The House of Favourite Newspapers

Mwakinyo, Ndugu wa Pacquiao Ulingoni Novemba 29

BONDIA wa kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo anatarajiwa kupanda ulingoni Novemba 29, mwaka huu kupambana na Arnel Janiola Tinampay raia wa Filipino.

 

Pambano hilo limepangwa kupigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam litakalotanguliwa na mapambano matano ya utangulizi.

 

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mwakinyo ambaye anadhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa alisema anapigana na bondia huyo baada ya yeye na menejimenti kumuona anakidhi vigezo vya kupigana naye.

 

Mwakinyo alisema ameshindwa kupambana kwa muda mrefu baada ya kumpata bondia atakayekidhi vigezo, hivyo Tinampay ambaye ametokea kwenye gym ya bondia Emmanuel ‘Manny’ Pacquiao kutoka nchini huko.

 

“Mimi kwa kushirikiana na menejimenti yangu kwa pamoja tumejiridhisha kuwa Tinampay ni bondia aliyekidhi vigezo vya mimi kupigana naye baada ya kukaa pamoja na kufikia makubaliano mazuri ya kumleta nchini kuja kupigana naye.

 

“Ni kati ya mabondia bora na namba moja kwenye uzito wa Kg 69 nchini Filipino ambaye nitapambana naye ulingoni kwa ajili ya kumuonyeshea uwezo wangu, hivyo ninawaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi siku hiyo kwa ajili ya kunisapoti,” alisema Mwakinyo.

 

Mratibu wa Pambano hilo, Jay Msangi alisema: “Pambano hilo linatarajiwa kuwa la raundi kumi litakalokuwa na mapambano mengine matano ya utangulizi.

“Tayari tumepokea maombi ya mabondia mbalimbali kutoka Marekani, Indonesia na Kenya wakiomba kupanda ulingoni siku hiyo ya kihistoria,” alisema Msangi.

Comments are closed.