The House of Favourite Newspapers

Mwanamke Jini Alivyonipenda na Kunipeleka Ujinini! – 4

0

ILIPOISHIA

Nikafungua mlango wa gari na kujipakia. Nikajaribu kuliwasha gari hilo bila mafaniko.

“Mafuta yamo?” msichana akaniuliza.

“Nilitia mafuta ya kutosha.”

“Sasa itakuwaje?”

“Kama itawezekana, ningekuomba unisaidie kulivuta hili gari. Nikiliacha hapa linaweza kuibiwa”

“Sawa, nitakuvuta.”

“Nitakushukuru sana dada yangu.”

Msichana alirudi kwenye gari lake akalirudisha kinyumenyume hadi likakaribia nilipoliegesha lile gari. Akashuka na kuchokonoa kamba  ya chuma iliyokuwa nyuma ya gari lake. Tukasaidiana kulifunga gari lililozimika sehemu ya mbele.

SASA ENDELEA…

“Panda gari lako twende,” tulipomaliza aliniambia.

 

Nikajipakia kwenye gari hilo na yeye akaenda kupanda kwenye gari lake, akatia gea na kuanza kulivuta.

Tuliendelea kwa mwendo mdogo hadi tukaingia mjini. Tulipofika eneo la Kisosora alisimamisha gari na mimi nikafunga breki. Akashuka na  kunifuata.

“Unaishi wapi?” akaniuliza kwenye mlango wa gari.

“Ninaishi Chuda.”

“Chuda sehemu gani?”

Nikamuelekeza.

“Sasa ngoja nikupeleke.”

Dakika chache baadaye tuliyasimamisha magari hayo mbele ya nyumba yangu katika eneo la Chuda. Msichana alishuka na mimi nikashuka.

“Asante sana kwa msaada wako.” Nilimshukuru msichana huyo aliyeonesha kuwa pesa haikuwa tatizo kwake na pia alionesha alikuwa na moyo wa kibinadamu sana.

“Unaishi hapa?” akaniuliza.

“Hii ndiyo nyumba yangu.”

“Nimefurahi kuifahamu. Asante sana. Kwa hiyo asubuhi utalipeleka gereji?”

“Itabidi nilipeleke na bado nitapata tatizo la gari ya kunivuta.”

“Ulihitaji kulipeleka gereji saa ngapi?”

“Mapema tu, kama saa tatu hivi.”

“Naweza kuja kukuvuta tena?”

“Sitapenda kukusumbua tena dada yangu. Msaada ulionipa unatosha.”

“Sasa utafanyaje?”

“Nitatafuta hata gari la kukodi linivute.”

Msichana alitoa kicheko laini na kurudi kwenye gari lake. Wakati anafungua mlango ajipakie aliniambia:

“Nitakuja kukuvuta, usijali. Leo ni wewe kesho mimi.”

Akajipakia na kuliwasha gari. Nikabaki nimesimama nikilitazama gari hilo likiondoka.

Nilikuwa na hakika kwamba yule msichana nilikuwa simfahamu lakini jambo la ajabu ni kuwa alionesha kunichangamkia tangu tulipokutana kwenye harusi ya rafiki yangu na zaidi ya hapo alinionesha ubinadamu wa hali ya juu.

Baada ya kuwazi peke yangu nilifungua  mlango nyumbani kwangu na kuingia.

Nilikwenda kuoga kisha nikajilaza kitandani na kuutafuta usingizi uliokuwa umenipotea. Ile picha ya wale watu warefu niliowaona kule msituni ilinijia akilin. Nikajiuliza watu wale walikuwa kina nani? Walikuwa wanatoka wapi na wanakwenda wapi?

Hivi kuna viumbe warefu wa aina ile? Niliendelea kujiuliza. Kwa kweli nilipowaona nilitishika sana. Kweli msitu una mambo mengi na usiku pia kuna mambo mengi yanayojitokeza, mengine ni ya ajabu kabisa.

Nilijiambia kwamba kama si yule msichana kutokea na kunipa msaada, wale viumbe wangeweza kurudi na kuniletea rabsha.

Baada ya kuwaza kwa dakika kadhaa, usingizi ulinipitia nikalala hadi asubuhi.

Baada ya kumaliza kuvaa nilisikia gari likisimama huko nje. Sikujua llikuwa gari la nani. Baadaye kidogo nilisikia mlango ukibishwa.

Baada ya kumaliza kuvaa nilitoka chumbani na  kufungua mlango wa mbele. Nikashituka nilipomuona yule msichana aliyenikokota na gari lake usiku uliopita.

Alikuwa amesimama mbele ya mlango akitabasamu.

“Yakhe vipi. Umelala hadi muda huu?” akaniuliza.

“Ndiyo nilikuwa najiandaa kutoka. Habari ya tangu jana?”

“Nzuri, sijui wewe?”

“Mimi sijambo. Ndiyo umekuja kunivuta?”

“Si nilikwambia jana nitakuja!”

Nikanyamaza kimya. Kwa kweli nilisikia aibu.

“Sawa,” nikamwambia.

“Lakini ulijaribu kuliwasha tena?”

“Sijaliwasha. Haliwezi kuwaka bila kupelekwa kwa fundi.”

“Hebu nipe funguo nilijaribu.”

Nikampa funguo ya gari hilo.

Msichana alifungua mlango wa gari akajipakia na kuliwasha. Gari liliwaka mara moja kama ambalo halikuwa na tatizo. Nikashangaa.

“Si hili limewaka!” akaniambia.

“Sasa nikwambie kitu, hili gari si langu. Nilikuwa nimeliazima na nilitakiwa nilirudishe kwa mwenyewe asubuhi hii. Kama limewaka nashukuru Mungu.”

Msichana alishuka kwenye gari hilo.

“Basi lipeleke lisije likakugomea tena.”

“Nakushukuru sana. Acha nilipeleke,” nilisema na kusita kidogo kisha nikaongeza.

“Unaonaje tukutane Maimun Hotel saa saba mchana nikupe lunch?”

“Sawa.”

“Unaishi wapi?”

“Tutakuja kuzungumza.”

“Sawa.”

Msichana akajipakia kwenye gari lake na kuondoka. Na mimi nikajipakia kwenye gari hilo na kuondoka.

ITAENDELEA…

====

Usipitwe na Matukio, Download na Install ==> Global Publishers App

Daktari Achezea Kipigo Baada ya Kubambwa LIVE Akipokea Rushwa

Leave A Reply