The House of Favourite Newspapers

Mtambo wa Nyuklia wa Chernobyl Hatarini Kuanza Kuvujisha Mionzi

0

Serikali ya Ukraine imesema zimebaki saa 48 kuanzia leo Jumatano, kabla ya mtambo mkubwa wa nyuklia wa Chernobyl haujaanza kuvuja mionzi hatari ya nyuklia ambayo italeta madhara makubwa kwa Ukraine nzima na nchi inazopakana nazo.

 

Kampuni ya Nguvu za Nyuklia ya Ukraine, Energoatom ambayo ndiyo iliyokuwa ikiufanyia marekebisho mtambo huo, imesema athari kubwa zinaweza kuanza kuonekana baada ya saa 48, kwani umeme kwenye eneo hilo ulikatwa na majeshi ya Urusi na majenereta ya dharura, yanayoendelea kutumika hadi sasa, yameishiwa nguvu.

 

Kampuni hiyo imeongeza kwamba kukosekana kwa umeme kwenye mtambo huo, kumefanya kazi ya kupoza mafuta yaliyotumika kuwa ngumu na kuonya kwamba endapo majeshi ya Urusi hayatawaruhusu wafanye matengenezo makubwa ya dharura, basi balaa kubwa lipo njiani kutokea.

 

Imeongeza kwamba matengenezo yanayoendelea kufanyika hadi sasa, yameonesha kukwama kuzuia tatizo hilo na kuitaka Urusi itoe ushirikiano kwa kurudisha umeme haraka na kuwaondoa wanajeshi wake waliouzingira mtambo huo.

 

Majeshi ya Urusi yaliuteka mtambo huo na kukata umeme katika siku za mwanzo za uvamizi wake nchini Ukraine na kuanzia hapo, vifaru, magari ya kijeshi na wanajeshi wa Urusi, wameendelea kuuzingira mtambo huo.

 

Mtambo huo una historia mbaya ya kusababisha janga kubwa la nyuklia kuliko yote yaliyowahi kutokea duniani ambapo mwaka 1996, ulipata hitilafu iliyosababisha mionzi kuvuja kwa wingi na kusababisha madhara makubwa kwa binadamu na viumbe vingine.

 

Serikali ya Ufaransa kupitia kwa msemaji wake, Gabriel Attal imesema inafanya kila linalowezekana kuzuia janga hilo ambapo ipo kwenye mazungumzo na Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomiki, IAEA na kuisihi Urusi ioneshe ushirikiano.

 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Mnytro Kuleba, kupitia akaunti yake ya Twitter, ameonya kwamba majenereta ya akiba yanayotumia mafuta ya dizeli, hayatakuwa na uwezo wa kuendelea kuzalisha umeme kiwandani hapo baada ya saa 48 kupita kuanzia leo.

 

Kuleba amenukuliwa akisema kwamba endapo majenereta hayo yataacha kufanya kazi, hakutakuwa na uwezekano wa kuyapoza mafuta ya nyuklia na kusababisha mionzi hatari ianze kuvuja.

 

Kampuni ya Energoatom imesema endapo mionzi ya nyuklia ikianza kuvuja, inaweza kuingia kwenye mazingira na kusafiri kwa njia ya hewa mpaka kwenye nchi jirani za  Belarus, Urusi na bara zima la Ulaya.

 

Kampuni nyingine ya nyuklia nchini Ukraine, Ukrenergo imesema kuwa majeshi ya Urusi pia yameuteka mtambo mwingine wa nyuklia wa Zaporizhzhia ambao ndiyo mkubwa zaidi barani Ulaya, ukiwa unazalisha umeme unaotegemewa na nchi nyingi barani humo.

 

Taarifa hizo zimeibua taharuki duniani kote, ambapo taarifa zinaeleza kwamba kutokana na kuzimwa umeme na mitambo ya mawasiliano katika mtambo huo, taarifa za kinachoendelea zimekuwa ngumu kupatikana na idara maalum ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na udhibiti wa nguvu za nyuklia.

Leave A Reply