The House of Favourite Newspapers

Mtoto ajifungua mapacha walioungana

0

IMG-20151118-WA0011Tausi Hamdani akiwa na watoto wake mapacha walioungana.

Na Haruni Sanchawa
Hujafa hujaumbika! Mtoto mwenye umri wa miaka 17, Tausi Hamdani (pichani), mkazi wa Wilaya ya Ngara mkoani Kagera amejifungua mapacha wa kike walioungana hivyo kujikuta kwenye wakati mgumu katika maisha yake.

Tukio hilo la kuhuzunisha limetokea kijijini kwao, Rulenge kabla ya kufikishwa kwenye Hospitali ya Kata ya Rulenge, Ngara mkoani Kagera.

Habari zilizolifikia Uwazi kutoka kijijini hapo na kuzifanyia uchunguzi, zilieleza kwamba Tausi aliolewa mwaka jana akiwa na umri wa miaka 16 na kijana aliyetajwa kwa jina la Hamdani Tiholo mwenye umri wa miaka 20.

IMG-20151118-WA0012Baada ya kusimuliwa tukio hilo, mwanahabari wetu aliwasiliana na Diwani wa Kata ya Rulenge, Abroniz Ulindoli ambaye alisimulia kiundani juu ya tukio hilo.

Diwani huyo alisema kuwa baada ya kutokea tukio hilo, mama huyo alifikishwa kwenye Hospitali ya Rulenge ili kusaidiwa kimatibabu katika kuwahudumia watoto hao waliohitaji uangalizi maalum.

Mbali na diwani huyo, afisa mmoja wa Wilaya ya Ngara ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema kuwa mzazi huyo alijifungulia katika Zahanati ya Nyaruma.

Afisa huyo alisema kuwa wazazi wote wa watoto hao walioungana ni vijana wadogo wanaoishi katika mazingira ya shida kwani hawana kazi ya kuwaingizia fedha.
IMG-20151118-WA0017

Watoto mapacha walio ungana.

“Ilibidi ufanyike utaratibu wa kumhamisha Tausi na watoto kwenda Hospitali ya Rulenge ambapo watoto walikuwa wakinyonya maziwa ya mama yao lakini hatua zaidi zilikuwa zinahitajika kwa ajili ya kuwapeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (Mwanza),” alisema afisa huyo.

Kwa mujibu wa taarifa za kiafya za watoto hao, baada ya kuzaliwa Novemba 17, mwaka huu, watoto hao walikuwa na uzito wa kilo 5.2 ambapo walifanyiwa vipimo na Padri Frolence Mchunguzi aliyewapokea hospitalini hapo kutoka Zahanati ya Nyaruma na kukuta uzito wao umepungua hadi kilo 3.6.

Habari zilizolifikia Uwazi wakati linakwenda mitamboni zilieleza kwamba mzazi huyo na watoto wake walikuwa wamehamishiwa katika Hospitali ya Bugando kwa ajili ya huduma kubwa zaidi.

Kwa yeyote aliyeguswa na habari hii na anayetaka kuwasaidia, anaweza kuwasiliana na familia hiyo kwa namba 0787-776 123.

Leave A Reply