The House of Favourite Newspapers

Mtoto wa Nyerere Kuzikwa Kesho Pugu

0

 

MWILI wa mtoto wa Hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere, Rosemary Nyerere utazikwa kesho Jumatano, Januari 6, 2020 katika Kituo cha Hija, makaburi ya Pugu Misheni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

 

Msemaji wa familia ya Baba wa Taifa, Bhoke Nyerere alisema jana kuwa mwili huo utapelekwa katika makazi ya Hayati Baba wa Taifa Msasani, leo mchana na utalala hapo.

 

Kuhusiana na ratiba ya kuuga, Bhoke alibainisha kuwa hadi juzi jioni, familia ilikuwa inaendelea kushughulikia taratibu za kuuaga mwili huo ambapo familia imepanga kuwa watakaouaga ni ndugu, marafiki wa karibu na viongozi.

 

Pia, alisema ibada ya kuuaga mwili itafanyika katika Kanisa la Mtakatifu Imakulata Upanga jijini Dar es Salaam Jumatano kisha safari ya kwenda makaburi ya Pugu Misheni itafuata.

 

”Mwili utawasili nyumbani, Jumanne (leo) ambapo ukifika utalala hapa nyumbani Msasani, sasa hapo kuna ratiba itatolewa kuhusiana na kuuaga mwili huo hapo naomba nipewe muda zaidi kidogo… lakini Jumatano (kesho) kutakuwa na ibada ya kuaga mwili katika Kanisa la Mtakatifu Imakulata- Upanga, kisha kuanza safari ya kwenda kuupumzisha katika nyumba yake ya milele,” alisema Bhoke.

 

Wakati wa uhai wake Rosemary aliomba kuwa akifa mwili wake uzikwe kwenye makaburi hayo ya Pugu Misheni, makaburi ambayo pia hutumika kama sehemu ya hija kwa waumini wa dini ya Kikristu hasa Wakatoliki.

 

Eneo hili ndipo walipozikwa wafia dini wakati Ukristu unaingia nchini. Mapadre na watawa wengine walivamiwa na wenyeji na kisha kuuawa kutokana na wenyeji hao kupinga ujio wa dini ya ya Kikristu na kufanya makazi katika eneo hilo.

 

Aidha Rosemary alitumia muda wake mwingi kufanya kazi za kiroho kwenye kanisa katoliki lililopo eneo hilo.

 

Watu mbalimbali na viongozi wa serikali wamefika msibani Msasani kuhani akiwemo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dk Asharose Migiro, Mbunge wa Musoma Mjini, Profesa Sospeter Muhongo, na Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima.

 

Leave A Reply