The House of Favourite Newspapers

Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili – 15

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

“Tiaki,” nilimuita kwa sauti ya upole sana.

“Naam.”

“Ukiniambia ukweli mipango yetu itakwenda sawasawa kama unavyotaka wewe, lakini ukiendelea kunigomea itakufa. Hebu sema ukweli, wewe ni marehemu mume wangu, baba Kisu?”

JIACHIE MWENYEWE SASA…

Tiaki aliniangalia kwa macho yaliyojaa huruma lakini mimi nilikuwa nasubiri jibu lake tu.

“Nakataa mama Kisu. Mimi siyo mume wako baba Kisu. Nilishasema naitwa Tiaki, we unajua. Nimejitambulisha vizuri tu kwamba, nilikuwa rafiki wa mumeo.”

“Mh! Ni kwa nini mtoto wangu akukimbilie na kukuita wewe baba?”

“Sasa ulitaka aniite nani? Mjomba au kaka?”

“Oke, Tiaki tuyaache hayo, lakini mimi nitamwomba Mungu kuanzia leo ili anifunulie kuhusu wewe.”

“Muombe sana na ikibidi mwambie akufunulie hadharani, kusiwe na wasiwasi wowote ule.”

“Sawa,” nilimjibu nikiwa namshangaa kwa nini alijifanya anajiamini sana wakati mimi nilimwona kuwa ni adui yangu kwa kujifanya binadamu mwingine wakati yeye ni binadamu mwingine.

*  *  *

Tiaki aliendelea kukaa hapo huku pia nikijiuliza ni kwa nini anakaa kama nyumbani kwake na wala mimi simdadisi?

Mara simu yake iliita, akapokea na kuanza kuongea:

“Ee, niambie Pinto.”

Hapo tu nikashtuka, Pinto ninayemjua mimi alikuwa rafiki wa marehemu mume wangu,  jamaa yupo kwenye mambo ya leseni za biashara, anaishi Sinza Kwaremi. Tiaki akaendelea kuongea naye:

“Niliongea na mdogo wangu anaitwa Daniel lakini sema hajanipa jibu…”

Niligeuka kumwangalia Tiaki, hata mwanangu Kisu akawa anamkazia macho. Maana Daniel si yule shemeji yangu ambaye naye aliniletea sintofahamu kule kijijini siku ya kumaliza msiba. Na mpaka muda huo sikuwa najua nini kiliendelea kati ya Daniel aliyeonekana ni feki na yule orijino.

Baada ya kukata simu nilimuuliza:

“Huyo Pinto ni nani?”

“Ah! Rafiki yangu mmoja hivi.”

“Anafanya kazi wapi?”

“Yuko kwenye mambo ya biashara.”

“Anaishi wapi?”

“Sinza.”

“Sinza gani?”

“Mh! Sinza gani sijui ile! Hivi pale ukitoka Ubungo mfano, ukapita kwenye makaburi ya yako kushoto kama unakwenda Mwenge ni Sinza gani?”

“Kwaremi?” nilimuuliza.

“Ee, Kwaremi.”

Nilisimama, nikaingia chumbani na mwanangu Kisu nikimwacha Tiaki na msichana wangu wa kazi wamekaa sebuleni.

“Kwani mama, kwa nini baba anakataa kwamba yeye siyo baba angu? Halafu si alikufa lakini, ametokea wapi?” Kisu aliniuliza.

Nilikaa kitandani na mawazo, kwani kauli ya Kisu ilionesha kuwa, mpaka wakati huo anajua Tiaki ni baba yake mzazi ambaye ni marehemu ndiyo maana amesema si alikufa, ametokea wapi?

“Mwanangu Kisu,” niliita huku nikimkumbatia.

“Naam mama.”

“Yule si baba yako, anaitwa Tiaki. Anasema alikuwa rafiki wa marehemu baba yako. Hivi sasa anataka kunioa mimi. Wewe unasemaje Kisu?”

“Mama kubali.”

“Nikubali Kisu wakati mtu mwenyewe ana mawengewenge kama hivi.”

“Mama kubali, wewe si huwa unasali, kubali lakini uwe unasali mama.”

Nilijiinamia kwa muda kuwaza maneno ya Kisu lakini pia nikaanza kuhisi kwamba huenda naye si mwanangu Kisu mwenyewe. Huenda Tiaki amemtengeneza. Hii ni kutokana na maneno yake ya kunitaka nikubali niolewe na Tiaki.”

“Sawa Kisu, nitakubali.”

Nilipomaliza kusema hivyo, Tiaki akaniita kutokea sebuleni, nikaenda na Kisu.

“Mimi sasa naomba niondoke,” alisema.

“Sawa, karibu sana,” nilimuaga nikiwa nimesimama ili kumsindikiza.

Alisimama, akatembea kuelekea mlango mkubwa na mimi nikiwa nyuma yake.

“Utakuja lini tena shemeji?”

“Kesho nitakuja jioni nikitoka mazoezini maana siwezagi kabisa mazoezi ya asubuhi,” alisema Tiaki tukiwa tunapita nje ya kioski kimoja jirani na kwangu.

“Mh!” Niliguna.

“Mbona una guna mama Kisu?”

“Hata,” nilimjibu.

Lakini kusema ukweli niliguna kwa sababu aliniambia habari zilezile. Mume wangu marehemu alikuwa akienda mazoezini kila siku jioni na alikuwa akisema hawezi kwenda asubuhi.

Mbele kidogo nilimuaga Tiaki kwa ahadi ya kukutana kesho yake jioni, nikawa narudi nyumbani.

Nilipofika kwenye kile kioski, mwanamke mmoja anayeishi ndani ya nyumba kubwa alitoka mbio na kuniambia:

“Mama Kisu, yule mwanaume ni pacha wake baba Kisu?”

 

Je, nini kiliendelea hapo? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili wiki ijayo.

Leave A Reply