The House of Favourite Newspapers

TOP FIVE TOP MARAPA WAKALI KIZAZI KIPYA BONGO!

0

MUZIKI wa Hip Hop hapa Bongo ulikuzwa na wakongwe kama Joseph Haule ‘Professor Jay’, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Fareed Kubanda ‘Fid Q’, Selemani Msindi ‘Afande Sele’ John Makini na wengine kibao hadi kufika hapa ulipo.

Wakali hao kwa sasa wana mishe zao, wengine hawasikiki. Lakini wakati wakongwe hao wakianza kupoa, kuna kizazi kipya cha Hip Hop Bongo ambacho kinafanya vizuri kwa sasa.

Hii hapa Top Five ya makinda katika gemu la Hip Hop:

COUNTRY BOY

Jina lake halisi ni Ibrahim Mandingo, ni msanii ambaye amekuwa akifanya poa kwa kipindi kirefu. Turn Up, Kibegi, Yule Boy, Leo, Litakufa Jitu, Kama Ulaya, Wanaona Haya na nyingine nyingi, ni ngoma ambazo zimemfanya afanikiwe kutoa album yake aliyoipa jina la Yule Boy na imebeba ngoma yenye ngoma kali sana.

ROSA REE

Rosary Robert ni moja ya wasanii wa kike wa Hip Hop ambaye amekuwa akifanya poa sana, amefanikiwa kutoa ngoma kali japo mwanzo alitambulika na ngoma kama Up In The Air akiwa na ya lebo ya muziki ya The Industry chini ya Navykenzo ‘Aika na Nahreel’ ambao walikuwa wakisimamia kazi zake na baadaye kujitoa katika lebo hiyo.

Aliendelea kutamba na vibao kama Banjuka, Asante Baba, Nguvu za Kiume, Dip n ‘Whine it, Nazichanga na kolabo nyingi za kimataifa.

YOUNG LUNYA

Alianza kuonekana akiwa na kundi la OMG chini ya Switcher Records ya msanii Quick Racka, akitambulika na kibao kama Umbea ambacho walifanya na Baraka The Prince na kufanya vizuri sana akiwa na kundi hilo ambapo baadaye akaamua kusimama na kutoa kazi zake yeye mwenyewe.

Aliendelea kuonekana katika kolabo mbalimbali za wasanii wakubwa kama Joh Makini katika kibao cha Mchele na sasa anawika katika ngoma ya Bedroom Remix ya msanii Harmonize, mbali na hizo ameachia ngoma zake mwenyewe kama Tikisa akiwa na Country Boy, Moto na nyingine nyingi.

FRIDA

Frida Amani, uwezo wake wa kuchana freestyle unanifanya nimuweke katika orodha hii kwani tangu ametoka katika mashindano ya Bongo Star Search 2015, hakubweteka alitoa ngoma kali kama Mimi na Wewe, Pull Up, Tuone akiwa na G Nako, na nyingine nyingi. Mbali na hilo, pia ni mtangazaji katika kituo cha redio.

MONI CENTROZONE

Awadh Chami ni jina alilopewa na wazazi wake, mchanganyo wa melodi katika ngoma zake hakika unanivuta kumpachika katika gurudumu hili, kwani amekuwa akifanya ngoma kali na kushirikiana na wasanii wakali.

Ngoma kama Lamoto imekuwa ikitikisa katika vyombo mbalimbali vya habari, nyingine ni kama Chuchu Dede na Godoro. Uwezo wake umempa tiketi ya kushiriki katika ngoma ya mkali wa Bongo Fleva Harmonize ya Bedroom Remix.

MAKALA: Happyness Masunga, Risasi

Leave A Reply