The House of Favourite Newspapers

Mwakyembe Aipongeza Dasani Marathon Kwa Kuibua Vipaji

0
Mkurugenzi wa Michezo katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Yusufu Singo, akizungumza jambo.
Washindi wa kwanza na watatu wa mbio za km. 21 wakiwa katika picha ya pamoja.
Washindi wa mbio za km 10 wakiwa katika picha ya pamoja na zawadi zao.
Washindi wakiendelea kukabidhiwa zawadi zao.
Mshindi wa kwanza wa mbio za km 10 upande wa wanaume, Sylivester Simon akikabidhiwa zawadi.
Mmoja wa wanariadha akiwa katika pozi baada ya mashindano.
Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Coca-Cola Kwanza waliokuwa wadhamini, Nalaka Hettierachchi, (kulia) akimkabidhi zawadi mshiriki.
Baadhi ya washiriki wakiwa katika pozi baada ya kumalizika kwa riadha.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe ameyasifia mashindano ya mbio ya Dasani Marathon 2017 yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam kwamba yanaibua vipaji vipya vya wanariadha kwa hiyo yaungwe mkono.

Kauli hiyo ilitolewa kwa niaba ya waziri huyo kupitia kwenye hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Michezo wa wizara hiyo, Yusufu Singo, wakati wa kukabidhi zawadi kwa washindi wa mashindano hayo yenye umbali wa kilimita 10 na  21.

Pia aliipongeza Dar Running Club kwa maandalizi mazuri yaliyofanikisha mashindano hayo yaliyokuwa yanadhaminiwa na kampuni ya Coca- Cola Kwanza kupitia maji ya Dasani.

“Nawapongeza nyote kwa kuchukua jukumu kubwa la kufanikisha maandalizi ya mbio hizi ambayo siyo tu ni zito bali muhimu katika mchakato mzima wa kujenga utamaduni wa kuzijali afya  zetu na ustawi wa familia zetu, uelewano ulio thabiti katika kutekeleza majukumu yetu ya kifamilia na kitaifa,” ilisomeka hotuba hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Coca-Cola Kwanza, Nalaka Hettierachchi, alisema wanataka mashindano hayo yawe makubwa na hivyo wana mpango wa kuyapeleka mikoa mingine nchini.

Mashindano ambayo yalishirikisha zaidi ya watu 1,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini, yalianzia Bwalo la Maofisa wa Polisi Oyster Bay na kupita barabara mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam.

Aliyeibuka kidedea katika mbio za wanaume za umbali  wa km 21 ni, Augustine Sule, wa pili akiwa Stephano Huche na Said Makula aliyeshika nafasi ya tatu.

Kwa upande wa wanawake aliyeibuka mshindi ni Jacqueline Sakilu, wa pili akiwa  Noela Remmy na nafasi ya tatu ilikwenda kwa Antery John.

Kwa mbio za umbali wa km 10, mshindi kwa upande wa wanaume alikuwa Sylvester Seleman, wa pili akiwa  Daniel Sinda na Paul Pascal alishika nafasi ya tatu. Kwa upande wa wanawake mshindi alikuwa Mary Naari, wa pili akiwa Sara Hitis na Asia Seleman aliyetwaa nafasi ya tatu.

Kwa upande wa walemavu aliyeshinda ni Shukuru Khalfan, wa pili Mathias John na Jonis Stephano alishika nafasi ya tatu.

Mshindi wa kwanza wa mbio za km 21 kwa upande wa wanaume na wanawake kila mmoja alikabidhiwa sh. mil 1, wa pili sh. 750,000 na wa tatu sh. 600,000.

Leave A Reply