The House of Favourite Newspapers

Mwanaume Aliyepandikizwa Moyo Wa Nguruwe Afariki Dunia

0

Mwanaume aliyeingia kwenye rekodi ya kuwa binadamu wa kwanza kupandikizwa moyo wa nguruwe, David Bennett Sr amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 57, ikiwa ni miezi miwili tu tangu alipofanyiwa upasuaji huo.

Bennett alifanyiwa upaji huo ulioishangaza dunia, januari 7, 2022 katika Hospitali ya Maryland Medical Centre, Baltimore nchini Marekani na kuingia kwenye rekodi ya binadamu wa kwanza kupandikizwa kwa mafanikio moyo wa nguruwe.

Bennet alifariki Jumanne ambapo hospitali iliyokuwa ikifuatilia mwenendo wake baada ya upasuaji huo, haijaeleza chanzo cha kifo chake ingawa taarifa inaeleza kwamba hali yake ilianza kubadilika siku chache kabla ya kifo chake.

Taarifa zinaeleza kwamba baada ya madaktari kubaini kwamba isingewezekana kwa Bennett kuendelea kuishi, ndugu na jamaa zake walipewa taarifa na kumtembelea hospitalini hapo ambapo waliendelea kukaa naye mpaka alipofikwa na mauti.

Dokta Bartley Griffith ambaye ndiye aliyeongoza upasuaji huo wa kumpandikiza Bennett moyo wa nguruwe, ametoa taarifa akieleza masikitiko yake baada ya kifo cha mwanaume huyo na kueleza kwamba alikuwa mjasiri na mwenye uthubutu katika kupigania maisha yake mpaka hatua ya mwisho.

“Tunatoa pole kwa familia lakini pia tunamshukuru kwa uthubutu wake wa kihistoria wa kukubali kufanyiwa upasuaji huu ambao umefungua milango ya utafiti mkubwa zaidi katika fani ya upandikizaji wa viungo vya wanyama wengine kwenye mwili wa binadamu,” amekaririwa Muhammad Mohiuddin ambaye ndiye mkuu wa kitengo cha programu ya upandikizwaji wa viungo vya wanyama kwa binadamu.

Kabla Bennett hajafanyiwa upasuaji huo, hali yake ya kiafya ilikuwa mbaya ambapo ilishindikana kupandikizwa moyo wa binadamu katika hospitali hiyo, ndipo madaktari walipokuja na wazo hilo.

Siku za mwanzo baada ya upasuaji, afya ya Bennet iliimarika vyema na kuwashangaza wengi ambapo kwa wiki kadhaa, hakuonesha dalili zozote ambazo zingeashiria kwamba seli za mwili wake zinaushambulia moyo huo na aliweza kuendelea na maisha kwa kujumuika na wanafamilia.

Leave A Reply