The House of Favourite Newspapers

Mwaka unaisha hujatimiza ndoto zako? Simama, jipange upya!

Ndugu zangu, tumebakisha siku chache sana kabla mwaka huu wa 2015 haujaisha. Kila mmoja anajua alichokifanya kwa mwaka huu. Najua wapo ambao wanaumaliza wakiwa na furaha na amani katika mioyo yao kwa kuwa wamefanikiwa kutimiza kwa kiwango cha asilimia 100 yale waliyokuwa wamelenga au wamefikia kiwango cha kuridhisha.

Lakini natambua wapo ambao ndiyo wanashtuka mwaka umeishaa na hawajafanya chochote. Hawa wengi wao wapo katika kipindi kigumu sana. Baadhi yao wamebaki kujiinamia huku wakilalamika kuwa ulimwengu hauna usawa.

Wanashangaa mwaka umeishaje wakati maisha yao hayajabadilika? Wanajiuliza ni kipi walichokifanya kwa mwaka huu, wanabaki na jibu la hakuna. Inauma sana hasa kwa wale ambao siyo makini na maisha yao.

Nasema inauma kwa wasiyo makini na maisha yao kwa kuwa, wapo ambao hawajali, yaani wao bora siku ziende! Hawana muda wa kuyatathmini maisha yao kabisa.

Kwa kifupi hawa si watu makini na naamini wewe unayesoma makala haya si miongoni mwao.

Mtu anayejali maisha yake lazima awe amejiwekea malengo ya kutimiza ndani ya kipindi fulani. Wale walioweka mikakati ya kuhakikisha mwaka huu wanaoa na kujenga familia, au wale ambao walipanga kujenga nyumba na kumiliki magari au kampuni kubwa za biashara ndiyo wanaojua sababu ya kuletwa hapa duniani.

Hawa ndiyo wale ambao wakikwama katika kutimiza yale waliyoyapanga huumia sana. Huenda wewe ni mmoja wa wale ambao wameumaliza mwaka bila kutimiza yale waliyokuwa wameyapanga. Huna sababu ya kuumia na kujiona usiye na thamani ya kuendelea kuishi bali;

Jipe muda tena

Unachotakiwa kujua ni kwamba, bado nafasi ya kutimiza yale uliyoyapanga unayo. Kikubwa hapa ni kuamua kujipanga upya baada ya kujiambia kuwa mwaka ujao lazima utimize yale uliyokuwa umepanga kuyatimiza mwaka huu.

 Kumbuka kuteleza si kuanguka hivyo simama na ainisha upya malengo yako kisha weka dhamira upya.

Wapi ulikosea?

Haiwezekani ushindwe kutimiza malengo yako bila kuwepo sababu za msingi. Hebu jaribu kuchunguza wapi ulikosea. Ukibaini mambo yaliyokufanya usitimize malego yako, jaribu kuyakwepa katika mwaka ujao, naamini kwa kufanya hivyo mambo yatakwenda sawa.

Jifunze kwa waliofanikiwa

Kama nilivyosema hapo awali kwamba, najua wapo ambao wanajiandaa kusherehekea kumaliza mwaka kwa mafanikio. Jiweke karibu na watu hao, jifunze kutoka kwao kwa kuchunguza yapi waliyafanya hadi kutimiza malengo yao. Nina imani kutoka kwao utapata mwanga wa nini cha kufanya.

Ushauri, msaada ni muhimu

Si mbaya kujiamini lakini wengi waliofanikiwa hawakuyategemea mawazo yao tu. Kuna wakati walilazimika kuomba ushauri na msaada pale ambapo waliona kuna ulazima wa kufanya hivyo.

Nawe usisite kufanya hivyo. Usikubali kubaki na msongo wa mawazo pale unapohisi kushindwa badala yake jaribu kuwashirikisha walio karibu yako katika mbio za kuelekea mafanikio.

Usikate tamaa

Katika kujaribu kufikia malengo yako ni wazi utakutana na vikwazo vya hapa na pale na wakati mwingine kuhisi huwezi kuendelea tena.

Siku zote vikwazo unavyokutana navyo viwe ni changamoto kwako ya kujipanga upya na kuanzisha tena mapambano ya kufikia malengo yako.

Usikate tamaa kabisa kwani wanasaikolojia wanaeleza kuwa, idadi kubwa ya watu wanaoishi maisha yasiyokuwa na nyuma wala mbele wametawaliwa na tabia ya kukata tamaa hata katika mambo ambayo wakiwa wavumilivu wanaweza kufanikiwa.

Comments are closed.