The House of Favourite Newspapers

Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili

0

Tulipotoka kaburini kuzika, ndugu wa marehemu mume wangu waliniambia itabidi nikae pale nyumbani hadi siku arobaini ambapo kwa mila na desturi za kabila lao, msiba huhesabiwa umeisha na kila mwanafamilia anaweza kutawanyika kwenda kwenye shughuli zake.

Nilikubaliana na ushauri huo, nikamwambia mama yangu mzazi atangulie siku ya pili, mimi nitaendelea kubaki mpaka siku hizo arobaini zipite. Mama pia alikubaliana na ushauri wa baba mkwe wangu.

Lakini baada ya kupita wiki moja, wifi yangu mmoja, yaani mdogo wa marehemu mume wangu aliniita chumbani kwake na kuniuliza mambo haya:

Akaendelea: “Hivi we wifi unajua kwamba, siku ya kumaliza msiba ni baada ya siku arobaini?”
Ndivyo anavyoanza kusimulia, Waridi Msafiri au mama Kisu pale alipozungumza na mwandishi wetu kuhusu mkasa mzito uliowahi kumkuta mwanzoni mwa mwaka 2000.

Nilimjibu najua na ndiyo maana niliamua kubaki ili kusubiri siku hiyo. Akaendelea:
“Je, unajua kuwa siku hiyo ndiyo wewe utatakiwa kurithiwa na mdogo au kaka wa marehemu mume wako?”
Nilishtuka sana kusikia maneno hayo. Nikamuuliza ana maana gani kuniambia vile? Akanifafanulia:

“Sisi kwa mila za kabila letu, baada ya kifo cha mume wako, utatakiwa kurithiwa na mmoja kati ya uzao wa baba. Siku ya arobaini kutapikwa pombe halafu familia nzima itakusanyika hapa nyumbani.

Wewe utachotewa pombe kwenye chombo cha kimila mfano wa bakuli, kinaitwa kijomela. Ndugu wa kiume wa marehemu kaka watakaa kuzunguka mahali.
“Itapigwa ngoma halafu wewe ukiwa na kile kijomela chenye pombe utakuwa unapita kwa kila ndugu wa kiume.

Utakayependa akurithi utamkabidhi kijomela. Na yeye kama atakuwa amekubaliana na wewe, akishapokea atakunywa ile pombe kidogo na hapo vigelegele vitapigwa kuashiria kwamba, tayari umeshampata mrithi.”

Mwili wote uliniisha nguvu, nikahisi kutaka kuanguka, lakini nikajikaza sana.
“Wifi, kwani we uko tayari kurithiwa?” aliniuliza wifi yangu.
“Mimi sipo tayari wifi na tena kama ni hivyo afadhali niondoke kesho. Ningejua ningeondoka na mama,” nilimjibu.

“Wifi wala usiwe na wasiwasi. Nilikuwa sijamaliza. Sasa utakapopewa lile bakuli, kama hutataka kurithiwa na mwanaume yeyote katika ukoo wa mume wako, utakunywa wewe ile pombe au kama kuna ndugu yako yeyote, utampa bakuli anywe yeye. Hapo itathibitika kuwa, hutaki kurithiwa.”

Kwa mbali nilifarijika na kauli ya wifi lakini akaendelea kusema:
“Kurithi si suala la lazima. Unaweza kukataa au kukubali. Lakini hata ukikataa huna kesi wala hutaonekana wewe ni msaliti wa mila na desturi. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi.”
“Nashukuru sana wifi yangu, ndiyo maana nakupenda sana,” nilisema. Tukacheka kwa mbali maana bado msiba ulikuwa haujatutoka.

Basi, niliendelea kuwepo ukweni hapo mpaka wiki tatu, tukiwa tumebakiza siku kumi na saba ili kumaliza msiba wa mume wangu.

Siku hiyo, usiku nikiwa nimelala ghafla nilishikwa na haja ndogo, nikatoka kwa lengo la kwenda chooni, kujisaidia. Nikiwa nje ya mlango wa kuingilia chooni, nikasikia mtu amekohoa, lakini sauti ya ukohoaji ni wa marehemu mume wangu, nikashtuka sana.

Sikutaka kukimbia, nilisikiliza kwanza na kubaini kuwa, hakukuwa na kukohoa kokote na huenda mimi nilihisi tu. Nilifungua mlango, nikazama chooni na kumaliza shida zangu.

Niliamka asubuhi iliyofuata bila kumwambia baba mkwe, mama mkwe wala wifi yangu achilia mbali mashemeji zangu wote. Lakini kila baada ya muda, ile hali ilinirudia kichwani ya kuhisi aliyekohoa kule chooni ni mume wangu.

Moyoni nilisema kwamba, kama ni tukio la kweli maana yake litajirudia lakini kama zilikuwa hisia zangu, sitakuja kusikia kitu kama kile tena.
Basi, nilishinda salama, jioni ikaingia. Siku hiyo niliamua kwenda kuoga mapema ili giza likiingia nisishughulike na mambo ya kwenda kuoga.

Nilipeleka maji bafuni kwa kutumia ndoo. Lakini ghafla nikiwa natoka kwenda kuvaa kanga na taulo ili nirudi kuoga, nyuma yangu nikasikia kama mtu anaoga, maji yalilia mwaa, mara ya pili mwaaa! Nikakimbia mpaka kwenye mlango wa kuingilia ndani.
Mama mkwe aliniuliza: “Vipi mwanangu?”

Nilimjibu nimejikuta naogopa tu. akasema pengine ni kwa sababu ya tukio la msiba ambalo limenitokea, nikasema labda mama. Lakini moyoni nilijua nini kilitokea.
Basi, nikaenda kubadili nguo, nikavaa kanga na kujifunga taulo lakini akili ikawa inanipa wasiwasi kurudi bafuni kuoga, niliogopa.

Nilizungukazunguka mpaka mama alipokwenda jikoni ambako ni uani hukohuko na mimi nikaenda bafuni. Kabla sijavua taulo na kanga, nilizungusha macho kuangalia kila pembe ya bafu kama nitaona jambo lisilo la kawaida, lakini haikutokea.

Nilioga, mwishowe nikatoka zangu lakini miguu ilikuwa ikitetemeka. Nilipofika chumbani nilikutana na jipya tena. Kitanda changu nilikitandika vizuri sana, shuka ilikaza vizuri sana lakini cha ajabu ni kwamba, nilikuta alama ya mtu kukaa na kuondoka bila kuweka vizuri shuka.

Halafu juu ya stuli kulikuwa na chupa ya mafuta ya losheni ambayo mimi hujipaka ikiwa imefunguliwa. Ilionesha kwamba huyo aliyekaa kwenye kitanda alikuwa akijipaka mafuta hayo.

Wifi hakuwepo, mashemeji zangu hakuna mwenye tabia ya kuingia mle chumbani, sasa nani?

Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili.

Leave A Reply