The House of Favourite Newspapers

Mugalu Akomaa Asitoke First Eleven Simba

0

MSHAMBULIAJI tegemeo hivi sasa Simba, Mkongomani, Chris Mugalu, amesema kuwa nafasi anayoendelea kupewa ya kuanza katika kikosi cha kwanza, imempa mzuka wa kuipambania timu yake ili asitoke kikosini.

 

Mkongomani huyo amekuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha kwanza cha Mfaransa Didier Gomes, akimuweka benchi mfungaji bora mara mbili mfululizo wa Ligi Kuu Bara, Mnyarwanda, Meddie Kagere.

 

Mshambuliaji huyo kabla ya kuingizwa katika kikosi cha kwanza, Kagere na John Bocco aliyekuwa anasumbuliwa na majeraha, ndio waliokuwa wakipewa nafasi huku Mugalu akianzia benchi.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mugalu alisema hataki kumuangusha kocha wake Gomes na badala yake atahakikisha anatimiza majukumu yake ya uwanjani ya kufunga na kutengeneza nafasi za mabao.

 

Mugalu mwenye mabao mawili katika Ligi ya Mabingwa Afrika, alisema anaamini uwezo wake wa ndani ya uwanja, hivyo atahakikisha anaipa mafanikio timu hiyo kwa kushirikiana na wachezaji wenzake.

 

Aliongeza kuwa anafurahia ushindani wa namba ambao ameukuta Simba huku akiahidi kuendelea kupambana ili asitoke katika kikosi hicho cha kwanza kinachotetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

 

“Siyo kitu kidogo kwangu kwa kocha kuniamini na kunipa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, hivyo sitakiwi kubweteka na badala yake kuendelea kupambana ili nisipoteze nafasi katika kikosi cha kwanza.

 

“Kikubwa ninafahamu majukumu yangu ya ndani ambayo ninayatimiza kwa asilimia mia moja, hiyo ndiyo sababu ya kocha kuniamini na kunipa nafasi ya kuanza licha ya ushindani uliopo katika timu.

 

“Hivyo sitamuangusha kocha wangu katika kuelekea michezo yetu tuliyoibakisha ya kimataifa dhidi ya AS Vita na Al Ahly pamoja na ligi,” alisema Mugalu.

STORI: WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply