The House of Favourite Newspapers

Mwezi Mtukufu Kusawazisha Penzi Lako!

0

NA GABRIEL NG’OSHA | IJUMAA WIKIENDA | XX LOVE

SIMU; +255 679 979 785 

NINA kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuzidi kutupigania kila kukicha, lakini pia nikupe pole wewe msomaji wa safu hii ya XXLove kwa magumu yote unayoyapitia katika maisha yako.

Kupitia safu hii, napenda kuwatakia mfungo mwema Waislam wote kwa kipindi hiki cha toba katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Leo naomba kukukumbusha msomaji ambaye uko kwenye Mfungo wa Ramadhani juu ya kuutumia vyema mfungo ili kurekebisha ndoa yako, hata kama hujafunga, lakini nawe unaweza kujifunza kitu kupitia makala haya.

Kama unafunga kwa lengo la kutubu dhambi zako, unafunga ili kutengeneza uhusiano wako na Mungu uwe mwema na imara. Kama unafunga ili kufanya toba, basi hakikisha pia sehemu ya mfungo wako unaitumia katika kusafisha, kurekebisha na kuboresha ndoa yako.

Kama ulikuwa husemeshani na mwenza wako, basi msemeshe sasa kwa umuhimu wa mwezi huu wa toba na hakika atakusikiza, kaa naye chini, muangalie namna ya kumaliza tofauti zenu kwani hakuna maana kama utakuwa umefunga, lakini hakuna uelewano na mwenza wako, kama hamjamaliza tofauti zenu.

Ndoa nyingi zinakumbwa na misukosuko ya hapa na pale, wengine wanatukanana, wanapigana, wanaachana na kurudiana, wanasengenyana, wanasalitiana na kadhalika. Sasa muda huu wa toba ni wa kujiweka mikononi mwa Mungu ili kuiweka sawa ndoa yako.

Ni kweli miezi 11 yote umepewa nafasi ya kufanya ufanyayo, lakini Mungu, kwa sababu ya upendo wake, amekupa mwezi mmoja wa kufanya toba, basi itumie toba hiyo katika

 kweli ili ikuondolee mabalaa yote kwenye ndoa yako.

Mungu akuepushe na changamoto kwenye ndoa yako, akuepushe na kejeli, majigambo, dharau na chuki dhidi ya ndugu wa mumeo au mkeo, akupe moyo wa imani na upendo kwa ajili ya familia yako na watu wote wanaokuzunguka.

Mungu akupe busara kipindi hiki ili uweze kuitumia katika ndoa yako, kwani nina uhakika umekuwa ukisikia, ukisoma au ukiona ndoa nyingi zimeingiliwa na ibilisi kiasi cha wanandoa kutoana roho, kujinyonga kwa sababu ya mifarakano ya kifamilia na wengine kufungwa jela kwa sababu tu za mitifuano kwenye ndoa zao.

Ndugu zangu, muda huu ambao umepewa kwa ajili ya toba, basi tubu kweli na utumie Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kusawazisha mabonde yote ambayo umekuwa ukihisi kuwa ni chanzo cha migogoro kwenye ndoa au uhusiano wako.

Kwa sababu una nafasi ya kukaa na mweza wako, kuzungumza na hata kufurahia pamoja, usiogope, mwambie kuwa hukumuoa ili mje mgombane, hukumuoa ili mje mkwaruzane, mtupiane vyombo nje, mrudishane nyumbani mkiwa na manundu.

Bali mlipendana na kuamua kuishi pamoja ili kutengeneza familia bora na yenye upendo.

Kwa ushauri na maoni, tembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Ijumaa Wikienda kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Insta:@mimi_na_uhusiano au jiunge na M&U WhatsApp kwa namba zilizopo hapo juu.

Leave A Reply