The House of Favourite Newspapers

Mwakinyo Amuomba Radhi Matumla

0

BONDIA Hassan Mwakinyo, ameamua kuweka tofauti zake pembeni na bondia mkongwe Tanzania, Rashid Matumla baada ya jana kumuomba radhi mbele ya Watanzania.

 

Mwakinyo ambaye Ijumaa iliyopita alimpiga kwa pointi Mfilipino, Arnel Tinampay katika pambano la raundi kumi lilisokuwa la ubingwa lililofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, aliingia kwenye mgogoro na Matumla baada ya bondia huyo mkongwe kumkosoa licha ya kushinda kutokana na kubaini mapungufu yake.

 

Akizungumza wakati wa kuomba radhi kutokana na matamshi yake ya awali kuonekana ni kama dharau kwa bondia huyo mkongwe, Mwakinyo alisema: “Matumla ni kama mzazi wangu, ni kocha ambaye niliwahi kufanya naye mazoezi na bado ana nafasi ya kunifundisha. Yote kwa yote kila mwanadamu anakosea, naamini na yeye amenielewa, kila kitu kitakuwa sawa.”

 

Naye Matumla alisema: “Huyu ni kama mwanangu, mwenyewe ameshasema hapa kwamba nilishamfundisha, nimepokea radhi yake, sina kinyongo. Nashukuru kwa kuja mbele za watu kuniomba radhi, kama utakuwa na tatizo, nipo tayari kukusaidia.”

 

Baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye Studio za Azam TV na kurushwa moja kwa moja na Chaneli ya Azam Sports 2 jana mchana, wawili hao wakashikana mikono, kisha wakakumbatiana, mwisho wakapiga picha ya pamoja kudhihirisha kwamba wamezizika tofauti zao za awali.

MWANDISHI WETU,Dar

Leave A Reply