The House of Favourite Newspapers

Msigwa: Hitaji la Watanzania Sio Katiba, Wapinzani Wasubiri – Video

0

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema wapinzani wanatakiwa kuwa na subira kuhusu suala la kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan.

Msigwa ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na kipindi cha Front Page kinachorushwa kupitia +255 Global Radio ambapo alisema ahadi ya kukutana na makundi mbalimbali aliitoa Rais hivyo wawe na subira wakati wao utafika.

 

“Mhe. Rais alisema atakutana na viongozi wa vyama vya siasa, ndio kwanza ana miezi minne madarakani, watulie, muda bado upo mpaka 2025, alishasema atatekeleza, na sio kwamba akitaka kukutana nao yatakuwa matangazo, Mhe Rais anao utaratibu wake wa kuongea na viongozi. Anaweza kukutana nao bila kutangaza,’ alisema Msigwa.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa (kulia) akipokea maelezo ya utambulisho kutoka kwa Mhariri wa Gazeti la Championi Jumatatu, Philip Nkini (kushoto). Wa pili kushoto ni Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho, Meneja wa Global Radio, Lukas Masungwa na Mtangazaji wa Global Radio, Kissa Daniel.

Akiizungumzia hoja ya Katiba Mpya inayodaiwa na wadau wanaosema ndio matakwa ya Watanzania, Msigwa alisema hilo nalo sio kipaumbele kwani Watanzania wanahitaji afya, elimu na miundombinu hivyo Serikali imejikita katika kutekeleza zaidi mambo hayo muhimu.

 

“Unajua hata hao wanaosema Watanzania wanahitaji Katiba Mpya ukiwauliza ni Wanzania gani hawawezi kuwa na majibu. Tuache Serikali ijenge kwanza maendeleo yanayowahusu watu hilo la katiba lipo tu.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa (kushoto) akiteta jambo na Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally.

“Hili suala la Katiba sio kipaumbele cha Watanzania. Wananchi waache kwenda makazini, mashambani waingie barabari, hata hizo dawa hatutazipata wapi. Baada ya miaka mitano huwezi kuwaambia wananchi nilikuwa nahudumia maandamano,” alisema Msigwa.

 

Msigwa aliongezea kuwa, wakati mwingine suala hilo kuliweka kiporo sio dhambi kwani mbali na kuondoa utulivu wa watu kufanya kazi za kujiingizia kipato, linaingiza gharama kwa Serikali.

 

“Labda niwakumbushe Katiba hii ilitaka kufanyiwa mabadiliko mwaka 2013 lakini mchakato ule ulikwama na waliokwamisha ndio haohao wanaoidai sasa hivi. Huwezi kuweka fedha nyingi kwenye jambo ambalo huna uhakika litakamilika au la,” alisema Msigwa.

 

Stori: Erick Evarist

 

Leave A Reply