The House of Favourite Newspapers

Mwanamke Alivyomfanya Zezeta Kaka Yangu – 30

0

Tulikuwa tumefika mjini Lilongwe Malawi, yule mzee Mganga akasema hatuwezi kwenda kwa yule mwanamke aliyemfanya kaka Edgar zezeta bila kuwa na polisi.

“Unajua yule mama ananijua, akiniona tu tunaingia nyumbani kwake anaweza kutufanyia kitu kibaya sana. Anaweza akapiga kelele kwamba sisi ni wezi, tukamalizwa,” alishauri yule mganga.

Je, polisi watakubali kufuatana nao? SONGA NAYO:

Tuliangaliana mimi na kaka Ipacho lakini kabla ya sisi kusema chochote kuhusiana na ushauri huo, mzee Makang’ako alikohoa kidogo kisha akasema.

“Twendeni sentro polisi kuna shemeji yetu pale, yeye ni kamishna wa polisi, atatusaidia.”

“Kama ni hivyo ni vizuri kwa sababu lazima tuwe na polisi.” Akasisitiza mganga.

Bwana Makang’ako alimpigia simu huyo afisa wa polisi na akamthibitishia kuwa yupo ofisini. Alitaka kujua shida yake lakini hakumwambia kwa ahadi kwamba atamjulisha kila kitu wakionana uso kwa uso.

Tulipanda gari na tukaelekea kwenye hicho kituo cha kati cha polisi cha pale Lilongwe. Tulipofika, mimi, bwana Makang’ako na yule mganga tukapanda juu ghorofani kumuona huyo afisa wa polisi na kaka Ipacho yeye alibaki kwenye gari akililinda.

“Karibuni,” aliitikia mtu aliyekuwa ndani.

Bwana Makang’ako alifungua mlango na sisi tukamfuata kwa nyuma.

Tuliingia ndani na kukutana na kaka mmoja ambaye nilihisi kwamba ni katibu mnyeka wake, baada ya kusalimiana na kumueleza kusudio letu la kuwa pale, akaturuhusu kufungua mlango wa bosi wake.

“Ohh shemeji, karibu wewe na wageni wako,” alisema mtu ambaye ni mnene na ana sharafa nyingi lakini alikuwa amezinyoa bila shaka kutokana na maadili ya kazi yake, alikuwa amekaa na mezani kulikuwa na majalada mengi bila shaka ya kesi mbalimbali.

“Ketini kwenye makochi hapo, namalizia kazi moja, nitachukua dakika mbili-tatu,” alisema.

Tuliketi niliiangalia ofisi hiyo, ilikuwa kubwa sana maana ilikuwa na nafasi ya kutosha na kulikuwa pia na meza ya mkutano, friji ndogo ilikuwepo na tivi bapa ilikuwa ukutani karibu kabisa na picha kubwa ya rais wa nchi.

Yule kijana aliyetupokea aliingia na kutuuliza kama tunataka chai, kahawa, maziwa, soda au maji. Wote tulimuomba atuletee maji ya kunywa. Alikwenda kwenye friji na kuifungua, nililitupia macho na kuona kuwa ndani yake kulikuwa na vinywaji vyote alivyovitaja na matunda.

Nikasema kimoyomoyo kuwa huyu bosi anajali sana afya yake kwa sababu sikuwahi kuona bosi ana friji ofisini lenye kila kitu kama yeye.

Yule kijana alituletea maji na glasi na kuweka mbele yetu, akatukaribisha.

Wakati tunaendelea kunywa maji yule bosi alitoka mezani kwake na kuungana nasi. Tulisalimiana na mazungumzo yakaanza.

Tulimueleza kisa cha kuja pale na jinsi taarifa za kifo tulivyopata na mganga anavyoona.

“Yule mama tunamjua, ni kweli ana tabia hiyo, ngoja niandae polisi twende. Safari hii nataka nikashuhudie mwenyewe,” alisema.

Je watafanikiwa kumtia mbaroni? Fuatilia Jumanne ijayo.

Leave A Reply