The House of Favourite Newspapers

Watoto watatu wafia baharini wakiogelea

0

Abel
Makongoro Oging’ na Mayasa Mariwata

SIMANZI! Watoto watatu wa familia tofauti wakazi wa Kunduchi Mtongani jijini Dar es Salaam, wamekufa maji katika eneo la Bahari ya Hindi lijulikanalo kama Kondo Beach baada ya kuzidiwa na maji wakati wakiichezea meli mbovu iliyo ndani ya bahari mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa mmoja wa wazazi wa watoto hao, vijana hao walimfuata mjukuu wake nyumbani wakimtaka kwenda kucheza kama ilivyo kawaida yao, lakini baadaye alipata taarifa ya kufa maji kwa vijana watatu.

Devota Komba, bibi wa marehemu Abel Osmundi (11) aliyekuwa akisoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mtakuja, alisema watoto hao walimfuata mjukuu wake majira ya saa nne asubuhi na mara nyingi siku za wikiendi, huenda kwa Wakorea ambao huwapa vyakula na vinywaji kisha wanarudi nyumbani.

Andrew“Machale yakanicheza nikawakataza wasitoke, baada ya muda nikajisahau wakaondoka japo sikupata hofu sababu nilijua wameenda kwa Wakorea ambapo si mbali na eneo tunaloishi.

Cha kushangaza wakiendaga huko huwa kwenye saa sita wanarudi, lakini siku hiyo nikaona kimya hadi saa kumi, akaja kijana mmoja na kutuambia tukatambue miili ya watoto wetu Kondo Beach na kukuta mjukuu wangu kafariki, naiomba serikali iitoe hiyo meli mbovu majini,” alisema.

Akieleza jinsi vifo hivyo vilivyotokea, bibi huyo alisema walioshuhudia tukio hilo walimwambia kuwa watoto hao watatu ambao wenzao wawili walioondoka nao nyumbani hawakujiunga kwenye safari ya ufukweni, awali waliingia majini kuchezea meli mbovu ambayo ipo katikati ya bahari, baada ya maji kuanza kujaa wakafanya juhudi za kujiokoa lakini hazikuzaa matunda.

Kwa upande wake, mama mzazi wa mtoto Raphael Agustino (7) aliyejitambulisha kwa jina la Sikitu Joseph alisema anashindwa kuamini kilichotokea, kwa vile hakuwahi kumsikia mwanaye hata siku moja akizungumzia mambo ya beach.
Baba mzazi wa mtoto Andrew Masumbuko (11) aliyejitambulisha kwa jina la Masumbuko Donatus alisema naye alisikitishwa na kifo cha mtoto wake kipenzi, akisema mwanaye hakuwa na tabia za kutembelea ufukweni.

Watoto hao walizikwa Jumapili iliyopita katika Makaburi ya Kondo huko Kunduchi Beach, vifo vyao vimeacha simanzi kubwa kwa wakazi wa eneo hilo huku wakitoa wito kwa serikali kuiondoa meli hiyo mbovu ufukweni hapo.

Leave A Reply