The House of Favourite Newspapers

Muhimbili hii ndiyo tuliyokuwa tunaitarajia

0

HAKIKA Mungu ni mwema kwetu.

Nasema hivyo huku nikikumbuka hali ilivyokuwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili miaka ya nyuma ambapo kulikuwa na malalamiko lukuki kuhusiana na huduma zitolewazo na hali ilivyokuwa wodini.

Leo hii wagonjwa wote waliopo katika hospitali hiyo wanafarijika kwa jinsi huduma za uhakika zinavyotolewa na watendaji wote.

Muhimbili imekuwa kimbilio la wengi wakiwemo viongozi wa serikali na wale wa dini ambao miaka ya nyuma tulikuwa tukiambiwa hata wakiumwa mafua, walikuwa wakikimbilia nje ya nchi kutibiwa.

Sasa Muhimbili tumeweza kuwa na kitengo maalum cha huduma za moyo ambapo ndani ya taasisi hiyo, madaktari wanafanya kazi kwa weledi hata kusababisha kusifiwa na viongozi wetu wa kisiasa na hata wale wa kidini waliotibiwa hapo.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliwahi kulazwa hapo na akapongeza weledi wa huduma  za madaktari na huduma zinazotolewa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika hospitali hiyo ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alitoa pongezi hizo Januari 8, 2016 wakati akizungumza  na waandishi wa habari hospitalini hapo alipokuwa amelazwa kwa uchunguzi wa afya yake na matibabu.

Alisema kwamba awali yeye alikuwa anaogopa kutibiwa hapo kutokana na taarifa potofu zilizokuwa zinazotolewa kwenye vyombo vya habari juu ya operesheni tata zilizowahi kufanyika katika hospitali hiyo miaka ya nyuma na kwamba sasa kitengo cha magonjwa ya moyo cha hospitali hiyo kimemdhihirishia kwamba kina uwezo mkubwa wa matibabu ya moyo kama ilivyo hospitali zingine popote pale duniani.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu alisema kuwa hadi sasa serikali imeokoa kiasi cha shilingi bilioni nne zilizokuwa zipotee kwa ajili ya kupeleka wagonjwa wa moyo kutibiwa  nje ya nchi.

Mufti Mkuu wa Tanzania, Shehe Abubakary Zubeiry Bin Ally naye alilazwa katika hospitali hiyo na baada ya kupona alipongeza huduma bora alizopatiwa katika hospitali hiyo na hakusita kusema kuwa hospitali hiyo ina mabingwa wazuri waliobobea wenye uwezo na endapo wakitumika vizuri hali ya huduma ya afya hospitalini hapo itavutia kama zile zilizoko nje ya nchi.

Jambo muhimu kwa sasa ninalotaka kusema ni kuiomba serikali kuona umuhimu wa kuangalia suala la madaktari, vitendea kazi, pamoja na wauguzi hospitalini hapo ili huduma bora zizidi kutolewa kupita tunazozisifia sasa.

Namuomba Rais Dk. John Pombe Magufuli kuitazama hospitali hiyo mara kwa mara pamoja na mabingwa wetu tulionao kwani Muhimbili ni gereji ya binadamu hivyo panapaswa kuangaliwa kwa makini na kusikiliza matatizo ya watendaji wote.

Ni matarajio yangu kuona viongozi wote wa Tanzania wanatibiwa katika hospitali hiyo. Nasema bila woga kwamba madaktari, manesi na watendaji wengine wa Muhimbili mmetusaidia sana kutuma ujumbe kwa Watanzania kuwa tunaweza kutumia hospitali zetu katika kuwatibu viongozi wetu nchini.

Naamini Wizara ya Afya itaendelea kujitahidi kuboresha huduma za afya hospitalini hapo, ikiwemo suala la wataalam na vifaa vya tiba hospitalini hapo ili Watanzania wote kimbilio letu la kudumu liwe Muhimbili.

Nimalizie kwa kusema Muhimbili hii ndiyo tuliyokuwa tunaitarajia.

 Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply