The House of Favourite Newspapers

Mume wa Bi Harusi Aliyefariki Baada ya Ndoa Azua Taharuki

0
Zainabu Mkiwa enzi za uhai wake.

DAR ES SALAM: Mume wa aliyekuwa Bi harusi aliyefariki saa chache baada ya kufunga ndoa, Zainabu Mkiwa, Yasini Juma, mkazi wa Mtoni Kijichi jijini hapa amezua taharuki kubwa kwa ndugu na jamaa baada ya kutoweka kwenye mazingira ya kutatanisha.

Akizungumza na Gazeti la Amani, ndugu wa karibu wa jamaa huyo alisema kuwa, Yasini alitoweka nyumbani ghafla kwa siku nne bila kuaga wala mtu yeyote kujua mahali alipo kitu kilichoibua hisia za hofu miongoni mwa ndugu, jamaa na marafiki zake.

“Ni kweli Yasini alitoweka ghafla nyumbani kwa siku nne, hakuna aliyejua yuko wapi, tulimtafuta sehemu nyingi kama vile polisi, hospitali, mochwari na kadhalika lakini wapi, baada ya siku nne ndipo akatupigia simu kwa namba yake ya mkononi na kusema alisafiri na kwenda kwa bibi nayeishi Turiani Morogoro.

“Tulipomuuliza kwa nini hakuaga alisema kuwa kulikuwa na tatizo la mtandao,” alisema ndugu huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe.

Mtu mwingine aliyeshtushwa na kitendo hicho ni mama mkwe wake, Husna Ally ambaye alipata wakati mgumu na kuamini mkwe wake anaweza kuwa amepatwa na matatizo kutokana na muda machache uliopita kumpoteza mke wake kipenzi tena saa chache baada ya kufunga naye ndoa.

Mume wa marehemu.

“Nilishtuka baada ya kupata taarifa kuwa mkwe wangu Yasini hajulikani alipo, nilimpigia simu yake akawa hapatikani, nikahisi huenda yupo kwenye matatizo makubwa, lakini namshukuru Allah baada ya siku chache akapatikana hewani, nikawasiliana naye akasema yupo Morogoro na sehemu ambayo yupo mtandao ulikuwa unasumbua,” alisema Husna Ally.

Mwandishi wetu alimtafuta Yasini kupitia simu yake na kuzungumza naye kuhusu kuacha taharuki kwa ndugu zake ambapo alikiri kuondoka nyumbani bila kuaga kwa mtu yeyote kutokana na familia kumchunga sana kwa kuamini bado hayuko sawa kutokana na msiba wa mkewe.

“Nilisafiri na kuja Turiani bila kumuaga mtu kwa kuwa nilijua ndugu zangu wasingenikubalia kwa kuhofia ninaweza kukumbwa na tatizo kutokana na msiba wa mke wangu. Mbaya zaidi eneo nililopo mtandao ni shida kidogo, hadi upande kwenye kilima kidogo ndipo unapata netiweki.

“Siku nne nilipowasha simu na kuwasiliana na ndugu zangu ndiyo nikagundua niliwafanya watapetape kunitafuta lakini mimi niko salama, napumzika kwa muda kisha nitarejea Dar,” alisema Yasini.

TUJIKUMBUSHE

Yasini Juma alifunga ndoa na mchumba wake Zainabu Mkiwa Julai 31, mwaka huu hata hivyo, saa chache baada ya kufunga ndoa, mke wake huyo alifariki dunia kwa maradhi ya tumbo na kuzikwa siku iliyofuatia katika Makaburi ya Sinza, huku tukio hilo likichukua saa 24 tangu kufungwa kwa ndoa yao, kuugua, kufariki na kuzikwa.

STORI: ALLY KATALAMBULA, DAR

Leave A Reply