The House of Favourite Newspapers

Mungu Ndiye Hupanga Muda wa Kupata Watoto

0

Na Gabriel Ng’osha | IJUMAA WIKIENDA | XX LOve

NINA kila sababu ya kumshukuru M`wenyezi Mungu kwa nafasi aliyonipa, pole msomaji wa XX Love kwa changamoto na magumu mbalimbali unayokutana nayo kwenye maisha yako ya kila siku. Amini tu kuwa Mungu hajakuacha, amekuwa akikupigania usiku na mchana, ongeza juhudi katika kumuomba na milango ya baraka itafunguka siku hadi siku.

Mada ya leo inajikita katika kuzungumzia manyanyaso, matusi na mambo mengi ya ajabu ambayo wanakutananayo wanandoa, hususan wanawake ambao wamekuwa wakibebeshwa mzigo mkubwa na mzito na wanaume wao.

Kinachonishangaza ni kuona binadamu anajivisha mamlaka ya kumtaka mwenza wake awe na mtoto ilihali anajua kabisa kuwa hilo hana mamlaka nalo isipokuwa Mwenyezi Mungu. Si ajabu pengine anayelalamika na kutukana kuwa anahitaji mtoto, yeye mwenyewe hana uhakika kama ni mzima kwa upande wa viungo vya uzazi au mwingine naye unakuta hata yeye hajajua kama akiolewa atapata mtoto au lah!

Mara nyingi chanzo cha tatizo hilo, lawama nyingi hubebeshwa upande mmoja wa wanawake, kwa kuamini kuwa mwanaume yeye huwa siku zote yuko sawa, hawezi kuwa na upungufu katika kukamilisha utungaji wa mimba.

Mbaya zaidi mwanaume anapojiona kuwa faragha yuko vizuri, ndiyo basi kabisa anaona hana sababu ya kushindwa kumlaumu mwanamke kuwa ndiye mwenye matatizo ya kutokushika mimba.

Moja kwa moja anaanza

 kulalamika na kumtuhumu mwenza wake kuwa yawezekana alitoa mimba nyingi kipindi cha usichana wake, mgumba au alitembea na mume wa mtu akafanyiwa figisufigisu.

Kumlaumu mwanamke kuwa ni chanzo cha mwanaume kukosa mtoto ni kumuonea. Kumlaumu mwenza wako kuwa ameshindwa kukuzalia mtoto bila wewe kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu ni unyanyasaji wa kijinsia na ni kuingilia uumbaji wa Mungu. Hata kama akionekana ana tatizo, si vyema kumnyanyasa.

Zipo changamoto zinazowakumba wanandoa kwenye ndoa zao ikiwemo ugomvi wa mara kwa mara, malumbano ya hapa na pale na usaliti. Baadhi ya wanaume wamechukulia tatizo la kukosa mtoto kwa wenza wao kama fimbo ya kuwachapia wenza wao. Kila anapokosea jambo f’lani basi anaanza kusimangwa hata kama mwenye kosa ni mwanaume, lakini kibao kinamgeukia mwanamke.

Suala la mwanamke kutoshika mimba, pamoja na kwamba hata mwanaume anaweza akawa hana uwezo wa kuzalisha mbegu zenye uwezo wa kutengeneza mtoto, ni changamoto kwenye ndoa nyingi katika jamii.

Sehemu kubwa ya jamii inaamini kuwa wanandoa ambao wametimiza mwaka mmoja kwenye ndoa yao basi wanapaswa wawe na mtoto. Kama si mtoto, basi angalau mwanamke awe na mimba changa au kitumbo kiwe kimeanza kuonekana.

Ndugu yangu, si lazima kila ndoa iliyotimiza mwaka mmoja iwe na mtoto au mwanamke awe mjamzito. Suala la kupata mtoto ni uamuzi au majaliwa ya Mwenyezi Mungu. Wewe kama mwanamke huna mamlaka nalo. Wewe kama mwanaume, umebahatika kufunga ndoa na kuishi na mwenza wako, basi shukuru Mungu na hata suala la mtoto siku zote ni majaliwa ya Mungu na si upendavyo wewe.

Nayahisi maumivu makali anayopata mwanamke ambaye hana mtoto na mumewe badala ya kumfariji anageuka kuwa adui yake. Anageuka mtu wa kumnyanyasa. Inauma, inasikitisha na inatesa sana mioyo ya wanawake wengi.

Usikose sehemu ya pili ya mada hii wiki ijayo.

Leave A Reply