini tutamkabidhi huyu bwana nyumba yake, niko mapumziko kidogo, tungependa jambo hili limalizike haraka ili maisha mengine yaendelee,” alisema Mrisho.

Kwa upande wake, George Majaba alipoulizwa na Risasi Jumamosi juu ya mipango yake ya nyumba hiyo, kama atahamia na kuendesha maisha jijini Dar es Salaam au ataendelea kuishi Dodoma, alisema kwa sasa hana uhakika nini atafanya.

“Unajua ndiyo kwanza hata kukabidhiwa bado, nasubiri kwanza nikabidhiwe halafu niangalie mazingira ya wapi ninaweza kuishi, kwa sasa siwezi kusema lolote.

“Lakini ninachotaka kuwaambia ni kuwa nimekuwa nikipata simu nyingi na nimepata jukumu jingine la kununua magazeti yenu kila siku na kuyapeleka kule kijijini. Mimi nilikuwa ni msomaji wa gazeti la Michezo la Championi kwa sababu ninaamini ndilo gazeti bora la michezo Tanzania.

“Lakini baada ya kupata ushindi huu, sasa ninapata wageni wengi nyumbani na wote wanataka kusoma magazeti yenu, hivi sasa nalazimika kununua Uwazi, Amani, Risasi na Ijumaa na kila mtu nyumbani anapenda kusoma.

George Majaba akiwa nyumbani kwake Dodoma.

 

“Kule kijijini ninakokwenda, wanataka niwapelekee magazeti ya Global ya kila siku, hapa ninapoongea na wewe ninakwenda kibandani kununua gazeti la Amani, wanataka niwapelekee wasome, unajua pale mwanzo walikuwa wanadhani hili shindano linakuwa limepangwa washindi, lakini baada ya kuniona mimi kama ndiyo mshindi, wameamini ni bahati nasibu kweli.

“Hivi sasa wananunua magazeti na wako tayari kwa shindano lingine linalokuja, ninaomba niwashukuru sana Global Publishers kwa kunifanya niwe mmoja wa wamiliki wa nyumba za kisasa jijini Dar es Salam.”

Hii ni mara ya pili kwa Global Publishers kutoa zawadi ya nyumba baada ya kufanya hivyo mwaka jana baada ya mshindi wa kwanza, Nelly Mwangosi ambaye ni mwenyeji wa Mji wa Iringa.

Leave A Reply