The House of Favourite Newspapers

MWAKYEMBE Afanya Maandalizi, Kuwakutanisha DIAMOND, ALIKIBA

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe

DAR ES SALAAM: Kufuatia madai ya muda mrefu ya kuwepo kwa bifu kubwa kati ya mastaa wakubwa wa muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Ali Salehe Kiba ‘King Kiba’, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amefunguka na kueleza anachokiamini kuhusiana na bifu hilo.  

 

Waziri huyo alifunguka hivi karibuni alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati alipotembelea ofisi za Kampuni ya Global Publishers, wachapishaji wa Magazeti ya Ijumaa, Uwazi, Ijumaa Wikienda, Amani, Risasi, Championi na Spoti Xtra baada ya kuulizwa swali kwamba, yeye kama waziri na mlezi wa wasanii amechukua hatua gani kulishughulikia bifu la wasanii hao ambalo linaonekana kutokuwa na afya kwenye sanaa ya muziki.

Katika kujibu swali hilo, Dkt. Mwakyembe alisema kuwa, yeye hadhani kama kuna tofauti kubwa kati ya wasanii hao bali anaona kwamba mashabiki ndiyo wanaolikuza bifu hilo kwa sababu wanazozijua wenyewe.

Alisema kuwa, mara kadhaa amekuwa akikutana na mastaa hao kwa nyakati tofauti na katika maongezi yao hawaoneshi kuwa wana bifu, jambo linalomfanya aamini hakuna tatizo kati yao. “Sidhani kama kuna bifu kubwa kama inavyoelezwa, ninachojua Diamond na Kiba hawana tofauti ya kiivyo, nimewahi kukutana nao kwa nyakati tofauti na hawaoneshi kuwa wana tatizo.

“Nahisi mashabiki wa hawa wasanii wawili ndiyo wanaolikuza hili bifu. Lakini pia mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari vikishaandika ndipo inaonekana kuna shida lakini kumbe siyo hivyo.

“Labda niseme tu kwamba, kuna kitu naandaa na hivi karibuni mtawaona pamoja na hiyo itawafanya muamini kuwa hawana bifu kama inavyojaribu kukuzwa,” alisema Dkt. Mwakyembe ambaye kwenye ziara yake alikuwa ameongozana na Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza na maafisa wengine.

Diamond na Kiba kwa muda mrefu wamekuwa wakitajwa kuwa kwenye bifu kubwa ambapo mbali na mara kadhaa kurushiana maneno makali, wanapokutana hawachangamkiani na hata namna wanavyosalimiana najua kabisa kuna kitu kati yao.

 

Mbali na hivyo, wasanii hao hawajawahi kufanya kolabo ya aina yoyote wala shoo ya pamoja na wanapokuwa wanafanyiwa mahojiano na vyombo vya habari kisha kuulizwa tatizo ni nini, kila mmoja amekuwa siyo muwazi.

SHOWBIZ XTRA

Comments are closed.