The House of Favourite Newspapers

Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili – 4

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Mh! Wote tuliangaliana, lakini mimi moyoni nilikubaliana na madai ya Daniel kwa sababu ya ile hali iliyojitokeza pale kwenye shughuli. Yule mzee naye akatia neno lake, akisema:

“Ila mimi jamani nakubaliana na huyu kijana, Daniel. Ndiyo maana pale nilisema najua zaidi, mama ukaja juu ukitaka nikiseme hicho ninachokijua. Lakini ukweli ni kwamba, Daniel namfahamu, hawezi kukurupuka kutaka amrithi shemeji yake, wengine wangeweza.”

Mimi nikanyoosha mkono ili niseme, mama mkwe akanikatalia nisipewe nafasi ya kusema.“Hapana mama, mwache wifi aseme,” wifi alinitetea.
SASA ENDELEA…

“Aseme nini sasa? Mna maana Daniel huyu na Daniel yule aliyerithi pale ni mapacha?” alisema mama mkwe akiwa moto wa kifuu.
“Mama hakuna aliyesema hivyo, ila kuna kitu cha kuangalia,” wifi aliingilia kati mimi nikiwa bado nimenyoosha kidole. Mama akasema:
“Haya sema unachotaka kusema.”

“Kwanza napenda kusema kwamba, hata mimi nakubaliana na shemeji Daniel huyu. Lakini si na Daniel yule wa kwenye shughuli. Yaliyonitokea kabla ya shughuli na yaliyonitokea hata pale kwenye shughuli naamini kabisa kwamba, kuna vitu katika kifo cha mume wangu.”

“Una maana mimi nimemuua?” mama mkwe alidakia.
“Hata kama kaua, lakini si lazima awe na wewe mama. Yule ni mwanao mama, alikuwa anakusaidia kwa kila kitu, usingeweza kuchukua jukumu la kumuua. Ufanye hivyo ili uteseke! Hapana,” nilisema lakini nikiwa na hofu na maneno ya mama.

“Wifi mimi nimekuelewa kwamba, kwenye kifo cha kaka unahisi hapako sawasawa, pana mkono wa mtu badala ya matakwa ya Mungu,” alisema wifi, nikamkubalia kwa kutingisha kichwa.

“Na wewe sijui umekuwaje? Sijui upo upande wa nani?” mama mkwe aliingilia kati tena akimshutumu mwanaye au wifi yangu.

Kwa hasira, mama mkwe alisimama, akaondoka eneo lile. Mimi na wifi tukasimama pia na kuondoka, akabaki yule mzee na shemeji Daniel.

Mimi na wifi tuliingia chumbani kwake, nikafikia kukaa kitandani, wifi akasema:
“Wifi, mama yangu namjua mimi. Wewe jipe ujasiri tu. Naamini hata wewe unamjua. Si mtu wa kusema ana mawasiliano mazuri na wengine. Ni mtibuaji kama vile ulivyoona.”

Nilikubaliana na wifi lakini maneno yake hayakuwa wazi sana kwamba, sasa nijue mama anahusika na kifo cha mume wangu au la! Na kama anahusika ni kwa kiasi gani!
Ilifika muda wa kulala, nikaenda kulala ili nidamkie safari kesho yake.

Kulipokucha, mimi na ndugu zangu tulijiandaa, tukaondoka tukisindikizwa na wifi mpaka kituoni. Mama mkwe hakuwepo, tuliambiwa aliamka asubuhi na mapema na haikujulikana alikwenda wapi!

Tukiwa kituoni, kwa ng’ambo nikamwona Daniel. Lakini nikawa sijui ni Daniel mrithi wangu au yule wa kweli. Lakini niliamini nitajua kwa mwonekano wake. Daniel wa kweli alikuwa na uso wa tabasamu, Daniel mrithi wangu alikuwa na uso wenye hasira.

Tulipogongana uso na Daniel huyu aliukunja, akaonekana kuchukia sana. Mimi nikaachia tabasamu, yeye akazidi kuchukia. Nikamwambia wifi unamwona shemeji Daniel yule ng’ambo?

Cha ajabu, wifi aliangalia ng’ambo kwa muda mrefu lakini akasema hamwoni.
“He! Wifi humwoni Daniel yule kwenye kibanda cha mkaa pale pembeni yake?”
“Wifi acha utani bwana. Pale kwenye kibanda cha mkaa si pana yule mwanamke na wale wanaume wawili wanaongea, mmoja kashika panga?”

“Sasa nyuma ya yule aliyeshika panga humwoni Daniel?”
“Hapana mtu wifi. Kwanza wifi upo siriasi au unataka kunitania tu?” wifi aliniuliza kwa kujiamini.

Nilimshangaa sana wifi kwa kutomwona Daniel. Lakini ghafla akasema:
“Daniel yule kule unakotoka mkokoteni anakuja huku.”
Niliangalia unakotoka huo mkokoteni nikamwona Daniel kweli lakini niliporudisha macho pale kwenye kibanda cha mkaa, nikaendelea kumwona Daniel yule mwingine na nikamwambia wifi naye akawa anashangaa tu lakini hamwoni.

Daniel wa kwenye mkokoteni alipozidi kuja, nilimwona Daniel wa kwenye kibanda cha mkaa akipotea polepole mpaka akafutika kabisa machoni pangu.
Daniel wa kwenye mkokoteni akavuka barabara kuja tulipo huku akiachia tabasamu laini.

Alitusalimia, lakini muda huohuo basi likafika, mimi na ndugu zangu tukapanda, wifi akatupa mkono, shemeji Daniel naye akatupa mkono.

Nilikaa dirishani nikiangalia nje upande wa ng’ambo ya barabara tena nikiwa naangalia kile kibanda cha mkaa, nikamwona tena Daniel yule akiwa ananipungia mkono. Halafu mkono huohuo akafanya ishara kama anayeniambia tutakutana ninakoenda kisha akapotea machoni pangu.

Nilianza kusali sala zote ninazozijua mimi huku nikiendelea kuangalia nje kwa ujasiri wa hali ya juu.
“Hujambo mama Kisu?” nilisalimiwa na mtu kutoka kushoto kwangu kwenye siti niliyokaa. Nikashtuka sana.

Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili.

Leave A Reply