The House of Favourite Newspapers

Shoga Penye Kuku Wengi Hapamwagwi Mtama!

0

LEO sitaki uniulize, Anti Naa sijui hujaanza na salamu, sijui nimeamkaje na tena uishie hapohapo! Kuna jambo mwenzenu limenifika hapa! Kama chafya ikikubana lazima uiachie shoga siyo kujibanabana uongo? Hivi kuna faida gani kuolewa wakati nawe una hamu zako?

 

Unaniangalia? Niangalie sana, mimi nasema bila aibu, nasema kama mtu anayetaka kubanja kwa bahati mbaya likamtoka! Kama ulijua nitakuogopa kwa taarifa yako sikuogopi wala sikuonei haya usiyejua vibaya. Kisa cha kumuuzia mumeo mbuzi kwenye gunia, kama una pepo la ngono ndo’ unakwenda peku? Inaudhi kweli sisi wanawake wakati mwingine sijui tuna akili ya kushikiliwa!

 

Mnaniudhi, si bora ungekuwa changudoa tukajua moja kuliko kuwa mke mwenye akili kama punda wa dobi asiye na moyo wala masikio. Kabla ya kuolewa watu wamefanya michango, sherehe zaidi ya tatu sijui, send off, kitchen party na sherehe kamili.

 

Lakini huna moja, macho kama kuku wa kizungu aliyetoroka bandani na kutoka nje kila kitu anataka kukitazama. Hee heeiyaa unaloooo! Wanawake ninyi mmerogwa na nani au tukubaliane na usemi kwamba mwalimu wetu kipofu, sitaki kukubaliana na maneno haya ndo’ maana leo kuna wanawake wanaongoza wanaume kwa mafanikio makubwa.

 

Haya sasa tulikuwa tunafanya siri leo tunaumbuka tulikuwa tukiwabambikia watoto waume zetu kwa kisingizio mtoto anafanana na bibi mzaa bibi, Shuu! Wapi na wapi, mimba atie mwingine mtoto afanane na bibi mzaa bibi inahu!, leo hii vipimo vya DNA vinatuumbua mjini, tumebaki matumbo joto!

 

Nakuona moyo unakupiga kama mdundo wa ngoma za asili, upo? Lazima ushtuke mumeo akishtuka ndoa huna dada, huyo si mwanaye japo tunajua lakini hatuwezi kuingilia ndoa yenu.

 

Kipimo cha ‘DNA’ kitatambua vinasaba kitaharibu kila kitu, lakini najua kila mwanadamu hakosi kufanya kosa kwa vile ndivyo Mungu alivyotuumba.

Lakini makosa mengine ya kijinga tena ya kihayawani, umetoka nje ya ndoa, hilo ni kosa kubwa ambalo likigundulika huna ndoa, umefanya kosa lile bado unaona ufahari unakwenda pekupeku, hii akili matope?

Halafu wasomi si ndiyo wanaofahamu siku za hatari kwa mwanamke kupata ujauzito? Lakini hao ndiyo wamekuwa wa kwanza kujiachia na kubeba mimba na kukimbilia kuzitoa.

Jamani eeeh, mwenye masikio asikie, mpira si kwa ajili ya ukimwi tu hata kuzuia mimba pia kukulindia afya yako na magonjwa ya kuambukiza ya zinaa, upo? Basi jamani wakati mwingine tuwaonee huruma waume zetu kama tumeteleza kutoka nje, tusikubali kufanya ngono hatarishi, haya mimba unazaa, ukimwi je?

 

Haya umevuka salama umetoka nje ya ndoa hukutumia mpira na hukuathirika, lakini DNA inaonesha mtoto uliyembambikia mumeo si wake. Sijui umlaumu nani, hebu acheni kututia aibu wake za watu kukosa uaminifu hata akili ya kutumia kinga hamna.

Waswahili wanasema kuku mgeni hakosi kamba mguuni, sasa endelea kuwa kuku mgeni uliyeolewa kila kukicha kutanga na kamba mguu kwa waume za watu na wakikupatia mimba unakimbilia kutoa.

Shoga naona kama kichwa chaanza kunigonga maana si kwa mashushu haya ya leo, shuuuutuuuuu!

Kwa leo niishie hapa, tukutane tena wiki ijayo. Kumbuka ulikuwa nami Shangingi Mstaafu, Anti Naa.

Leave A Reply