The House of Favourite Newspapers

Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili -3

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Nikamsogelea, nikawa kama namnyooshea mikono ili kumpa kile kijomela, alipotaka kukipokea, nilishangaa sana kuona sura yake kama ya marehemu mume wangu, yaani vilevile na aliachia tabasamu lilelile, nikashtuka.

SASA ENDELEA NAYO MWENYEWE…

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Nikamsogelea, nikawa kama namnyooshea mikono ili kumpa kile kijomela, alipotaka kukipokea, nilishangaa sana kuona sura yake kama ya marehemu mume wangu, yaani vilevile na aliachia tabasamu lilelile, nikashtuka.

SASA ENDELEA NAYO MWENYEWE… 

“He!” nilisema na kujikuta kile kijomela nimekiachia na kudakwa na huyo ndugu wa mume wangu ambaye alichelewa kufika kisha akakipeleka kinywani kama ishara kwamba na yeye amekubali kunirithi.

Makofi yakapigwa pale lakini nilipowageukia ndugu zangu walionekana kunishangaa na mimi palepale akili zikanirudia na kugundua kuwa, nilitenda jambo kinyume na moyo wangu, nikasema kwa sauti:

“Ah! Sitaki sitaki, mmenichezea.”

Watu walisimama, wifi akanifuata na kuniambia: “Wifi hata mimi nimeshangaa sana, wewe urithiwe na Daniel?! Ni jambo lisilowezekana, kwanza humjui Daniel. Umewahi kumwona hata siku moja?”

“Simjui wifi na sitaki,” nilisema huku namwaga machozi.

Mzee yule aliyekuwa anaratibu au anaongoza shughuli akanishika mkono na kuniambia nitulie. Kweli nikatulia.

“Hebu nikuulize binti, kwani umeona nini? Maana nahisi kama hauko katika mazingira ya kawaida.”

“Mimi bwana nahisi nimechezewa. Si akili zangu. Wakati namfuata huyu kijana nikamwona kama mume wangu.”

“Kivipi?” yule mzee aliniuliza.

“Sura yake na alipotabasamu.”

Watu wote walishangaa sana, akina mama watu wazima wakanong’onezana. Wazee wanaume pia wakaweka chemba kuzungumza. Ilionekana kuna jambo wamelihisi na ndiyo maana waliweka vikundi vidogovidogo.

Lakini cha ajabu, yule kijana akakaza uzi kwamba mimi ni mkewe yeye ni mrithi halali kauli ambayo iliungwa mkono na mzee mmoja aliyesema:

“Hata mimi nakubali. Ukweli ni kwamba, mjane mwenyewe ameamua kutulia kwa kijana na ndiyo maana kijomela amekivusha kote, akakiachia kwa kijana ambaye ni chaguo lake. Mila zetu hazisemi lazima anayetaka kurithiwa awe anamjua mrithi bali zinasema mrithi atatoka miongoni mwa ndugu wa marehemu, finishi.”

Kifupi shughuli ilivunjika, mama mkweli alitulia sana, alikuwa akimwangalia kwa umakini kila aliyekuwa akisema. Sijui moyoni mwake alikuwa akiwaza nini.

Yule mzee aliyekuwa mratibu akasema: “Jamani, mimi ni mtu mzima sana. Nina uzoefu na haya matambiko ya hivi. Huyu mjane ameona kitu, mimi najua na najua kwa sababu najua kitu zaidi.”

Mama mkwe alisimama ghafla na kumfuata yule mzee, akamuuliza:

“Unajua kitu zaidi unajua nini? Hebu kiweke wazi hapahapa kwenye kikao.”

Wifi naye alisimama, akanifuata, akanishika mkono na kunipeleka ndani chumbani kwangu.

“Wifi kwani imekuaje? Daniel? Yaani Daniel ninayemjua mimi awe mrithi wa kaka! Hakuna wifi, kuna jambo. Kwanza ujaji wake si wa kawaida, kaja anakimbia sijui alichelewa wapi.”

Nilibaki nikitetemeka, nilimwambia wifi sina zaidi ya kuondoka asubuhi inayofuatia kwani maisha ya pale kwao kwa siku ile yalinishinda.

Shughuli nje iliisha, watu walitawanyika, lakini Daniel ambaye niliambiwa alikuwa anaishi kwenye mji mwingine aling’ang’ania mimi ni mke wake akitaka tuondoke muda huohuo lakini wifi yangu alimchachamalia na kumtaka aondoke nyumbani la sivyo angemwitia polisi.

“Kwanza hiyo mila mimi sikubaliani nayo. Mtu afe, eti ndugu arithi, je kama kafa kwa maradhi ya kuambukiza,” alisema wifi kwa ukali kabisa wa kunitetea mimi.

Daniel aliondoka zake, sikujua alikwenda kuwaza nini. Lakini kwenye saa mbili usiku nikiwa napangapanga mizigo yangu tayari kwa safari ya kesho yake, yule mzee mratibu wa shughuli alikuja akiwa ameongozana na Daniel.

Wifi alishtuka sana, mama akawakaribisha naye akishangaa kwani Daniel alionekana mpole sana. wakakaa, wote tukakaa. Akaanza yule mzee:

“Jamani, Daniel amenifuata nyumbani kwangu usiku huu na kuniambia jambo la ajabu sana.”

Tukakaa vizuri ili kumsikiliza, akaendelea kusema:

“Anasema amepata habari kwa watu kwamba yeye amekuja kwenye shughuli ya kurithi mke wa marehemu kaka yake wakati mila hizo zimepitwa na wakati. Sasa akaniuliza mimi kwa vile alisikia nilisimamia shughuli je, nina uhakika ni Daniel yeye? Maana leo asubuhi alikwenda mjini na amerudi giza limeshaingia.”

Wote tulishtuka sana, wifi akamuuliza:

“Wewe Daniel una uhakika na unalolisema? Wewe hukuja hapa na kusema ndiye mume wa wifi? Unataka kutupumbaza akili siyo?”

“Dada mimi sijaja. Kwanza hiyo shughuli yenyewe nimeambiwa jana jioni na mzee mjomba Dan. Na nilimwambia kwamba, sitahudhuria kwa sababu tayari nina ratiba yangu nyingine.”

Mh! Wote tuliangaliana, lakini mimi moyoni nilikubaliana na madai ya Daniel kwa sababu ya ile hali iliyojitokeza pale kwenye shughuli. Yule mzee naye akatia neno lake, akisema:

“Ila mimi jamani nakubaliana na huyu kijana, Daniel. Ndiyo maana pale nilisema najua zaidi, mama ukaja juu ukitaka nikiseme hicho ninachokijua. Lakini ukweli ni kwamba, Daniel namfahamu, hawezi kukurupuka kutaka amrithi shemeji yake, wengine wangeweza.”

Mimi nikanyoosha mkono ili niseme, mama mkwe akanikatalia nisipewe nafasi ya kusema:

“Hapana mama, mwache wifi aseme,” wifi alinitetea.

Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili.

Leave A Reply