The House of Favourite Newspapers

Mwamnyeto: Bado Kidogo Tu Nasaini Yanga SC

0

NAHODHA na beki wa kati wa Coastal Union ya Tanga, Bakari Nondo Mwamnyeto amesema kuwa kama mazungumzo yakienda vizuri, basi huenda akatua kukipiga Yanga siku chache zijazo.

 

Beki huyo ni kati ya wachezaji wanaotajwa kwenye usajili wa msimu ujao katika kuiimarisha safu ya ulinzi ya timu hiyo inayoongozwa na Mghana, Lamine Moro, Kelvin Yondan Ally Mtoni ‘Sonso’, Andrew Vicent ‘Dante’ na Said Makapu.

 

Awali, beki huyo alikuwa anawaniwa vikali na Simba iliyokuwa na mipango ya kumsajili katika kuiboresha safu yao ya ulinzi inayoongozwa na Pascal Serge Wawa na Erasto Nyoni kabla ya kushindwana kwenye dau la usajili ambalo ni Sh Mil. 100.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Mwamnyeto alisema kuwa Yanga ndiyo iliyoonyesha nia kubwa ya kumpa mkataba wa miaka miwili kukipiga Jangwani Aliongeza kuwa, kabla ya Yanga zilikuwepo baadhi ya klabu zilizoonyesha nia ya kumsajili ambazo ameshindwana nazo huku akificha majina ya timu hizo, lakini gazeti hili linafahamu Simba ilikuwa mojawapo.

 

“Ni mapema kuzungumzia wapi ninakwenda, kwani bado muda wa usajili na isitoshe bado nina mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea Coastal.“Lakini nipo kwenye mazungumzo mazuri na Yanga, kama mazungumzo yakienda vizuri basi nitasaini kuichezea baada ya usajili kufunguliwa, hivi sasa nakamilisha baadhi ya vitu vya msingi ndani ya klabu yangu ninayoichezea.

 

“Kikubwa ninachokiangalia hivi sasa ni maslahi pekee yatakayonifanya nisaini Yanga, nafahamu zipo klabu nyingine zilizokuwa kwenye mipango ya kuwania saini yangu lakini nimeshindwana nazo katika maslahi na siyo kingine,” alisema Mwamnyeto.

 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Uwekezaji wa Kampuni ya GSM, Injinia Hersi Said juzi alisema kuwa wameandaa utaratibu mzuri wa utambulisho wa wachezaji wao wapya watakaowasajili kabla ya siku ya tamasha lao kubwa la Wiki ya Mwananchi, ambayo wanaitumia kutambulisha wachezaji wote watakaowatumia katika msimu ujao.

 

“Lengo letu ni kuona tunafaidika na mauzo ya jezi mpya kupitia wachezaji wapya tuliowasajili kama ilivyokuwa kwa Morrison (Bernard) ambaye mauzo yake ya jezi ndiyo yaliyoyoongoza kwa usajili uliopita,” alisema Hersi.

Stori: Wilbert Molandi,Dar es Salaam

Leave A Reply