The House of Favourite Newspapers

Mtibwa, Azam FC Watoleana Vitisho

0

KESHO Jumatatu kuanzia saa 10:00 jioni, Mtibwa Sugar watapambana na vinara wa Ligi Kuu Bara, Azam kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro ukiwa ni mwendelezo wa ligi hiyo.

 

Mtibwa yenye pointi nane ikishika nafasi 14 kabla ya mechi za jana Jumamosi, itakuwa na kazi kubwa ya kuisimamisha Azam ambayo hadi sasa imeshinda mechi zote saba ilizocheza msimu huu ndani ya ligi hiyo.

 

Ofi sa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, amesema: “Haitakuwa kazi rahisi kwa Azam kutwaa pointi tatu katika uwanja wetu wa nyumbani, tunahitaji kupata matokeo mazuri katika mechi zetu zinazofuata kwa kuwa matokeo yetu hayakuwa mazuri huko nyuma.

“Azam wajiandae tu kupokea kipigo, tunahitaji ushindi kwa hali yoyote ile, makocha wetu wamejipanga kuona wanafanya vizuri kwani iwapo watafanya vizuri, basi watajiwekea mazingira ya kuaminiwa zaidi na uongozi.”

 

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Azam, Zakaria Thabith ‘Zaka Zakazi’, alisema: “Tumeanza vizuri msimu huu ambapo mpaka sasa tumefanikiwa kushinda michezo saba ya kwanza na kuandika historia mpya tangu tuanze kushiriki Ligi Kuu Bara mwaka 2008.

 

“Licha ya mafanikio hayo kazi kubwa tuliyonayo kwa sasa ni kuhakikisha haturidhiki bali tunaendelea kulinda kiwango na kasi yetu ili kuendeleza matokeo ya ushindi kwenye kila mchezo ulio mbele yetu.”

Stori: JOEL THOMAS NA KHADIJA MNGWAI,

Leave A Reply